
Sheikh Ruga, mwanasafu wa Gazeti Imaan aliyeibuka mwanafunzi bora SUMAIT
Januari 25, 2025 huko Zanzibar, Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-Sumait kilichopo wilaya ya Magaharibi B” Chukwani Zanzibar, kilifanya mahafali yake ya 24 ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.
Pamoja na wanafunzi kuhitimu katika mahafali hiyo, zawadi zilitolewa kwa wanafunzi bora, waliofanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho. Mmoja wa wanafunzi aliyebahatika kupokea zawadi kutoka kwa Rais, Dkt Mwinyi, ni mwanasafu wa Gazeti Imaan, sheikh Seif Ruga aliyehitimu chuoni hapo Shahada ya Uzamili katika Sharia na Sheria ya Kiislamu.
Simulizi ya sheikh Ruga inashangaza kidogo kwani si mtu aliyepita katika mifumo ya elimu iliyozoeleka ya kidato cha nne na cha sita. Gazeti Imaan limezungumza na Ruga na kumuuliza kuhusu safari yake ya kielimu, amewezaje kufikia mafanikio hayo na matarajio yake kwa ujumla. Mazungumzo yetu yalikuwa kama ifuatavyo.
Gazeti Imaan: Seif Ruga ni nani, na tupe historia yako japo kwa uchache
Seif Ruga: Seif Ruga ni mwandishi wa vitabu. Kielimu, nilipata elimu yangu ya msingi katika Shule ya Msingi Manza iliyopo wilaya ya Mkinga mkoani Tanga. Nilipata elimu yangu ya msingi katika dini Madrasat Al-Shamsiyya (TAMTA), Tanga. Baada ya hapo nilifika jijini Dar es Salaam na kujiunga na shule ya Alharamain iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam kuendelea na elimu ya dini.
Nikiwa Al Haramain, nilisoma kwa muda wa miaka mitatu ngazi ya Mutawasitwa (sawa na sekondari), kisha nikaelekea nchini Saudi Arabia katika Chuo Kikuu cha Madina ambapo niliendela na elimu ngazi ya thanawi (sawa na kidato cha sita katika elimu ya sekyula).
Katika Chuo hicho cha Madina nilisoma kwa miaka saba; kati ya hiyo, mitatu ilikuwa ngazi ya thanawi na minne ngazi ya Shahada katika Kitivo cha Sharia ambapo nilihitimu mwaka 2001 na kurejea Tanzania.
Gazeti Imaan: Tunajua kuwa kuna changamoto kwa mamlaka za kielimu kutambua shahada za nje za dini ilhali hujasoma sekondari. Wewe ulifanyaje hadi ukatambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na sasa umehitimu Shahada ya Uzamili hapa nchini?
Seif Ruga: Simulizi ya elimu yangu kidogo ni tofauti na za wengine. Mimi sikupita katika njia hizi za kawaida, kwa maana ya kujiunga na kidato cha kwanza hadi cha nne na kuendelea kidato cha tano na sita. Baada ya kumaliza ngazi ya Matawasitwa (sekondari ya dini) pale Alharamain nikajiunga na Chuo Kikuu cha Madina ambako, kama niivyotaja hapo awali, nikasoma ngazi ya thanawi kisha nikafanya shahada ya kwanza ya Shariah.
Bahati mbaya sana, shahada hii, kama ulivyodokeza, haikutambuliwa na TCU. Ikanibidi nirudi tena darasani ili kutafuta sifa za shahada yangu kutambuliwa.
Nikawa nafanya kazi shule ya Yemen huku nasoma masomo ya sekondari kwa mfumo wa QT katika kituo cha Al-Amin Islamic Centre kilichopo mkabala na Uwanja wa Taifa pale Temeke. Nilisoma kwa miaka miwili na kufaulu mitihani yangu ya mwisho ambayo iliniwezesha kujiunga na kidato cha tano na sita.
Kidato cha tano na sita nilisoma katika Kituo cha Elimu cha Wailes kilichopo Temeke karibu na kwa Aziz Ali, ambapo nilianza mwaka 2016 na kumaliza 2017 na kufaulu kwa wastani mzuri.
Baada ya hapo, nilianza kufanya harakati za kwenda TCU kwa ajili ya kuitambua shahada yangu ambayo niliipata kule Madina. Nakumbuka mwaka 2018 nilifika TCU na kulipia Tsh 100,000 kwa jili ya zoezi hilo, na nashukuru jambo lilikwenda vizuri.
