Tujikumbushe

Atakayevumilia Allah atampa uvumilivu

Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu- Sa’id Al-Khudriy [Allah amridhie] amehadithia kwamba, watu fulani katika Maanswaar walikwenda kumuomba Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie], akawapa alichokuwa nacho. Kisha, wakaenda kumuomba tena akawapa. Kisha, wakamuomba tena akawapa, mpaka kikaisha kile alichokuwa nacho.

Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] akawaambia: “Chochote cha kheri nitakachokuwa nacho sitawanyima na atakayetaka kujizuia kuombaomba Allah atamzuia na huko kuomba. Na yoyote atakayetosheka, Allah atamtosheleza; na atakayekuwa na subira Allah atampa uvumilivu. Na hajapata mtu kupewa kipawa kilichobora na chenye wasaa kuliko uvumilivu.”[Bukhari na Muslim].

Answaar ni watu waliotokana na makabila mawili maarufu ya wenyeji wa mji wa Madina ambao ni Aus na Khazraji. Hawa walimpokea Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] pale Yeye na Maswahaba zake [Allah awaridhie] walipohamia Madina. Ansaar walimuamini Mtume, wakamtetea na kusimama kidete katika kuitetea dini ya Allah Aliyetukuka.

Wakati mmoja, walikwenda kumueleza Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] shida zao na kumuomba awape chochote alichokuwa nacho, naye aliwapa. Walifanya hivyo mara tatu, hadi kilichopo kikaisha, ndipo akawafahamisha njia iliyokuwa bora katika maisha yao badala ya utaratibu huo wa kuomba. Mtume akawaelekeza kujizuia na tabia ya kuomba, watosheke na kile walichokadiriwa na wawe wavumilivu.

Mafundisho ya tukio: Ukarimu wa Mtume(saw).

Tukio hili, kwanza, linatufundisha ukarimu wa Mtume [rehema za.Allah na amani zimshukie]. Mtume alikuwa mkarimu mno kiasi cha kuwashangaza watu kwani wakati mwingine akiona mtu amevutiwa na nguo yake, basi humpa. Mtume hakuwa mwenye kumnyima yoyote mwenya kumuomba, na ushahidi upo wazi katika maneno aliyowaambia hao waliokwenda kumuomba. Alisema: “Mali yoyote nitakayokuwa nayo sitawanyima;” akionesha wazi kuwa hakuwa mtu mwenye kuurudisha patupu mkono wa muombaji kama anacho cha kumpa.

Taufiq ya Allah ipo sambamba na juhudi ya kibinadamu Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] anatufahamisha kuwa, inatakiwa kila mmoja achukue hatua muafaka, yaani afanye juhudi za kibinadamu, katika lile ambalo amelikusudia ili ategemee kupata taufiq ya Allah. Ni kwa kufanya juhudi binafsi ndio Allah Aliyetukuka atamsaidia katika hilo alilokusudia, kama maneno ya Mtume yalivyothibitisha pale alipowaambia lile kundi la Answaar:

Atakayetaka kujizuia kuombaomba Allah atamzuia,atakayekuwa na subira Allah atampa uvumilivu na atakayetosheka Allah atamtosheleza.”

Maneno haya yanatupa muongozo kuwa, binadamu anahitajika kwanza kuchukua hatua fulani kuoneshe njia ya kile anachokikusudia, kisha Allah atamuafikisha katika hilo. Kuombaomba si tabia nzuri Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] na Maswahaba zake [Allah awaridhie] walipohamia Madina walipitia maisha magumu na walipata msaada mkubwa kutoka kwa wenyeji wa mji huo; lakini pamoja na ufukara waliokuwa nao, wahamiaji hawakuudhihirisha umaskini wao kwa kuombaomba.

Maswahaba walikuwa wavumilivu na wenye kuchapa kazi naye Allah akawafanyia wepesi katika maisha yao. Hata ngawira zilipopatikana, Allah aliwataja kwa sifa ya ufukara waliokuwa nao na kuelekeza kuwa wanastahiki kupewa na kusaidiwa.

Wapewe mafakiri wahajiri waliotolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake, na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao ndio wa kweli.” [Qur’an, 59:8].

Licha ya ukweli huo, Maswahaba hawakuwa na tabia ya kuombaomba, bali walijizuia na kuvumilia. Walivumia licha ya kuwa hali zao ngumu zilichangiwa na kujishughulisha zaidi katika harakati za kuipigania dini ya Allah. Hili lipo wazi katika kauli ya Allah:

Nawapewe mafakiri waliozuilika
katika njia za Mwenyezi Mungu, wasioweza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiyewajua hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua kwa alama zao; hawang’ang’anii watu kwa kuwaomba. Na kheri yoyote mnayo toa, basi kwa yakini Mwenyezi Mungu anaijua.” [Qur’an, 2:273].

Tunaona wazi kuwa, suala la kuombaomba si tabia nzuri katika Uislamu. Ni tabia ambayo inapaswa kupigwa vita katika jamii ya Waislamu ili watu waishi kwa kujishughulisha na kumtegemea Allah ambaye ni mbora wa kuruzuku. Yatupasa Waislamu kuamini kuwa, kila mmoja amekadiriwa riziki yake katika maisha haya madhali yupo hai. Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa, tunafanya kazi na kumtegemea Allah kama inavyotakiwa na kujizuia na tabia hii mbaya ya kuombaomba ambayo imechukua nafasi kubwa katika
maisha ya watu.

Kuvumilia na kukinai

Uvumilivu ni sifa muhimu sana katika maisha ya Muislamu. Muislamu anatakiwa aoneshe wazi uvumilivu kuanzia mwanzo katika matukio magumu anayokabiliana nayo. Yawe ni maumivu ya maradhi au matatizo mengine ya kimaisha kama vile ufukara au ugumu wa maisha, Muislamu asiyakabili kwa kufadhaika, kulalama na kutoa maneno yasiyokuwa mazuri au kuanza kuhaha na kuranda ovyo akitangaza hali yake inayomkabili.

Tufahamu kuwa ikiwa mtu ataifungulia nafsi yake mlango wa kuombaomba, ajue wazi kuwa nafsi haitosheki wala haikinai na matokeo yake ni kumzowesha mtu kutegemea kupata kwa urahisi pasi na juhudi yoyote ya kujishughulisha.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close