1. Habari

Tusiache kufunga Swaumu ya Ashura

Hakika Allah aliyetukuka ameumba majini na wanadamu kwa hekima na lengo maalum, nalo ni kumuabudu yeye, kama anavyobainisha:

Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi,” [Qur’ an, 51:56].

Na maana hasa ya ibada ni kule kuonesha udhalili na unyenyekevu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kupenda, kutukuza na kutekeleza amri zake, kadhalika kujiepusha na  aliyoyakataza.

Swaumu au funga ni miongoni mwa ibada kubwa ambazo Muislamu ameusiwa kuzipenda na  kuzitekeleza. Allah Aliyetukuka amefaradhisha funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ikiwa ni moja kati ya nguzo tano za Uislamu. Vilevile, Allah Aliyetukuka ameweka utaratibu wa kufunga siku maalumu za Sunna ili Muislamu apate fursa ya kujiongezea thawabu.

 

Funga ya Ashura ambayo hutekelezwa katika siku ya kumi ya Mwezi wa Muharram (mfunguo nne), ni miongoni mwa funga zenye utukufu na malipo makubwa mbele ya Allah ‘Azza Wajallah’. Imepokewa Hadithi kutoka kwa Ibn Abbas (Allah amridhie) akisema:

Sijapata kumuona Mtume akitilia maanani zaidi funga ya siku iliyo bora kama funga ya Ashura, na mwezi huu, yaani mwezi wa Ramadhani.” [Bukhari].

Katika maelekezo yake kwa Waumini juu ya siku hii adhimu, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

Fungeni siku ya Ashura na mjitofautishe na Wayahudi, fungeni siku moja kabla yake, na siku moja baada yake.” [Ahmad].

Katika kufafanua Hadithi hii, Imamu Ibn Qayyim (Allah amrehemu) amesema kuwa, ufungaji wa sunna ya siku ya Ashura, upo aina tatu.

Mosi, ni utimilifu, yaani kufunga siku moja kabla ya Ashura na siku moja baada ya Ashura, kwa maana kufunga siku tatu, siku ya mwezi 9, siku ya mwezi 10 na siku ya mwezi 11.

Pili, namna ya pili ni kufunga siku ya 9 na ya 10. Aina hii ndiyo iliyoelezwa na Hadithi nyingi za  mtume. Tatu, ni kufunga siku ya 10 pekee. Hivyo, ndugu Waislamu tusiache kufunga siku ya Ashura ili iwe sababu ya kufutiwa dhambi za mwaka mzima. Hii ni kwa neno lake Mtume  rehema za Allah na amani zimshukie):

Funga ya Ashura hufuta dhambi za mwaka uliopita.” [Muslim].

Pamoja na hivyo, ifahamike wazi kuwa Mwenyezi Mungu husamehe dhambi ndogo tu kwa mtu aliyefunga siku ya Ashura, ama dhambi kubwa, ni lazima mtu alete toba ili kupata msamaha. Mtu anayefunga Sunna ya Ashura hufutiwa dhambi zake ndogo, na kama hana huenda akafutiwa kubwa, na kama hana ‘Inshaa Allah’ atampatia thawabu.

Tusiache kufunga swaumu ya Ashura .

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close