1. Habari

Uislamu na Mfumo wa Kodi

{Baada ya kuangalia katika makala iliyotangulia masuala ya sera za fedha na kodi za Kiislamu, leo tuangalie vyanzo vikuu vya mapato katika Dola ya Kiislamu. Vipato hivi na mali ya umma, zaka, ngawira (fai’), kodi ya ardhi (kharaj), kodi ya kichwa (jizya).}

Aina tofauti ya mapato ya mali ya umma.

Dola ya Kiislamu inagharamia mahitaji ya msingi ya watu wake wote kwa kusimamia huduma yoyote inayodhaniwa kuwa ni muhimu kwa jamii. Ile huduma ambayo inapokosekana, watu wanalazimika kuhangaika huku na kule, inachukuliwa kama mali ya umma.

Kwa mfano, kama mali ni ngumu kupatikana na haiwezi kutumiwa mpaka ichimbwe na kusafishwa, hiyo inachukuliwa kama mali ya umma. Vitu kama maji, mafuta, umeme na huduma nyingine muhimu kwa maisha, hivi vinamilikiwa na umma, na mapato yanayotokana navyo yanasimamiwa kwa manufaa ya wananchi wote. Msimamo huo unatokana na hadithi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) inayosema: “Waislamu ni washirika katika mambo matatu, maji, malisho na moto,” (Abuu Daud).

Ingawa hadithi imetaja vitu vitatu tu, wanazuoni wanatumia kanuni ya Qiyas kupanua zaidi ushahidi huu na kuingiza masuala yote ambayo ni muhimu kwa jamii. Kwa hiyo, vyanzo vya maji, misitu ya kuni, malisho ya mifugo na vingine kama hivyo ni mali ya umma, kama yalivyo maeneo ya uchimbaji mafuta, mitambo ya umeme, bahari, maziwa, mabwawa, ghuba, mikondo na kadhalika.

Serikali ya Kiislamu itaweka malipo fulani ya usimamizi wa huduma hizo kwa wananchi, ambayo yatakuwa ni mapato ya serikali. Pia itasafirisha mafuta nchi za nje, hatua ambayo italeta utajiri mkubwa katika hazina ya taifa.

Mwaka 2006 mapipa milioni 81 ya mafuta yalizalishwa kwa siku duniani, ambapo asilimia 45 ya mafuta hayo, yalitoka kwenye nchi za Waislamu, ambayo ni takriban mapipa milioni 38 kwa siku. Kwa bei ya wakati ule, mwaka 2007, pipa moja lilikuwa sawa na dola 80 za Kimarekani, hiyo ni sawa na mapato ya dola bilioni tatu kwa siku!

Mali za zaka
Zaka ni kodi ya mali ambayo watu wanawajibika kulipa asilimia 2.5 ya mali yao ambayo imekaa mwaka mzima. Mali za zaka zinahifadhiwa mahali maalumu kwenye Bait ul-Mal (Hazina ya Serikali) na haitumiki isipokuwa kwa vipengele nane ambavyo vimetajwa ndani ya Qur’an.

Lakini, hata hivyo, khalifa anaruhusiwa kutumia mali hizo, kwa mujibu wa vile anavyoona na Ijtihad, yaani kwa wale anaowaona wanastahili kupewa kulingana na vipengele vile nane. Kodi hii ni kodi ya usambazaji mali ambayo inasambazwa tena kwa watu masikini, wenye kuhitaji, wenye madeni na walinganiaji miongoni mwa vipengele vingine.

Ngawira (Fai’)
Hii ni mali inayopatikana wakati wa vita vya jihadi au ile inayoingia kwenye dola ya Kiislamu kupitia utangamano wa ulimwengu wa Waislamu (Intergration). Uislamu unawataka Waislamu kuishi chini ya dola ya Kiislamu, ambayo ndiyo muundo wa kisiasa wa Uislamu.

Matokeo ya hilo, uchumi wa dola hii utazidi kuendelea kutengemana (kuungana) na chumi zingine ambazo zitakuwa chini ya dola hii ya Kiislamu.

Kodi ya Ardhi
(Kharaj)
Kharaj ni tozo inayowekwa kwenye ardhi. Ni aina ya kodi ya ardhi. Kodi hii inakokotolewa kwa mujibu wa ubora wa ardhi na uwezekano wa thamani ya uzalishaji katika ardhi hiyo.

Kodi hii itachanganyika na sera nyingine kadhaa. Kwa mfano dola inaweza kuanzisha mapinduzi ya kilimo kwa kutoa mikopo, ukodishaji nafuu wa ardhi kwa raia, ili kuhakikisha sera ya kilimo iliyowekwa inafikiwa. Wale wanaomiliki ardhi ambayo haitatumiwa kwa miaka mitatu watanyang’anywa ardhi hiyo.

Kodi ya Kichwa
(Jizya)
Kodi ya jizya inatozwa kwa wanaume watu wazima wasio Waislamu (dhimmiy) ambao wana nyenzo za kulipa kodi hiyo. Wanawake na watoto wamesamehewa kodi hii kama walivyo masikini na wale wasiokuwa na nyenzo ya kulipa kodi hii.

Jizya inatozwa kulingana na ustawi wa dhim-miy. Wakati wa Umar bin al-Khattab (Allah amuwie radhi), alianzisha viwango tofauti vya jizya kulingana na ustawi wa mtu.
___________
Itaendelea toleo lijalo In Shaa Allah

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close