Habari

Ratiba mashindano ya Qur’an Ramadhan hadharani

Taasisi maarufu katika uandaaji wa mashindano ya Qur’an nchini, zimetangaza ratiba zao za mashindano ya Qur’an katika msimu huu wa Ramadhan unaotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Machi 2025.

Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, (SMZ) Dkt Hussein Mwinyi, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, wanatarajiwa kuwaongoza maelfu ya Waislamu katika mashindano makubwa ya kusoma Qur’an kwa njia ya Tajweed yaliyoandaliwa na Khidmatul Qur’an yatakayofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere uliopo jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa mashindano hayo, Iddi Abdallah Chudi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa mashindano hayo yatashirikisha washindani kutoka mataifa 12, yakiwamo Afrika Kusini,  Pakistan, Lebanon, Iraq, Afghanistan, Uturuki, Malaysia, Morroco, Yemen, Mali, Egypt, Indonesia na Tanzania ambayo itatoa washiriki wawili

Ustadh Chudi alisema zawadi za mashindano hayo kwa mwaka 2025 hazina mabadiliko na zile za mwaka jana, ambapo mshindi wa kwanza atachukua dola 5,000, wa pili dola 3000 na wa tatu dola 2000.

Ustadh Chudi amewashauri Waislamu wasipange kukosa katika mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika Machi 15, 2025, kwani ni ya kipekee na hakuna mahala pengine wanapoweza kuyaona.

Alisema, Jaji Mkuu wa fainali hizi, anatarajiwa kuwa Haafidh wa Kimataifa, Sheikh Yassir Sharqaw. Naye Jaji Mkuu wa kimataifa wa mashindano yote hapa Tanzania na Imam Msaidizi wa Msikiti wa Mtoro, Sheikh Abdallah Al-Mundhir atakuwa miongoni mwa majaji.

Majaji wengine ni Sheikh  Alhabib Swaleh Al-Ahdar na Dkt Abdulmanan Hassan.

Mashindano ya Aisha Sururu

Kwa mujibu wa ratiba, mashindano mengine yanayotarajiwa ni yale ya Aisha Sururu yatakayofanyika Machi 9, 2025 katika ukumbi wa Diamond Jubilee, uliopo  jijini Dar es Salaam.

Mchujo wa awali wa mashindano hayo utafanyika Machi 8, 2025 kwenye ukumbi wa City Garden ambapo mgeni rasmi na zawadi katika hatua hiyo bado havijatangazwa.

Mwaka jana, katika fainali kama hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, washindi wa kwanza wa juzuu 30 upande wa wanawake na upande wa wanaume walipewa zawadi ya nyumba.

 Pia Rais Samia alitoa kiasi cha Sh 10 milioni ambazo ziligawanywa kwa washindi hao wa jumla.

Al-Hikma Foundation

Baada ya mashindano ya taasisi ya Aisha Sururu, yatafuata Mashindano ya Kimaitaifa ya Afrika yanayoandaliwa na taasisi ya Al–Hikma Foundation chini ya rais wake, Sheikh Abdulqadir Al-Ahdal na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Sheikh Nurdin Kishk.

Kwa mujibu wa Sheikh Kishk, fainali ya mashindano ya Qur’an Tukufu ya Afrika Mashariki itafanyika Jumapili ya Machi 16, 2025 kuanzia saa 12 hadi saa sita mchana, katika uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Mashindano mengine

Mashindao mengine ambayo yatafanyika katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan ni,  pamoja na yale yanayoandaliwa na taasisi ya Raudhwa iliyopo Temeke ambayo yatafanyika Jumamosi ya Machi 8, 2025. Mashindano haya yatafanyika katika Ukumbi wa Yemen schools (DYCCC HALL)

Vilevile yapo mashindano ya As-haabul Kahfi yanayotarajiwa kufanyika Machi 8, 2025 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Posta, Annujuum yatakayofanyika Machi 2, 2025 na mashindano ya wilaya ya Ilala yanayoandaliwa na taasisi ya Faraja Islamic Foundation yanayotarajiwa kufanyika Machi 2, 2025.

Pia mashindano ya Qur’an Afrika Mashariki yanayoandaliwa na Manahil yatafanyika Machi 08, 2025.

Mashindano mengine ni yale yanayoandaliwa na Umoja wa Shule za Kiislamu Tanzania (TIPSO)  yatakayofanyika Machi 22, 2025 katika ukumbi wa DYCCC Vilevile, Machi 22, 2025 kutakuwa na mashindano ya Qur’an kwa njia ya Tajweed kwa upande wa wanawake yakiandaliwa na Ummu Salama Madrasa na yanatarajiwa kufanyika katika jengo la Mayfair Hall, jijini Dar es Salaam.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button