Gazeti imaan

Tusikubali maridhiano yanayodhoofisha dini yetu!

Neno ‘Hikmah’ (busara) limekuwa likipotoshwa kwa muda mrefu. Lina maana ya kuwaendea watu katika njia bora zaidi inayowezekana au kufanya mambo kwa namna inayofaa zaidi kwa kuzingatia hali halisi.

Haijawahi kumaanisha kuleta sura potofu ya Uislamu kwa ajili ya maslahi binafsi au hata ya jamii. Waislamu tutakapokuwa tayari kulegeza msimamo wa dini yetu katika vipengele vyote vya maisha yetu, basi tunapoteza neema za Allah ‘Azza wa Jallah’, tunaonesha udhaifu mbele ya maadui zetu na kupoteza heshima mbele ya Muumba wetu.

Kibwagizo maarufu cha kizazi cha leo ni neno ‘compromise’ (kuridhiana). Watu dhaifu wanaliona neno hili halina madhara, wajinga wanalikumbatia kama lenye faida, na wale waliopotoka wanalihesabu kama muhimu. Hitimisho hilo linaweza kuonekana ni msimamo mkali lakini huo ndiyo uhalisia.

Katika Uislamu, hakuna kabisa mwanya wa ‘compromise’. Sisi tunaridhiana na jamii nyingine katika mambo yanayompendeza Mwenyezi Mungu tu na siyo kinyume chake, na hiyo kwetu siyo ‘compromise’ kama inavyofahamika na wengi leo.

Hakuna ushahidi kwamba Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwahi kufanya hivyo, wala Maswahaba wake walifanya hivyo, au Qur’an imetoa nafasi kwa ajili hiyo. Msimamo huu unaleta mantiki kwa wale wanaozama kwa kina zaidi.

Mtu anayeugua ugonjwa wa moyo atakuwa mpumbavu iwapo atachagua kutumia nusu ya dawa alizoandikiwa, halafu akaamua kumeza vidonge vya sukari kama mbadala wa dawa zilizobaki. Anamdanganya nani?

Siyo daktari, ambaye alitafuta ufumbuzi bora wa ugonjwa wake, wala mfamasia aliyegawa kwa usahihi dawa zilizoandikwa na daktari. Bali mgonjwa mwenyewe ndiye atakayekuwa amekula hasara.

Kwa hakika, Allah ‘Azza wa Jallah’ katika hekima yake na rehema amechagua Uislamu kama dawa ya magonjwa ya wanadamu na jamii tunayoishi. Uislamu ni tiba kwa saratani ya riba, migogoro ya kisiasa, unyanyasaji kwa wanawake, migawanyiko ya kijamii, na hulka ya mwanadamu na matamanio yake yasiyotosheka.

Kwanini tunakubali kuridhiana?

Inaonekana kuna sababu kuu tatu kwanini watu wanaamua kukubali kuridhiana (compromise) kwa kulegeza msimamo wa Kiislamu. Sababu ya kwanza, watu hawa huwa wanasema, “Unajua tunaishi katika nyakati ngumu, katika jamii ngumu, na kwamba Allah anaturuhusu kulegeza msimamo kwa sababu Uislamu ni mwepesi, wala siyo mgumu.”

Na hadith inayonukuliwa ni ile iliyosimuliwa na mama Aisha (Allah amridhie) ambaye alisema, wakati Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alipolazimika kuchagua kati ya vitendo viwili, basi alichagua kilicho rahisi zaidi.

Ni kweli, Uislamu ni rahisi kuufuata, lakini siyo kwa kiwango ambacho tunaruhusiwa kubadili sheria na kanuni zilizowekwa na Allah ‘Azza wa Jallah’ ili kujiwekea urahisi. Wakitakiwa ushahidi wa kauli kwamba tunaweza kulegeza msimamo wa Kiislamu, wanadai kwamba hali yetu leo ni kama ile ya Makka kipindi cha Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Wanadai tunapaswa kuwa wavumilivu kama alivyofanya Mtume na kuchukua hatua kama alivyofanya katika mazingira yale. Upotofu wa hoja hiyo uko wazi kabisa tukitafiti sababu hasa za kwanini Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alifanya vile wakati ule Makka, na vipi baadaye katika maisha yake alifanya tofauti.

Sasa tunaishi katika zama za Madina, zama ambazo Qur’an imekamilika. Kipindi cha Makka kinaweza kuonekana kama cha mpito, ambapo Maswahaba walipewa mafunzo na kutayarishwa katika mazingira yale maalumu.

Lakini Uislamu ulikamilika, ukimalizia na aya hii: “Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe Dini yenu.” [Qur’an, 5:3]. Uislamu ulishakamilika, kwa hiyo kuturudisha nyuma mpaka zama za Makka ni jambo lisilo na mantiki.

Kikombe cha maziwa safi kitaharibika iwapo tone moja tu la mkojo litadondokea ndani yake. Allah ‘Azza wa Jallah’ hajawahi kutuamrisha kufanya mambo yaliyo nje ya uwezo wetu ili kumridhisha.

