Tujikumbushe

Ikhtilafu ndogondogo zisitujengee uadui

Kwa miongo kadhaa, Waislamu hapa nchini wamekuwa wakitofautiana kimtazamo juu ya masuala mbalimbali yahusuyo dini likiwemo suala la kudhihirisha ‘Bismillah’ wakati wa kusoma Surat Fat–ha ndani ya Swala na mengineyo.

Ukifanya tathmini ndogo, utagundua jinsi ikhtilafu hizi zilivyochukua sura ya umimi na ubinafsi kiasi cha kuwagawa Waislamu. Hili linadhihiri katika zama hizi ambazo Waumini katika baadhi ya misikiti wamegawika makundi mawili – kuna wanaounga mkono kudhihirisha ‘Bismillah’, kadhalika kuna wanaopinga.

Ukweli ni kwamba, Waislamu wengi tunaohudhuria ibada ya Swala msikitini si wataalamu bobezi kwenye masuala ya dini kiasi cha kuweza kutoa fat–wa, lakini kwa inavyoeleweka suala la tofauti katika Uislamu siyo jambo geni. Na kwa sababu ikhtilafu za kimawazo zipo katika Uislamu kwa muda mrefu, hatushangai kuwaona Waislamu wanaounga mkono suala hilo na mengineyo.

Kinachotuhuzunisha zaidi ni kuona hivi sasa ikhitilafu hizi hazilengi kuinua dini kwa kuwa uwepo wake unachangia kuibomoa dini na watu wake. Waislamu wengi hawaelewi kuwa suala la kutofautiana katika mambo mbali mbali ni jambo la kimaumbile. Allah Ta’ala anaelezea ukweli huu pale aliposema:

“Na angelitaka Mola wako angewafanya watu umma mmoja na wala hawatoacha kuwa wenye kutofautiana. Isipokuwa wale aliowarehemu Mola wako na kwa jili hiyo (Allah) amewaumba…” (Qur’an,
11:118).

Allah Ta’ala akasema tena: “Na angependa Mola wako wangeamini watu wote kwa pamoja, basi wewe utawalazimisha watu mpaka wawe Waumini?” (Qur’an, 10:99). Maa na yake ni kwamba, Allah Ta’ala hakutaka watu wote wawe kitu kimoja kiimani kwani amewapa vipaji mbalimbali hivyo kutofautiana ndiyo maumbile.

Kilicho muhimu kwa Waislamu ni kutumia hekima, busara na maneno mazuri wakati wanapojadili ikhtilafu zao kwani hata Wanazuoni wa zamani walipokuwa wanapingana kwenye masuala ya dini hawakuthubutu hata siku moja kupanda majukwaani kutukanana, kushambuliana na kushutumiana. Walikuwa wastaarabu kwa kudumisha heshima baina yao.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close