Habari

Mufti ahimiza uadilifu, huduma bora taasisi za Hijja

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, amewataka wamiliki wa taasisi za Hijja hapa nchini kutanguliza uadilifu na huduma bora kwa wateja ili kuongeza idadi ya mahujaji hapa nchini.

Mufti alitoa rai akizungumza na wamiliki wa taasisi za hijja katika mkutano uliolenga kuangalia namna wanavyoweza kuongeza idadi ya mahujaji mwaka huu.

“Ipo taasisi moja iliharibu. Waziri Mkuu alikuwa anafika mara kwa mara ofisini kwangu, serikali yote ilihamia hapa. Hata hivyo, nilijitahidi kumsaidia mhusika asipate matatizo ya kumuangamiza. Lazima mfahamu kuwa kazi mnayofanya ni hijja, sio biashara. Hakikisheni kuwa kazi mnayofanya inafuata misingi yote anayoiridhia Mwenyezi Mungu.” alisema.

Sheikh Zubeir aliongeza kusema kuwa anatamani kuona Tanzania bara inaongeza idadi ya watu wanaokwenda kutekeleza ibada hiyo, na ili kufikia azma hiyo n lazima kujitathmini na kuchukua hatua kwa sehemu ambazo hawajafanya vizuri kwa mwaka 2024.

Pia Sheikh Zuberi alitoa maelekezo kwa taasisi hizo kutumia njia mbalimbali kuhamasisha watu kwenda hijja kwa kueleza kwa kina juu ya ratiba za ibada hiyo.

Kwa mujibu wa Mufti, taarifa kutoka Wizara ya Hijja ya Saudi Arabia zinasema mikataba yote kwa ajiri ya shughuli za hijja itafungwa Februari na hivyo ni lazima watu wakaelezwa ukweli ili waharakishe mchakato.

Katika hatua nyingine, Sheikh Abubakar Zubeir amehimiza wanaotaka kwenda hijja kwa mwaka 2025 wajitahidi kujisajili mapema ili kuenda sambamba na ratiba ambayo tayari imeshatoka

“Msisubiri mpaka mwezi wa Ramadhan. Jipangeni sasa hivi. Mkichelewa kulipia mtajikuta mnashindwa kwenda hijja katika wakati muafaka na kujikuta mkisafirishwa mwakani. Tunawahimiza mahujaji na wanaotamani kulipia mahujaji kwenda hijja kufanya zoezi la kujiandikisha mapema. Mikataba inafungwa mwezi wa pili hivyo hakuna muda utakao ongezwa,” amesema.

Taasisi zilizokidhi vigezo

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uratibu wa Hijja Tanzania, Sheikh Musa bin Hemed bin Jumaa alizitaja taasisi zilizokidhi vigezo na kuruhusiwa kufanya kazi ya kupeleka mahujaji kwa mwaka 2025 kuwa ni Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Ahlu-Daawa, Jamaarat, Peace Travel, M2 travel, Ibn Batuta, Zamzam Centre, Muslim Hajj Trust, Alhusna Hajj Trust na Manaski Hajj. Nyingine ni Masjid Al-dir, Furkaan Hajj and Umra, Ajuwa Hajj and Travel agency, Al-Hashm agency for Hajj and Umra, Safwa Travel, Atwaif Hajj and Umra, Rawdha Hajj and Travel Agency, Muswafi Hajj, Alhubeity Hajj and Umra, Masjid Jabar Hilla, Itravel Hajj and Umra

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button