1. TIF News

Ndugai: TIF Inafanya Kazi Kubwa ya Kuisaidia Serikali

Job Ndugai, Spika wa bunge
TIF imekuwa ikifanya shughuli zake kwa uweledi wa hali ya juu na kwamba serikali hususan bunge linaunga mkono jitihada za taasisi hiyo

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) inafanya kazi kubwa ya maendeleo ya jamii ambayo ni sawa na kuisaidia Serikali.

Spika Ndugai ameyasema hayo mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za makao makuu ya TIF mkoani Morogoro hivi karibuni ili kujionea shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo.

“The Islamic Foundation inafanya kazi kubwa sana, hatukujua kama inafanya nchi nzima, sisi tulikuwa tunajua ni Morogoro tu, lakini ni nchi nzima, upande wa dini mnafanya kazi nzuri, lakini kazi nzuri na kubwa zaidi inafanyika katika maendeleo ya jamii, na huduma za jamii,” alisema Spika.

Spika aliongeza: “Kinachotuvutia zaidi ukiacha masuala ya kusaidia maji na mengine ni kuwalea yatima, hili ni jambo ambalo linawapa thawabu kubwa sana, tungependa kuwashukuru sana kwa sababu serikali peke yake haiwezi kulea yatima na makundi yasiyojiweza.”

Spika Ndugai ameongeza kuwa TIF imekuwa ikitekeleza kwa vitendo sera za serikali katika kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama kwa kuwachimbia visima.

Pia Spika amesema kuwa TIF imekuwa ikifanya shughuli zake kwa uweledi wa hali ya juu na kwamba Serikali hususan Bunge linaunga mkono jitihada za taasisi hiyo zikiwemo za kuwasaidia wabunge majimboni katika masuala ya maendeleo.

Akiwa hapo TIF, spika Ndugai alifanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa taasisi hiyo akiwemo Mwenyekiti Aref Nahdi, Mkurugenzi Mtendaji wa TIF, Sheikh Ibrahim Twaha na Mkurugenzi wa TIF Mwanza, Sheikh Abdul Abeid.

Aidha spika Ndugai aliweza kutembelea vituo vya matangazo vya Radio pamoja na TV Imaan ili kujionea shughuli zinazofanywa na vyombo hivyo vya habari katika kuuhabarisha umma wa Kiislamu na Watanzania kwa ujumla. Kwa upande wake Mwenyekiti wa TIF, Aref Nahdi amesema ujio wa Spika Ndugai ni faraja kubwa kwa taasisi hiyo na unaonesha jinsi kazi za TIF zinavyotambuliwa na serikali.

“Ujio wake unatufariji sana watu wote hapa, ujio wake ulikuwa wa ghafla sana na kwa kweli ametuonesha mapenzi makubwa sana na tumefarijika zaidi alipotuambia kwamba wanaelewa nini inafanya The Islamic Foundation (TIF),” alisema Mwenyekiti Nahdi.
Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close