Mhadhiri wa kimataifa Sheikh Fariq Zakir Naik anatarajiwa kutoa khutba ya Ijumaa, Januari 3, 2025, katika Msikiti Mkuu wa Bakwata ambao rasmi unaitwa Mfalme Mohammed VI wa Morocco, uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Aidha, Dkt Zakir Naik, gwiji katika masuala ya ulinganiaji kwa njia ya dini linganishi, naye atapata fursa ya kuongea na Waumini msikiti hapo kabla ya mwanawe huyo, sheikh Fariq, kupanda katika mimbari hiyo.
Walinganiaji hao wawili, watakuwa nchini kwa takriban wiki moja kwa ajili ya Kongamano la Amani linalojumuisha mfululizo wa mihadhara ya wazi Zanzibar na Tanzania Bara, baadhi ikimhusisha pia mke wa Dkt Naik, ustadhat Farhat ambaye atazungumza na wanawake katika mihadhara miwili tofauti, Zanzibar na Dar es Salaam.
Injinia Limbanga Mohamed, mmoja wa waratibu wa ziara ya Dkt Naik kutoka taasisi ya The Islamic Foundation iliyoleta ugeni huo, ziara ya wageni hao msikitini hapo itawakutanisha na Mufti na Sheikh mkuu wa Taznania, Abubakar Zubeir.
“Tunatarajia atakutana na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir katika msikiti Mohamed VI hapo yatazungumzwa mengi,”
alisema Limbanga.
Aidha, Limbanga alisema siku hiyo hiyo ya Januari 3. amesema kabla ya kufika katika msikiti wa Mohammed VI, Dkt Naik akiwa na sheikh Fariq na timu yao watatembelea vyombo vya habari vya Azam na kufanya mahojiano.
Imeelezwa kuwa ujio wa wageni hao ni fursa kwa Waislamu wa Tanzania hasa kwa wahadhiri wa ndani kujifunza mbinu za ulinganiaji na pia ni nafasi kwa Waislamu na watu wa dini nyingine kuongeza ufahamu wao wa dini.
Kwa mujibu wa ratiba walinganiaji hao wanataraji kuwasili Disemba 30 uwanja wa ndege wa Zanzibar kisha Disemba 31, 2024 watatoa mada katika kongamano kubwa visiwani humo.
Januari 2, 2025, wageni hao watafanya kongamano katika ukumbi wa Diamond Jubilee kuanzia saa 12 jioni hadi saa tano usiku kabla ya kumalizia kwa mkutano mkubwa utakaofanyika Januari 5 katika uwanja wa michezo wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam kuanzia saa 12 asubuhi.