Ilipofika mwaka 2022 ndipo nikajiunga na Chuo cha SUMAIT Chukwani Zanzibar kwa ajili ya Shahada ya Uzamili katika Shariah na Sheria ya Kiislamu (Master of Shariah and Islamic Jurisprudence) ambayo mpaka namaliza nilifanikiwa kuwa mwanafunzi bora kwa kupata wastani wa GPA ya 4.5.
Gazeti Imaan: Kitu gani kilikuvutia kwenda kusoma Shahada ya Uzamili?
Seif Ruga: Kilichonivutia ni kuongeza maarifa. Hilo ndiyo lilikuwa kusudio langu la kwanza kabisa. Hususan, kipekee, nilitaka kujua kwa kiasi gani sharia za Kiislamu na hizi za kisekyula zinatofautiana
Mbali na shauku ya kujua namna sheria za duniani nikilinganisha na za Kiislamu zinavyotofautiana, pia nilitaka kusaidia jamii katika eneo hilo. Mimi ni mwandishi wa vitabu, hivyo elimu inanisaidia zaidi wakati ninapoandika mada mbalimbali za kuelimisha umma.
Tanzania bado tuna shida ya ufahamu wa kanuni za kisheria, na wataalam nao siyo wengi. Kutokana na kazi yangu, elimu hii inanisaidia zaidi kuongeza wigo wa uelewa wangu.
Gazeti Imaan: Safari ya masomo yako ilikuwaje?
Seif Ruga: Kwa kweli safari ilikuwa nzito. Nimepita katika njia ngumu kiasi ambacho kama siyo moyo wa uvumilivu huenda nisingefika hapa nilipofika. Nakumbuka changamoto kubwa ilikuwa ni kutimiza majukumu ya familia na huku nikitenga muda kwa ajili ya kusoma.
Hai ilikuwa ngumu sana hasa ukizingatia nina watoto wanasoma shule ya Yemen ambapo ada pekee inafika Tsh milioni 2.5, na nilitakiwa kulipa siyo chini ya Tsh milioni 7. Wakati huohuo, natakiwa kutafuta fedha kwa ajili ya kuhudumia familia. Mambo yalikuwa yameshikana lakini yote yamekwisha na Mwenyezi Mungu akaajalia nimefanikiwa.
Gazeti Imaan: Jambo gani hutalisahau katika safari yako hii ya masomo ya Shahada ya Uzamili?
Seif Ruga: Jambo ambalo sitaweza kusahau katika safari hii ya masomo ni jinsi nilivyotaka kukata tamaa ya kuendela. Kuna kipindi nilijikuta napata ugumu kufanya maamuzi, yaani mke wangu anaumwa anatakiwa kupelekwa hospitali, na shule tayari nimeshatoa fedha zangu na nimesoma nusu mwaka.
Kulikuwa hakuna namna ambayo ningeweza kurejeshewa ada yangu ili nibaki na zoezi la kumtibu mke wangu. Kwa kweli, nilikuwa njia panda, sijui nishike njia gani. Nashukuru mke wangu alinitia moyo akaniambia endelea. Jambo la kushukuru nimemaliza, nimebakisha hili la ugonjwa wa mke wangu, na naendelea nalo.
Gazeti Imaan: Ungepewa nafasi ya kuwashauri viongozi wa dini, hasa masheikh, katika jambo la kutafuta elimu, ungewapa ujumbe gani?
Seif Ruga: Niseme tu kama Waislamu, tunatakiwa tusikate tamaa katika kujiendeleza. Nitoe wito kwa masheikh kutafuta maarifa zaidi ili kujiendeza. Qur’an na Sunna za Mtume zimesisitiza umuhimu wa kutafuta elimu, basi tufanye mambo hayo kwa vitendo
Pia, tufahamu kuwa elimu ni nyenzo muhimu sana hasa katika zama hizi ambapo vitu vinabadilika kila uchwao. Itafika wakati watatakiwa watu wenye sifa hizi, na kama watu hawatakuwepo, basi itatulazimu kwenda kuazima. Nadhani tusifike huko
Hatuwezi jua, huenda kesho watu wakahitajika serikalini au sekta binafsi, zikiwemo benki, kwa ajili ya kuhudumia watu. Ttafanya nini kama masheikh wenye sifa hizi za vyeti hawatakuwepo. Mimi Mwenyewe hamu yangu ni kuona nafika ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD), na naamini nitafika huko, inshaAllah.
Gazeti Imaan: Ulijisikiaje baada ya kutangazwa kuwa mwanafunzi bora na kupewa cheti na Mh. Rais Dkt. Mwinyi
Seif Ruga: Kwangu ilikuwa ni furaha, nililiwazika sana, Alhamdulilah.