Kwa hiyo, hoja za kigonjwa kama “Lazima nifanye kazi katika mazingira ya haramu kwa sababu sina chaguo lingine”, ni hoja isiyo sahihi. Iwapo wanawake wetu lazima wachanganyike na wanaume mahala pa kazi katika kiwango kisichofaa, Mwenyezi Mungu hakuwahi kuwaamrisha wafikie kiwango hicho.

Tukila chakula ambacho kimetajwa kuwa ni haramu, tusitarajie msamaha wa moja kwa moja, kwa sababu hakuna kisingizio kinachobaki hapo, tumechupa mipaka ya Mwenyezi Mungu.

Wakati watu wengi wanapenda kutumia akili zao kuthibitisha madai yao dhaifu, Mwenyezi Mungu anasema hivi: “Basi huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu wa haki. Na kipo kitu gani baada ya haki isipokuwa upotovu tu.” [Qur’an, 10:32]. “Haiwi kwa Muumini mwanaume wala Muumini mwanamke kuwa na hiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi.” [Qur’an, 33:36].

Unadhani hali yetu ya sasa ni ngumu zaidi kuliko vile alivyoteseka Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na Maswahaba wake, au Mitume wengine waliotangulia kabla yake? Hakika hii ni kanuni ile ile iliyoamrishwa juu ya Mtume na juu yetu.

Nabii Yusuf (amani ya Allah imshukie) alipitia mateso mengi lakini hakusalimu amri wala kulegeza msimamo, bali alimgeukia Muumba wake akasema: “Ewe Mola wangu! Napendelea kifungo kuliko haya anayoniitia.” [Qur’an, 12:33].

Haikuwa katika asili ya Yusuf (amani ya Allah imshukie), wala Mtume mwingine yeyote, wala katika waja wema wa Mwenyezi Mungu kulegeza msimamo wa kidini kwa lengo la kupata manufaa ya dunia. Nabii Yusuf alihiyari kwenda jela kuliko kusalimu amri kwa tamaa za wanawake.

Sababu ya pili, kuna hoja nyingine potofu: “Tunataka kuwaonesha watu dini ambayo ni rahisi na haihitaji nguvu kubwa. Hatutaki kuwafanya watu waukimbie Uislamu.”

Kiukweli, watu wamekuwa wakiukimbilia Uislamu kila wanapooneshwa mwanga wake halisi, kwa sababu Uislamu unatoa ufumbuzi wa matatizo mbalimbali, ufumbuzi ambao wamekuwa wakiutafuta. Hawataki mseto wa Uislamu na Ukafiri walioukimbia.

Kuuonesha Uislamu katika vigezo vyake vya uwastani na ulaini peke yake huleta picha potofu ya dini ambayo tayari imeshakamilika.

Hoja ya tatu huwa wanasema, “lazima tulegeze msimamo wa kidini (compromise) ili kuimarisha Uislamu. Lazima tuingie na kujiunga na taasisi zile, tuwaunge mkono wasio Waislamu ambao ni washirika wetu katika maisha haya bila ya kuchunga mipaka ya dini yetu. Basi kwa njia hii tunaweza kueneza Uislamu na hivyo kuishi kwa furaha baada ya hapo.’ Kosa!

Kwa mara nyingine, hakuna ushahidi katika shariah isipokuwa kinyume chake. Sura ya al–Kaafiruni (Qur’an, 109:1–6) ni mfano mkubwa wa hilo: “Sema: Enyi makafiri! Siabudu mnachokiabudu, wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Wala sitaabudu mnachoabudu. Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu.”

Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) alitangaza kwamba dini yake ni ile ya Ibrahim (amani ya Allah imshukie). Makafiri nao wakaleta hoja kwamba hakuna sababu ya wao kuacha imani yao na kushika ile ya Muhammad, wakiona kwamba wote walikuwa dini ile ile.

Walitafuta maelewano (compromise) na Mtume wakipendekeza kwamba asujudie miungu yao ili na wao wamsujudie Allah ‘Azza wa Jallah’, na kwamba baada ya hapo angeweza kudai chochote anachotaka kutoka kwao.

Sura hii iliteremshwa kwa sauti isiyo na maelewano (uncompromising tone) ikitenganisha wazi tauhidi kutoka kwenye shirk na kuweka kigezo cha kweli cha jinsi ya kuangalia mambo haya bila ya kuruhusu mabishano zaidi. Hayo hayakuwa mazingira pekee.

Baba zake wadogo Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) walipohisi kwamba Mtume anazidi kupata nguvu walijaribu kumhonga zawadi mbalimbali za hapa duniani.

Walimpa uongozi wa Makka, utajiri kama hilo ndiyo lengo lake, mke mrembo zaidi kama hilo ndilo linalompendeza, lakini alikataa yote hayo kwa sababu alitamani tu haki itawale katika jamii.

Katika mazingira hayo magumu na yenye ushawishi mkubwa, Mtume alisema kwamba hata kama jua lingewekwa mkono wake wa kulia na mwezi mkono wa kushoto, kamwe asingeacha harakati hizo mpaka Mwenyezi Mungu azinyanyue au afe akiwa katika jitihada za kufanikisha hilo.

