Blog
Trending

Watoto 510 wafanyiwa upasuaji moyo Tanzania katika miaka 10 ya mradi wa Little Hearts

“Tunawashukuru sana Muntada Aid kwa kutuamini na kutufanya kuwa washirika wao Tanzania na kuwa sehemu ya mradi uliiokoa maisha ya mamia ya watoto kupitia matibabu ya upasuaji wa moyo” – Aref Nahdi, Mwenyeiti wa taasisi ya The Islamic Foundation

NA MWANDISHI WETU

Kuelekea miaka 10 tangu kuanza kwa mradi wa Little Hearts, takwimu zinaonesha kuwa, kwa Tanzania pekee, maisha ya zaidi ya watoto 500 yameokolewa baada ya kufanyiwa matibabu ya upasuaji wa moyo

Mradi huo wa taasisi ya Muntada Aid ya Uingereza uliingia hapa nchini mwaka 2015 ukienga kuhudumia watoto wenye shida mbalimbali za moyo kwa kuwafanyiwa operesheni na kuwarejeshea afya zao katika hali ya utimamu, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.

Katika mfululizo wa miaka hii 10 ya utekelezaji wa mradi huu, taasisi ya Muntada Aid imekuwa ikishirikiana na ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambao ndiyo taasisi mtekelezaji mwenyeji huku The Islamic Foundation ikihusika kama wawezeshaji na waratibu wa ndani.

Aref Nahdi, Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, akikumbuka athari chanya ya takriban miaka hii 10 ya utekelezaji wa mradi, amesema inampa furaha kupitiliza kuona kwao taasisi yake imeshiriki katika kurejesha furaha ya maisha kwa familia hizo zaidi ya 500 kwa kuokoa maisha ya watoto.

“Hauwezi kujua Allah Mtukufu amewapangia nini hawa watoto, huenda miongoni mwao kuna viongozi wakubwa, wanasayansi, madaktari bingwa, wanazuoni … huenda hata Rais wa nchi. Ni furaha iliyoje kwangu kuwa sehemu ya watu waliowarejeshea watoto hawa matumaini ya kusaka ndoto zao.”

Aref Nahdi aliongeza: “Tunawashukuru sana Muntada Aid kwa kutuamini na kutufanya kuwa washirika wao Tanzania na kuwa sehemu ya mradi uliiokoa maisha ya mamia ya watoto kupitia upasuaji wa moyo.”

Takwimu rasmi ambazo Gazeti Imaan ilipewa kuhusu upasuaji uliofanyiwa watoto unaonesha kuwa mara ya kwanza mradi huu kuanza kutekelezwa ilikuwa ni mwaka 2015 ambapo watoto 64 walinufaika na tangu hapo kambi nane zimeandaliwa na kuokoa maisha ya watoto 510.

Mara ya mwisho mradi huu kufanyika hapa nchini ilikuwa ni Aprili 24, mwaka huu ambapo watoto 35 walinufaika huku kukiwa na matumaini ya matibabu ya upasuaji wa aina hii chini ya Muntada Aid kuendelea miaka mingi ijayo.

Tanzania imefaidika vipi?

Mradi huu wa Little Hearts umezaa faida nyingi, ingawa kubwa zaidi ni kuokoa maisha ya watoto ambao hivi sasa wengi wanaendelea na maisha yao ya kawaida, wakiwa wanafunzi katika ngazi mbalimbali. Mradi huu pia umeleta faraja kubwa kwa wazazi ambao baadhi walishakata tamaa.

Ikumbukwe kuwa matibabu haya ya upasuaji yamekuwa yanatolewa bure na walengwa ni watoto kutoka katika familia maskini, zisizojiweza huku gharama zikilipwa na waja wema waliotoa sadaka zao kwa maslahi na ustawi ya watu. Mradi huu pia hauna ubaguzi kabisa – umekuwa ukitoa matibabu kwa watoto wa rangi, dini, kabila, jinsia zote na hivyo kudumumisha mshikamano wa Kitanzania.

Katika hali ya kawaida, bila mradi huu, watoto hawa wa kimasikini huenda hata kama wangefanyiwa hizo operesheni, ingewasubiri kusubiri kwenye foleni kwa muda mrefu na kuzidi kuhatarishi maisha yao. Huenda hata wasingeweza kumudu gharama za matibabu hata kwa bei za hospitali za serikali, hivyo thamani ya mradi huu wa Muntada Aid haiwekeki kifedha.

Kwa upande mwingine na muhimu zaidi, juhudi za Muntada Aid wakishirikiana na The Islamic Foundation, ni mkakati wa kuisaidia Serikali katika kusambaza huduma za jamii, ikiwa ni wajibu muhimu na kitendo cha kuonesha uwajibikaji wa hali ya juu wa taasisi za Kiislamu.

Faida nyingine kubwa ya mradi wa Little Hearts ni kujengeana uwezo na kubadilishana ujuzi baina ya madaktari wageni na wenyeji ambapo bila shaka hadi hivi sasa madaktari wenyeji watakuwa tayari wamejifunza utaalamu husika na kuendelea kutibu watoto wengine.

