Tujikumbushe

Sema Bismillah Wakati Wa Kula

Hudhayfatu Ibnu Alyamaaniy [Allah amridhie] amesema: “Tulikuwa tunapohudhuria kwa ajili ya kula chakula pamoja na Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] hatuweki mikono yetu [katika sahani] mpaka aanze Mjumbe wa Allah kuweka mkono wake. Wakati fulani tulihudhuria pamoja naye kula chakula, akaja kijakazi mmoja kama vile amesukumwa [alikuwa mwenye haraka], akaenda kwa ajili ya kuweka mkono wake kwenye chakula, Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] akaushika mkono wake, akaja Bedui mmoja [mwarabu wa mashambani], kama vile amesukumwa,

Mtume akasema: ‘Hakika shetani hujihalalishia chakula pasipotajwa jina la Allah na hakika yeye [Shetani] amekuja pamoja na huyu binti ili aweze kula nikaushika mkono wake, akaja pamoja na huyu bedui ili aweze kula nikaushika mkono wake. Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu ipo mikononi mwake: Hakika mkono wake [Shetani] upo mkononi mwangu pamoja na mikono yao [aliishika pamoja] kisha akalitaja jina la Allah [Bismillahi] akala,” [Muslim].

Mtume [rehema za Allah  na amani zimshukie] aliwafafanulia tukio hili Maswahaba [Allah awaridhie] kwa kusema, shetani hupata nafasi ya kula chakula ambacho hakikutajiwa jina la Allah ndio maana alishika mikono yao. Katika tukio hili tunajifunza adabu mbalimbali ambazo muislamu anatakiwa kujipamba nazo wakati wa kula.

Mosi, kumtanguliza kiongozi Imesisitizwa katika uislamu kumtanguliza kiongozi [mtu mwenye cheo/wadhifa], hadhi au mtu mzima katika kuosha mikono na kuanza kula. Imamu Nnawawiy [Allah amrehem] amesema: “Hiki ndicho kitendo cha Maswahaba [Allah awaridhie], wao walikuwa hawaanzi kula mpaka aanze Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie]”. Amesema Kadhi Iyaadh: “[Maswahaba] walipendelea [Mtume] awe wa kwanza kati ya watu waliohudhuria pale kuosha mikono na kula ili awachangamshe katika hilo, na kinyume chake pia awe wa kwanza kunyanyua mkono na kuuosha baada ya kula.”

Kusema Bismillahi wakati wa kula

Amesema Imamu Nnawawiy [Allah amrehem]: Ni sunna kusema ‘Bismillahi’ wakati wa kuanza kula na hili ni jambo walilokubaliana wanazuoni, vilevile kusema ‘Al’hamdulillahi’ baada ya kumaliza kula na katika kila jambo muhimu, na kama mtu ataacha kusema ‘Bismillahi’ kwa makusudi anapoanza kula chakula, au kusahau, au kulazimishwa, au kushindwa kwa sababu yoyote iliyojitokeza kisha ikawezekana kuisema katikakati ya chakula, basi aseme ‘Bismillahi awwaluhuu wa-aakhiruhu’.

Inatakiwa kila mmoja aseme ‘Bismillahi’ lakini kama watu wanakula pamoja na ikatokea mmoja wao ameitamka, basi itatosheleza, na villevile sunna itakuwa imepatikana, kwa sababu Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie], amesema kuwa: ‘Shetani anapata fursa ya kula chakula ambacho halikutajwa jina la Allah juu yake, na makusudio yatafikiwa kwa kutajwa hata na mtu mmoja,” [ameeleza hayo Imamu Shafi].

Pindi mtu anapoingia nyumbani kwake akamtaja Allah wakati wa kuingia kwake na wakati wa kula, shetani huwaambia wenzake hamna pa kulala wala hamna chakula cha usiku, na pindi anapoingia akawa hakutaja jina la Allah wakati wa kuingia shetani husema mmepata pa kulala, na ikiwa hatotaja jina la Allah wakati wa kula, shetani husema [kuwaambia wenzake], mmepata chakula na mahala pa kulala,” [Muslim]

Kuwafundisha watu kwa vitendo

Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] aliushika mkono wa kijakazi yule pamoja na Bedui, kisha akatumia fursa  hiyo kuwaelimisha Maswahaba juu ya kitendo hicho cha kushangaza ili awafundishe watu wote kwa pamoja. Hii ilikuwa ni desturi yake pale anapokosea mtu naye akataka kutumia tukio hilo kwa ajili ya kuwazindua watu.

Amru Ibnu Abii Salama [Allah amridhie] amesema: “Nilikuwa kijana mdogo chini ya malezi ya Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] na mkono wangu ulikuwa unazunguka zunguka kwenye sahani ya chakula, Mtume akaniambia: Ewe kijana! Taja jina la Mola wako [Sema Bismillah], kula kwa mkono wako wa kulia na ule sehemu inayokuelekea [upande wako], haukuacha kuwa ndio ulaji wangu baada ya hapo,” [Imepokewa na Bukhari].

 

Shetani anakula na anao mkono

Imamu Nnawawiy [Allah amrehem] amesema, huu ni mfano wa miongoni mwa hadithi zinazozungumzia kula kwa shetani zinazochukuliwa kwa dhahiri yake kwa sababu jambo hilo halipingani na akili na sharia haijalikanusha, bali imelithibitisha, kwa hiyo ni wajibu kuamini kuwa shetani naye anakula na ana mkono kama ilivyoelezwa katika hadithi.

Madhara ya kutosema ‘Bismillahi’ wakati wa kula

Mafundisho ya Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] yana faida kubwa kwetu. Kitendo cha kushika mkono wa mtu katika sahani ya chakula kinaweza kuonekana kuwa kizito, cha kustaajabisha lakini madhara aliyoyazuia yalikuwa makubwa zaidi.

Jabir Ibnu Abdillahi [Allah amridhie] amesema: “Nilimsikia mjumbe wa Allah [rehema za Allah na amani zimshukie] akisema: “Pindi mtu anapoingia nyumbani kwake akamtaja Allah wakati wa kuingia kwake na wakati wa kula, shetani huwaambia wenzake hamna pa kulala wala hamna chakula cha usiku, na pindi anapoingia akawa hakutaja jina la Allah wakati wa kuingia shetani husema mmepata pa kulala, na ikiwa hatotaja jina la Allah wakati wa kula, shetani husema [kuwaambia wenzake], mmepata chakula na mahala pa kulala,” [Muslim]. Hii ni dalili kuwa watu wengi wanashirikiana na shetani wakati wa kula kutokana na kutolitaja jina la Allah.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close