Hii ilikuwa ni fursa kubwa kwake kama ingekuwa ni hulka yake kulegeza msimamo (compromise), kwamba angeweza kukubali uongozi huku akificha imani yake ya kweli na baadaye akaeneza Uislamu baada ya kuwa na nguvu za kutosha.

Mtume alijulikana kama Mwaminifu na kutokana na ukweli huu, alikuwa na uwezo wa kuwasha moto wa uzalendo wa Kiarabu na kuwaunganisha Waarabu wote chini ya mwamvuli huo. Waarabu wote wangemuunga mkono kwa sababu ya kuchoshwa na vita vyao vya kikabila.

Baada ya hapo, Mtume angeweza kuzikomboa ardhi zote za Waarabu kutoka utawala wa Warumi na Waajemi. Angeweza kuunda dola ya Waarabu kwa urahisi zaidi kupitia njia hii badala ya kuvumilia miaka 13 ya tabu na mateso.

Angeliweza awali kuwafanya watu waipigie magoti mamlaka yake, kisha angeliweza kutumia nafasi yake ya mamlaka kupandikiza imani ya tauhidi, na kuwafanya watu wamuabudu Mungu wa Kweli. Lakini hivyo sivyo Allah ‘Azza wa Jallah’ alivyotaka, na huo siyo Uislamu.

Uislamu unatafuta kubomoa aina zote za uovu kupitia njia safi, siyo kufanya ujanja wa uovu ili kufikia lengo safi. Hiyo haiwezekani na wala hairuhusiwi.

Hata katika hali ya kufa au kupona, tunaambiwa kuhusu malipo tutakayopata iwapo tutajitahidi na kuvumilia kwa subira. Nabii Ibrahim (amani ya Allah imshukie) alichagua kuchomwa kwenye moto ulioandaliwa na baba yake mwenyewe, kuliko kuficha dini yake, kukimbia eneo lile, au kuacha kueneza neno la Mwenyezi Mungu.

Ikiwa Allah ‘Azza wa Jallah’ au Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) wametukataza kufanya kitu, lazima tuamini kwa nguvu zetu zote kwamba jambo hilo limekatazwa kwa manufaa yetu.

Kwa mfano, muziki ni haramu. Usijaribu kugeuza maneno ili kukidhi matamanio yako. Kama Mtume amekataza, basi kubali tu, usijaribu ‘kuusilimisha’ kwa kuleta kisingizio hiki na kile.

Mfano mwingine ni suala la hijab. Dada zetu wengi wamejaribu hata ‘kuisilimisha’ hijab, vazi ambalo Mwenyezi Mungu mwenyewe ameliwekea miongozo! Wanataka kuvaa hijab zinazoendana na fasheni kwa kutumia hoja dhaifu sana kama hii, “Lakini, kama tukiendana na fasheni, wasio Waislamu hawataona ugumu kushirikiana nasi.” Kosa!

Allah ‘Azza wa Jallah’ anasema ndani ya Qur’an: “Hawatakuwa radhi nawe Mayahudi wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao. Sema: Hakika uongofu wa Mwenyezi Mungu ndiyo uongofu hasa. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya ujuzi uliokujia, hutapata mlinzi wala msaidizi kwa Mwenyezi Mungu.” [Qur’an, 2:120].

Hakuna kisingizio

Alhamdulillah, tumeruzukiwa mahitaji yote muhimu ya maisha. Tuna fedha za kutosha kununua bidhaa ‘Halal’ na hizi zipo kila mahali. Kwa hiyo hatuhitaji kulegeza msimamo wa dini yetu kuhusu chakula chetu. Tunaweza kuvaa kwa uhuru nguo zinazotakiwa na Mwenyezi Mungu, kwa hiyo hatuna kisingizio cha kutofanya hivyo.

Dada zetu hawahitajiki kuchanganyika na wanaume katika kiwango kisichofaa kwenye vyuo vyetu vikuu au mahali pa kazi, kwa sababu Allah ‘Azza wa Jallah’ hakuwataka kulegeza msimamo wa Uislamu ili kupata elimu ya kidunia.

Tunaweza kuchagua kazi yetu, washirika wetu, mtindo wetu wa maisha, na bado tukajiona tunapigana Jihad ya kufikirika ya nafsi. Kwa hakika, hatukuwa na udhuru wakati ule, na wala hatuna sasa, kwa hiyo shikilia njia yote aliyoichagua Mwenyezi Mungu.

Hii ndiyo namna pekee tunayoweza kujiondoa kwenye shimo hilo bovu tulilotumbukia. Bila shaka tutaanguka kwa kumhusisha Mwenyezi Mungu na maagizo ambayo hakuwahi kuyatoa: “Sema: (Ewe Muhammad): Hii ndiyo Njia yangu – ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua mimi na wanaonifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.” [Qur’an, 12:108]. “Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyonyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia Yake. Haya amekuusieni ili mpate kumcha Mungu.” [Qur’an, 6:153].

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button