Waislamu wanaunda asilimia 29 ya wahamiaji wote wa kimataifa, imeelezwa. Asilimia hiyo 29 inatokana na takriban Waislamu milioni 80 waliohama kutoka katika nchi zao, wakitafuta hifadhi, fursa, na maisha bora, kwa mujibu wa Kituo cha UtafIti wa Pew.
Utafiti wa Pew unaonesha kuwa njia za Waislamu za uhamiaji mara nyingi huongozwa na ukaribu wa kijiografia, wakipendelea kuhamia ndani ya kanda zao, hususan katika maeneo ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini (MENA) na eneo la Asia-Pasifiki.
Muelekeo huu unaonyesha uhusiano wa kina kati ya imani na kutafuta utulivu na maadili, wachambuzi wanasema.
Uhamiaji wa Waislamu, ingawa umeenea, mara nyingi unategemea ukaribu na nchi za asili ambapo mhamiaji wa kawaida Muislamu husafiri umbali wa maili 1,700, ambao ni mfupi zaidi ikilinganishwa na umbali unaosafiriwa na wahamiaji wa makundi mengine ya kidini.
Ukaribu huu unaonesha uhusiano thabiti wa kitamaduni na kihistoria ndani ya Umma wa Kiislamu, kama inavyodhihirishwa na uhamiaji wa Wasyria kwenda Uturuki na Lebanon.
Eneo la MENA lin asilimia 40 ya wahamiaji Waislamu, likithibitisha utafiti kuwa wengi wanatafuta hifadhi katika mazingira ambayo maadili na desturi za Kiislamu yanadumishwa.
Saudi Arabia, chimbuko la Uislamu, ndiyo nchi inayowavutia wahamiaji wengi zaidi Waislamu, ikiwa na takriban wahamiaji Waislamu milioni 10.8.
Taifa hilo la Kifalme, si tu inaongoza kwa kuvutia Waislamu bali pia ni taifa la tatu duniani katika kuwavutia wahamiaji wengi sababu zikitajwa kuwa ni ustawi wake wa kiuchumi na maadili ya Kiislamu ndani ya miji mitakatifu ya Makkah na Madina.
Nchi nyingine inayovutia wahamiaji wengi ni Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) yenye wahamiaji Waislamu milioni 6, sababu zikitajwa kuwa ni uimara wa uchumi wake unaokua kwa kasi na mahitaji ya wafanyakazi wa kigeni.
Syria, iliyoharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2011, imekuwa chanzo kikubwa cha wahamiaji Waislamu, ikitoa watu milioni 8.1 ikifuatiwa na. India ikitoa wahamiaji Waislamu milioni 6, ingawa Waislamu ni asilimia 15 tu ya idadi ya watu nchini India.
Uhamiaji kutoka India kwenda nchi zenye Waislamu wengi katika Ghuba, kama vile UAE na Saudi Arabia, unaonyesha uhusiano kati ya fursa za kiuchumi na uhusiano wa kidini. Afghanistan, iliyopitia miongo kadhaa ya migogoro, ni ya tatu katika miongoni mwa nchi vyanzo vya wahamiaji Waislamu wakielekea Iran na Pakistan.
Idadi ya wahamiaji Waislamu duniani imeongezeka mara mbili tangu mwaka 1990, huku kukiwa na ongezeko kubwa katika nchi kama Saudi Arabia, UAE, na Uturuki. Hata hivyo, si maeneo yote yameshuhudia ukuaji huu ambapo kwenye nchi za Pakistan na Iran kuna hali ya kupungua kwa idadi ya wahamiaji Waislamu, kwa kiasi fulani, kutokana na kurejea kwa wakimbizi wa Afghanistan.