Tujikumbushe

Kumaliza mitihani si mwisho wa kusaka elimu

Hivi sasa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na elimu ya juu hapa nchini wamekamilisha taratibu za udahili na tayari wameanza masomo yao ya vyuo vikuu.

Sisi Imaan media tunawapa kongole nyote mliopata nafasi hiyo muhimu, na ambayo tunaamini itarahisisha safari yenu ya kutafuta elimu. Tunapongeza kuchaguliwa kwenu tukitambua kuwa, elimu si mateso, bali ni sehemu ya mchakato wa kutengeneza hatima njema ya maisha yenu.

Pia, tunawapongeza wazazi na walezi ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa pamoja nanyi katika kuhakikisha mnapata mahitaji muhimu ili muweze kusoma kwa ukamilifu. Hata hivyo, yafaa mtambue jukumu lenu katika jamii na dini yenu. Vyovyote itakavyokuwa, nyinyi kama vijana wa
kiislamu, mnalo jukumu la kuuletea Uislamu na waislamu maendeleo.

Lakini jambo kubwa zaidi ni kuwataka mfanye juhudi ya kuwalingania vijana wenzenu huko shuleni na katika vyuo mnavyokwenda. Kama vijana wa Kiislamu mnapaswa kutambua kuwa jukumu la kuulingania Uislamu katika jamii ya wanavyuo linawahusu nyote, si jukumu la jumuiya au vyama vinavyowawakilisha wanafunzi pekee.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Fikisha kutoka kwangu japo aya moja,” (Bukhari).

Ni kwa msingi huo mnao wajibu wa kuhakikisha mnailingania jamii ya waislamu vyuoni sambamba na kutatua changamoto zao. Kwa hakika hizi ni ibada mbili muhimu ambazo mnatakiwa kuzidumisha.

Kama watu mlio na malengo maalumu mnapaswa kujipamba na sifa ya maadili, tabia njema na kujenga mahusiano mema na ndugu zao waislamu na wasio waislamu. Hii ni pamoja na kuendeleza matukufu yote ya kiislamu ikiwemo kudumisha swala tano. Hivyo, ni imani yetu kufanya kwenu hivyo kutapelekea wasiokuwa Waislamu kuusoma Uislamu kwa uangalifu na umakini, kwani daima ujumbe wa Uislamu unamtaka kila mwanadamu kutegemea dalili na kufanya utafiti wa kina ili kubaini ukweli. Naam! hii ndio mantiki ya Uislamu kuwahusu wafuasi wa dini nyingine.

Kwa muktadha huo mna kila sababu ya kuwa wawakilishi wazuri wa dini kwa kujipamba na tabia njema muwapo vyuoni. Mbali na hilo, pia mfahamu mnapofanya mambo mema ni kwa faida yenu, kadhalika mkifanya mabaya mtakuwa mnajidhoofisha wenyewe.

Ni ukweli kuwa tabia njema inaweza kumshawishi mtu asilimu na ndio maana Mtume wetu (rehema za Allah na amani zimshukie) alijipamba na mazungumzo ya bashasha kwa watu wote (waislamu na wasiokuwa waislamu).

Hivyo ni imani yetu wanafunzi wa Kiislamu waliochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu mwaka huu watakuwa chachu ya mabadiliko ya kitabia katika jamii kwa sababu wao wanamfahamu zaidi Muumba wao.

Mwenyezi Mungu anasema: “Kwa hakika wanaomuogopa zaidi Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni Wanazuoni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe,” (Qur’ an, 35:28).

Kumaliza mitihani si mwisho wa kusaka elimu…

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close