Blog

Wazazi wachungeni wanaohitimu la 7, Buluki

BAKARI HASSAN SALIM, MOROGORO

Katibu Mkuu wa taasisi ya The Islamic Foundation, Mussa Ally Buluki, amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwachunga watoto wao wanaotarajiwa kumaliza darasa la saba mwaka huu ili waendelee kuwa vijana wema.

Buluki alitoa wito huo katika hafla ya mahafali ya wahitimu watarajiwa wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Mchikichini ‘B’ yaliyofanyika katika viwanja vya shule hiyo iliyopo kata ya Boma ndani ya Manispaa ya Morogoro.

Buluki, aliyekuwa akmuwakilisha Mwenyekiti wake, Aref Nahdi, alisema baadhi ya vijana huharibikiwa katika kipindi hicho kwa kujiona wakubwa na kusahau kuwa safari yao ya elimu ndiyo kwanza inaanza na wana hatua nyingi za kupiga hadi kufika vyuo vikuu.

Aidha Buluki alitumia fursa hiyo kuahidi kuwa The Islamic Foundation itaendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto za shule hiyo kama zilivyowasilishwa katika risala.

Licha ya wahitimu watarajiwa 75 wakiwemo wasichana 40 na wavulana 35, mahafali hayo yalihudhuriwa pia na wazazi, walezi, ndugu na jamaa wa wanafunzi hao, bila kusahau viongozi kadhaa waandamizi katika sekta ya elimu wa manispaa ya Morogoro.

Awali, akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, mwanafunzi Shadia Sharif amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fensi, madawati, uchakavu wa majengo pamoja na vifaa vya Tehama

Naye Afisa Elimu wa Kata ya Boma, Prosper Josephat Kiwia, kama ilivyo kwa mgeni rasmi, naye alihimiza wazazi kujitahidi kuwaongoza watoto hao ili waendelee kuwa vijana wema katika maisha yao ya baadae.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Morogoro, Mgeni Gerald Mussa, aliipongeza taasisi ya The Islamic Foundation kwa kuwa mdau mkubwa katika sekta ya elimu kwa kuchimba visima vya maji mashuleni ikiwa ni jitihada zake za kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button