Gazeti imaanRisala ya Allah

Mbinu za uling’aniaji za Dkt. Zakir Naik zimewashawishi wengi

Dkt. Zakir Naik ni miongoni mwa wahadhiri mashuhuri wa Kiislamu ulimwenguni anayewavutia wengi kutokana na aina ya uling’aniaji wake. Yeye amejikita zaidi katika uchambuzi wa Dini Linganifu Comparative Religion), eneo ambalo ana uzoefu nalo kwa miaka mingi akiandaa na kushiriki midahalo mingi inayohusu Uislamu na Ukristo.

Dkt. Naik, ambaye ni mzaliwa wa Mumbai nchini India alisomea shahada ya udaktari wa binadamu (Doctor of Medicine) katika Chuo cha  Utabibu cha Topiwala. Hata hivyo ameitumikia taaluma hiyo kwa miaka minne tu kabla ya kuamua kujikita katika ulinganiaji.

Uamuzi wake huo unatajwa kuwa ulitokana na yeye tangu akiwa mdogo kupenda kulingania watu hasa kwenye eneo la Dini Linganifu. Anasema kuwa alipenda sana eneo hilo kutokana na kufuatilia sana midahalo ya Marhum Sheikh Ahmed Deedat, mzaliwa wa Afrika Kusini mwenye asili ya India.

Mapenzi hayo ndiyo yalimfanya aamue kuacha kazi ya udaktari na kujikita kwenye da’awah. Uamuzi wake huo umekuwa na tija kubwa sana ulimwenguni kwani umewezesha watu wengi wasiokuwa Waislamu kusilimu; na pia kuondoa dhana potovu dhidi ya Uislamu na Waislamu duniani.

Dkt. Naik amekuwa akitumia kituo chake cha runinga cha Peace TV kutoa mihadhara yenye kutoa taswira njema ya Uislamu dhidi ya wakosoaji.

Vilevile, aina ya ulinganiaji wake umewavutia watu wengi duniani na baadhi yao kuamua kufuata nyayo zake katika utoaji da’awah hasa katika midahalo baina yake na wasiokuwa Waislamu.

Mbinu hizo zinatajwa kuwavutia Waislamu wengi kumsikiliza na kumuiga, na watu wa dini nyingine kusilimu. Miongoni mwa wafuasi wake ni Firdaus Wong, raia wa China aliyesilimu. Kwa mujibu wa andiko linaloangazia athari za Dkt. Zakir Naik nchini Malaysia lenye kichwa cha habari “Zakir Naik’s impact on Malaysia: Religion and Politics,” ni kwamba, ushawishi wa Dkt. Naik nchini Malaysia ndiyo ulisababisha Wong kusilimu na yeye kuanza kulingania watu.

Nao baadhi ya Wanazuoni wa Kiislamu wamefanya tafiti mbalimbali ili kubaini mbinu za Dkt. Zakir Naik katika utoaji wa da’awah. Mohammad Aminul Islam na Thameem Ushama waliandika andiko la kitaaluma liitwalo “Zakir Naik’s techniques in comparative Theological Discourse: Some reflections, ili kuangazia ushawishi na mbinu za Dkt. Zakir Naik katika ulinganiaji.

Andiko hilo linapatikana katika jarida la Sayansi ya Kiislamu na Stadi za Ulinganifu, toleo namba 4 la mwaka 2022. Kwa mujibu wa andiko hilo ni kuwa, Dkt. Zakir Naik amekuwa na ushawishi mkubwa kutokana na uwezo wake wa kukariri na kukumbuka kwa usahihi aya za Qur’an Tukufu pamoja na mistari ya Biblia anapokuwa kwenye midahalo ya kidini.

Pia ni tabia ya Dkt. Naik kupenda kumsikiliza kwa makini mtoa hoja na kisha kuandika kila nukta inayosemwa, hali ambayo inachangia yeye kumjibu kwa usahihi mtoa hoja.

Vile vile anatajwa kuwa, kabla ya kujibu hoja hutumia kwanza muda kusahihisha baadhi ya hoja za  mpinzani wake ili kuweka kumbukumbu sawa na kisha kumjibu mtoa hoja kwa kutumia maandiko ya dini zote, aghlabu Uislamu na Ukristo lakini wakati mwingine akitumia pia maandiko ya Kihindu, Kibudha na kadhalika.

Pia, Dkt. Naik anatajwa kuwa mvumilivu dhidi ya mpinzani wake hasa pale anapokuwa anauzungumiza vibaya Uislamu au anatoa maneno ya upotoshaji. Dkt. Naik humsubiri mtoa hoja amalize na kisha yeye kumsahihisha kwa kutumia vitabu vyote viwili, aghlab Qur’an na Biblia, ingawa pia hutumia vitabu vya dini nyingine zisizo hizo.

Mbinu nyingine ni kumheshimu mpinzani wake anapokuwa kwenye mdahalo. Hutumia maneno ya heshima kama ‘Mpendwa rafiki yangu’ badala ya kumuita majina mabaya. Hali hiyo humfanya mpinzani wake kujiona anaheshimiwa na anashindana na mtu mstaarabu. Anapokuwa anaanza kujadili mada, huhakikisha anaitendea haki kwa kutaja mfanano na tofauti iliyopo baina ya dini zote mbili badala ya kujikita kwenye utofauti tu. Mada inapokuwa kwenye mfumo wa maswali basi hujaribu kutoa majibu yenye ushawishi kutetea upande wake na kukosoa upande wa mpinzani wake.

Aidha, kitendo cha yeye kutoshika kitabu chochote anapokuwa kwenye mdahalo kinaonesha kuwa ana ufahamu wa kutosha wa kile anachokizungumza, mbinu ambayo inamfanya mpinzani wake amuogope na hata kushawishika.

Lakini pamoja na mbinu zote hizo, Dkt. Naik anasema kuwa ni Allah ndiye anayemuongoza katika utoaji wake wa da’awa kwani kabla ya kufanya mdahalo humuomba ili amuongoze. Dkt. Zakir Naik, ambaye ni miongoni mwa watetezi wakubwa wa Uislamu na Uislamu hutembelea nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kutoa mihadhara. Siku chache zijazo, ‘Insha Allah’ atatua hapa nchini kwa ajili ya mdahalo unaohusu Mtume Muhammad (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) na Yesu (Nabii Isa – amani ya Allah imshukie).

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button