1. Habari

Umaskini bado kikwazo cha elimu kwa jamii za Waislamu

Wakati tukielekea mwishoni mwa mwaka ambapo shule za msingi na sekondari hufungwa, tayari kwa maandalizi ya mwaka mpya wa msomo utakaoanza Januari, uchunguzi wa gazeti la Imaan  unaonesha kuwa, umaskini ufukara bado ni kikwazo kikubwa kwa jamii za Kiislamu katika kuitafuta elimu, hususan ya mazingira.

Athari ya ufukara na umaskini inaonekana wazi kwa familia zenye watoto ambao wamemaliza ngazi moja ya elimu kwenda ngazi nyingine, mfano kutoka msingi kwenda shule ya upili au kutoka shule ya upili kwenda sekondari ya juu. Baadhi ya hawa, hususan wale ambao watoto wao wameshindwa kupata nafasi katika shule za serikali, wameshindwa kupeleka watoto wao katika shule binafsi kwa sababu ya kushindwa kumudu gharama kubwa za ada na mahitaji mengine.

Gazeti Imaan limekuwa likipokea simu za watu mbalimbali wakiulizia uwezekano wa kupata ufadhili au mikopo ya masomo kwa ajili watoto, huku wengine wakiomba ushauri waende wapi, hali inayoonesha jinsi ufukara na umaskini unavyoviza ndoto za harakati za kusaka elimu za vijana wengi.

Mama mmoja, Ummu wa Ilala, alipiga kwa mhariri wa Gazeti hilo, akiomba aelekezwe wapi aende kupata msaada ili mwanae wa kiume mwenye umri wa miaka 13, aliyemaliza elimu ya msingi na  ambaye hakubahatika kuchaguliwa  katika shule za serikali, apate fursa ya kuendelea na masomo!

Mwanangu baba yake alifariki. Sasa alifeli somo moja ambalo limemgharimu sana na hivyo hakuchaguliwa kwenda sekondari; na mimi pesa ya kumsomesha  shule binafsi sina. Namuonea huruma mwanangu ni mdogo! Miaka 13 jamani akae nyumbani atafanya nini?” alilalama mama huyo.

Changamoto inayomkabili Ummu katika jitihada za kumuendeleza mwanae inawakabili watu wengi baadhi yao ni wanawake kama Ummu kutokana na hali ya ujane na hivyo kukosa usaidizi wa  waume, na wengine ni kutokana tu na ufukara na umaskini uliokithiri.

Katika wanawake waliowahi kuomba msaada kwa mhariri ni Rehema Musa wa Magomeni ambaye mumewe wa kwanza alipata maradhi ya akili, hali iliyopelekea mama huyo kupambana pekee katika kumsomesha mwanae ambaye sasa yuko kidato cha kwanza. Mama huyo alihadithia kwa masikitiko jinsi walimu walivyomuita shuleni na kumsema kuhusu sare za mwanae ambazo zimechanikachanika, hususan suruali ambayo imelika kwenye makalio.

Mifano ya wazazi wa Kiislamu kama Ummu na Rehema, wanaoshindwa kusomesha watoto wao ni mingi, nchi nzima. Na ukizingatia kuwa wawili hawa ni wanawake wa mjini, unaweza kuhisi namna hali ilivyo mbaya maradufu katika maeneo ya vijijini. Hata hivyo, jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa, ni vigumu kwa wazazi wa hawa kupata taasisi za Kiislamu zinazoweza kuwapa usaidizi au mikopo, jambo linafanya umaskini kubakia kuwa changamoto kubwa katika harakati za baadhi ya familia za Kiislamu kujikomboa kielimu.

Ziko wapi mali za Wakfu?

Matatizo kadhaa yametajwa kusababisha Waislamu kushindwa kuwa na mifumo ya kitaasisi ya kusaidia jamii za Waislamu masikini katika kujikomboa, hususan kupitia elimu, kwani elimu imethibitika kuwa ndio mwangaza wa maisha.

Miongoni mwa matatizo hayo ni kukosekana kwa juhudi za pamoja, miongoni mwa taasisi, za kukabiliana na changamoto hizi. Ni wazi kuwa, taasisi nyingi zinajitahidi kusaidia watu katika mambo ya kielimu lakini kama Waswahili wasemavyo, umoja ni nguvu, hivyo basi, ushirikiano wa kitaasisi ungeweza kuleta nguvu na chachu mpya ya kukabiliana na tatizo kwa kuliwekea mikakati mipana na imara zaidi. Hata hivyo, changamoto kubwa zaidi ni usimamizi na uendelezaji wa mali za wakfu ambazo kama zingetumika vema zingewaondolea Waislamu adha na shida nyingi, mfano wa hizi.

Kuna taasisi kadhaa zilizokabidhiwa mali na Waislamu, zikiwemo mali za wakfu, likiwemo Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), misikiti, zawiya, na taasisi nyinginezo. Imefikia wakati sasa, mali hizo za wakfu zilizopo ziboreshwe, ziendelezwe na zitumike katika kutatua matatizo yanayowakabili walengwa wote badala ya kuwanufaisha watu wachache. Hii ni kwa sababu, kumekuwa na taarifa zisizofurahisha za ufujaji mkubwa wa mali hizo, ikiwemo kuuzwa kwa manufaa ya watu wachache.

Baadhi ya mali za wakfu zimekuwa ni majengo yaliyopo kwenye maeneo mazuri na ghali katika majiji makubwa, kama Dar es Salaam, lakini taasisi zilizokabidhiwa zimeshindwa kuziendeleza mali hizo ili zizalishe fedha zaidi itakayoweza kuwakwamua Waislamu katika shida mbalimbali, ikiwemo misaada ya kielimu kwa familia masikini.

Umefika wakati sasa, mfuko mmoja wa mali za wakfu wa taifa uundwe utakaoendeshwa kwa ushirikiano wa viongozi wa Kiislamu waaminifu kutoka taasisi mbalimbali ili mali hizo ziendeshwe kiweledi zaidi na  kuwasaidia Waislamu, vinginevyo matajiri wachache ambao kila siku tunawakimbilia kuwaomba hiki na kile, watashindwa! Tunaamini matajiri wakubwa hawatasita kutoa fedha katika mfuko huo wa Takaful au ‘Cash wakf’ wakijua zitawekezwa na kuzalisha faida na kuwasaidia Waislamu katika hali ya uendelevu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close