1. TIF NewsTujikumbushe

Swala inahitaji maandalizi-3

Kabla ya kuelekea msikitini, inapendeza zaidi ukichukua udhu nyumbani. Msingi wa hili ni Qur’an. Allah Aliyetukuka anasema: “Enyi watu, chukueni mapambo yenu wakati wa kila swala, na kuleni (vizuri) na kunyweni (vizuri) lakini msipite kiasi, hakika yeye (Mwenyezi Mungu hawapendi wapitao kiasi.” (Qur’an, 7: 32)

Aya hii, licha ya kututaka tutumie neema na riziki, ikiwa ni pamoja na vyakula na vinywaji, alivyotupa Allah Aliyetukuka kwa uangalifu, pia inatutaka kufanya maandalizi tunapotaka kutoka kwenda msikitini kwa kuvaa nguo safi na zilizo twahara, kupiga mswaki na kuchukua manukato. Fiqhi ya Swala inatutaka tunapotoka kwenda misikitini tuwe tumevaa nguo pana zinazotusitiri vizuri na zisizo na picha huku tukiamini kuwa tunaelekea kwenye hadhara takatifu mbele ya bwana Mtakatifu.

Basi haipendezi, na vilevile inakera, mmoja wetu akijitokeza akiwa amevaa nguo chakavu na chafu anapokwenda katika hadhara hiyo, lakini akienda katika hadhara nyengine anaonekana mtanashati na amevaa nguo nzuri za kupendeza. Hakuna hadhara takatifu zaidi kuliko hadhara ya Allah, Mfalme wa wafalme, Muumba wa kila jambo. Vile vile haipendezi Muislamu kwenda msikitini akiwa ananuka kikwapa au kinywa chake kikitoa harufu mbaya!

Haya ndio aliyoyapiga marufuku Mtume wa Allah aliposema: “Yoyote atakayekula kitunguu thaumu au kitunguu maji basi (hata) asiukaribie msikiti wetu huu.” Katika Hadithi, kumetajwa kitunguu thaumu na kitunguu maji kwa sababu ni viungo vyenye harufu kali, lakini tunatakiwa tunatufahamu kwamba kitu chochote chenye harufu kali au mbaya itakayowaudhi Waislamu msikitini kimekatazwa.Na kwa upande wa pili, harufu nzuri za wastani zinatakiwa.

 

Kuwahi msikitini

Jambo jengine linalompasa Muislamu katika kufanya maandalizi ya Swala ni kuzijua kwa ufasaha nyakati zake na kuwa na pupa ya kuwahi kuziswali mwanzo wa nyakati hizo. Allah Aliyetukuka anasema: “…hakika ya Swala ni wajibu uliowekewa wakati (maalumu).”[Qur’an 29:45]

Waislamu wanatakiwa wawahi mapema msikitini kabla ya Swala kuanza, na njiani wawe watulivu sana, wasipige makelele, wasibishane wala wasifanye jambo lolote litakalowatoa kwenye lengo la shughuli iliyowatoa majumbani mwao. Wakifika msikitini, Waislamu wanatakiwa wafuate taratibu zote za kiibada kwa kuingia kwa mguu wa kulia pamoja na dua maalumu, kisha kusali rakaa mbili za kuamkia msikiti.

Kisha wakae kwa utulivu na kuendelea na ibada nyengine kama kusoma Qur’an au kuleta nyiradi mbalimbali wakisubiri adhana. Baada ya Adhana, wanatakiwa waswali rakaa mbili ikiwa ni namna ya kuzihifadhi Swala kulikoamrishwa katika Qur’an Tukufu na Hadithi za Mtume na kuahidiwa kupata pepo kwa kusema: “Zihifadhini Swala (zote) na (hususan) Swala ya kati na kati (sala ya Al-asr) na simameni mkiwa wanyenyekevu.” (Qur’an, 2: 238). Katika aya nyingine anasema: “na wale ambao Swala zao huzihifadhi (huzitunza). Hao watakuwa katika mabustani wakikirimiwa.”

Aidha, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amelielezea jambo la kujiandaa, kuwahi mapema msikitini na kuingojea Swala kulekule, kuwa humfutia Muislamu makosa yake. Mtume pia amefananisha msikitini na kambi ya kuvizia mafanikio au sawa na jeshi linapojipanga kambini kwa ajili ya vita au kimbilio la wahitaji. Mtume amesema katika Hadithi iliyosimuliwa na Abuu Huraira: “Je nisikwambieni jambo ambalo Allah hufuta madhambi kwalo?” Wakasema: “Kwa nini (tuambie).” Akasema: “Ni kutawadha vyema nyakati zenye karaha na mashaka; na kwenda misikitini kwa kutembea, na kuingojea Swala nyingine baada ya Swala (iliyopita). Hayo ndio mavizio (makimbilio ya kheri), hayo ndio makimbilio, hayo ndio makimbilio.” (Muslim). Na pia kutoka kwa Abuu Huraira, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mmoja wenu huzingatiwa kwamba yumo katika Swala muda wote ambapo (amekaa msikitini na) Swala ndio iliyomzuia kurudi kwa jamaa zake.” (Imam Bukhari na Muslim)

Vilevile, kutoka kwa Abdullah bin Masoud (Allah amridhie) amesema alimuuliza Mtume ni ipi amali bora zaidi? Mtume akasema: “Ni Swala juu ya wakati wake.” yaani mwanzo wa wakati wake. (Bukhari na Muslim).

Inapokimiwa Swala

Swala Inapokimiwa utaratibu ni kwamba, Waislamu wanatakiwa waache papara na waiendee vilevile kwa utulivu. Katika hadithi, Mtume amesema: “Ikikimiwa Swala iendeeni na jilazimisheni kuwa watulivu na wenye heshima. Mlipopawahi katika Swala hiyo, swalini (na imamu) na palipokupiteni timizeni (baada ya salamu ya imamu).” Hadithi hii pamoja na kusisitiza busara na utulivu tunapoiendea swala, inatukataza pia papara na kufanya vishindo kulazimisha kuwahi rakaa ya imamu tunapochelewa kuingia pamoja naye katika swala.

Swala inahitaji maandalizi -2

Swala inahitaji maandalizi-1

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close