Kwa msingi huo, hata kauli kuwa wanufaidika wa mradi huu katika miaka hii takriban 10 ni 500 inaweza kuwa siyo sahihi sana kwa sababu uwezo uliojengwa kwa madaktari wenyeji unaendelea kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi, pengine ni kwa maelfu, ukizingatia kuwa madaktari wengi wanafanya kazi maeneo zaidi ya moja.

Inawezekana kabisa taasisi mwenyeji JKCI pia imefaidika kwa kuachiwa vifaa mbalimbali ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujenga uwezo wa hospitali wenyeji.

Kuhusu Little Hearts

 Little Hearts ni mradi muhimu zaidi wa Muntada Aid uliozinduliwa Aprili 2012 ambapo kupitia mradi huu taasisi hiyo inatoa matibabu ya bure ya kuokoa maisha kupitia upasuaji wa moyo, walengwa wakiwa ni watoto hususan kutoka katika familia maskini waliozaliwa na matatizo hayo, lakini pia bila kujali jinsia, kabila, rangi wala dini zao.

Kidunia, tangu mwaka 2012 mradi huu ulipoanza, Muntada Aid imeandaa kambi hizo za upasuaji katika nchi 13 ikihusisha safari 49 ambapo watoto 2,990 walifaidika kwa matibabu ya upasuaji. Fikiria Tanzania kuwa sehemu ya nchi 12 za mradi huu ni bahati iliyoje?

Ukiacha Tanzania, nchi nyingine zilizofaidika ni pamoja na Misri, (kambi 8 katika miaka tofauti, watoto wanufaika 313), Kazakhstan (kambi moja, wanufaika 31), Morocco (kambi 4, wanufaika 2000 na Sudan (kambi 8, wanufaika 627).

Nchi nyingine zilizofaidika na mradi huu ni Bangladesh (kambi 5, wanufaika 741), Yemen (kambi moja, wanufaika 64, Mauritania (kambi moja, wanufaika 28), Libya (kambi 6, wanufaika 275), Kenya (kambi 3, wanufaika 102), Benin (kambi moja, wanufaika 5), Uganda (kambi moja, wanufaika 14), na Kosovo (kambi mbili, wanufaika 80).

Kwa mwaka 2023, kupitia mradi wa Little Hearts nchi tano, zikiwemo Tanzania, Libya, Kenya, Kosovo na Bangladesh zilifikiwa huku watoto 260 wakinufaika kwa matibabu na upasuaji. Katika mwaka 2023, ni Tanzania ndipo watoto wengi walitibiwa (57), kuliko nchi nyingine zote, wakifuatiwa, kuonesha namna Muntada Aid inavyoithamini Tanzania.

Miradi mingine ya Muntada Aid

Ukiacha mradi wa Little Hearts, Muntada Aid pia inaendesha miradi mingine kadhaa ikiwemo uchimbaji visima (drop of life) ambapo watumiaji 51,800 katika nchi nane wamenufaika. Mradi mwingine ni wa upasuaji wa macho uitwao ‘gift of sight’ kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa mtoto wa jicho ambapo watu 1900 wamenufaika katika nchi nne. Mradi mwingine ni wa huduma za dharura ambapo watu 34,000 wamenufaika katika nchi saba.

Muntada Aid pia imekuwa ikitoa msaada wa vyakula katika mataifa yenye migogoro ya ndani ikiwemo Yemen ambapo kwa mwaka jana, 2023, watu 10500 wamenufaika. Huko Gaza nako, watu 36,400 wameufaika.

Katika afya ya mama wajawazito na shughuli za ukunga, Muntada Aid imetoa mafunzo kwa wakunga zaidi ya 80 katika nchi mbili za Uganda na Sierra Leone na kujenga vituo sita vya kijamii katika nchi nne za Togo, Niger, Mali na Ghana vikihudumia zaidi ya watu 1000 kila siku.

Takwimu za maradhi ya moyo kwa watoto

Kwa mujibu wa maelezo yanayopatikana katika tovuti ya Muntada Aid, inakadiriwa kuwa takriban watoto milioni 1. 5 kila mwaka huzaliwa na matatizo ya moyo duniani kote na asilimia 10 ya watoto hao hawafikishi mwaka mmoja bali hufariki. Maelfu wengine hufariki kabla ya kufikia utu uzima.

Maelezo yanazidi kufafanua kuwa katika nchi maskini, ukosefu wa miundombinu ya afya hufanya watoto wenye matatizo hayo kukosa fursa ya matibabu. Kwa kuona hilo, Muntada Aid, inaamini kupuuzia maradhi haya hatari ni kama kuwahukumu watoto hao adhabu ya kifo.

Kuonesha kujitoa kwa taasisi hiyo, tovuti ya Muntada Aid inanadi: “Kwa kujua kuwa mengi ya maradhi haya (ya moyo ka watoto) yanatibika ila kinachokosekana ni rasilimali, miundombinu na wataalamu, tunajitoa kwa watoto waliozaliwa na matatizo haya kuwapa nafasi ya maisha yenye siha njema.”

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button