1. Habari1. TIF News

‘TIF Girls’ wawafariji watoto Muhimbili

Vijana wa kujitolea wa taasisi ya The Islamic Foundation upande wa wanawake (TIF Girls) wameendeleza utaratibu wao wa kujitolea kusaidia masuala anuai ya kidini na kijamii, ambapo hivi karibuni waliwatembelea watoto wenye maradhi ya vichwa vikubwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa lengo la kuwafariji.

Safari hiyo ni mwanzo wa azma endelevu ya kutembelea wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi tofauti katika hospitali mbalimbali za jijini Dar es Salaam na baadaye nchi nzima kwa lengo la kuwajulia hali, kuwafariji, kukidhi baadhi ya mahitaji yao na kuwasaidia inapowezekana. Vijana hao walifika katika hospitali ya Muhimbili mnamo Jumapili ya tarehe Agosti 26 majira ya saa tatu asubuhi ambako walipokelewa vizuri na uongozi wa hospitali hiyo, kisha walipelekwa katika wodi ya MOI ghorofa ya tano ambayo ni mahususi kwa watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa.

Wasichana hao wanaojituma katika kheri, walipata wasaa wa kuwafariji watoto hao kwa kuwajulia hali watoto hao, kucheza nao, kuwasikiliza wazazi wao juu ya matatizo na changamoto mbalimbali walizonazo na kuwapatia zawadi kadhaa walizokwenda nazo kwa ajili ya kukidhi baadhi ya haja zao.

Miongoni mwa mambo yaliyowavutia katika safari  hiyo ni kupewa elimu ya kitabibu juu ya maradhi hayo ya vichwa vikubwa. Kwa mujibu wa madaktari, kichwa kikubwa ni ugonjwa unaotambulika kitaalamu kama Hydrocephalus, ambalo ni neno lenye asili ya kigiriki lenye maana ya maji ndani ya kichwa. Hata hivyo, sio kila mwenye kichwa kikubwa ana hydrocephalus. Madaktari walisema, kwa kawaida ndani ya ubongo kuna sehemu nne zenye uwazi, ambazo wataalamu huziita ‘ventricles.’  Madaktari walisema, sehemu hizo huwa haziko wazi bali huwa na kiasi fulani cha majimaji yanayojulikana kitaalamu kama ‘cerebral spinal fluid’ ambayo hutengenezwa kwenye damu na seli ambazo zipo kwenye kuta za ‘ventrices.’

Madaktari waliongeza kuwa, majimaji hayo ambayo hutengenezwa ndani kabisa ya ubongo kwenye hizo ventricle hupitia sehemu maalumu na hivyo kutoka nje ya ubongo na kuuzunguka, jambo ambalo hupelekea kuufanya ubongo kuelekea kwenye majimaji hayo. Kwa maana hiyo, madaktari walisema, ndani kabisa ya ubongo kuna chumba au chemba (ventricles) ambazo huwa zina maji kwa nje ubongo umezungukwa na hayo maji. Ili kuhakikisha maji hayo hayazidi kichwani, mwili unao mfumo kamili unaohakikisha kuna uwiano kati ya maji yanayotengenezwa na maji yanayofonzwa na kurudishwa kwenye damu.

Majimaji hayo yana faida nyingi, moja miongoni mwa hizo ni kuweka uwiano wa msukumo (balance intracranial pressure) na kuzuia mtikisiko wa ubongo (shock absorber).

Yapo baadhi ya magonjwa ambayo hufanya majimaji hayo yatengenezwe kwa wingi kuliko yanavyorudishwa mwilini au utengenezazwaji wa majimaji hayo unaweza ukawa wa kawaida lakini ufyozwaji haupo. Ikitokea hali hali, maji hujazana kichwani na kufanya kichwa kiwe kikubwa.

Magonjwa hayo yanayoleta hitilafu katika uwiano wa maji, ikiwemo yale ambayo mtoto amezaliwa nayo, yaani ‘congenital defect’. Pia mtoto anaweza asizaliwe na shida hiyo lakini akaipata baadaye kutokana na kupata magonjwa yanayoshambulia sehemu zinazofyonza maji hayo. Magonjwa hayo ni kama Meningitis, Toxoplasmosis, Cytolomegalovirus nk. Lakini pia kama mtoto atapata baadhi ya kansa ambazo zinashambulia utando unaozunguka ubongo (meninges), anaweza kupata shida hiyo.

Kwa mujibu wa madaktari, tiba ya kujaa maji kichwani ni kuweka mpira (tube) unaoitwa ‘VP shunt set,’ kutoka kichwani na kuyapeleka maji hayo tumboni na hapo tumboni hufyonzwa na kurudishwa kwenye damu.

Wasichana hao wanaojituma katika kheri, walipata wasaa wa kuwafariji watoto hao kwa kuwajulia hali watoto hao, kucheza nao, kuwasikiliza wazazi wao juu ya matatizo na changamoto mbalimbali walizonazo na kuwapatia zawadi kadhaa walizokwenda nazo kwa ajili ya kukidhi baadhi ya haja zao.

Miongoni mwa faida walizopata vijana hao wa kujitolea wa TIF ni kujifunza kuhusu ugonjwa wa vichwa
vikubwa, kupandisha Imani zao kwa kutazama wagonjwa, kupata wasaa wa kunasihiana mambo mbalimbali ili kudumisha umoja na udugu wao wa kiimani na mwisho kabisa waliwaombea dua wagonjwa wote waliopo hospitalini hapo na maeneo mengine.

Wasichana hao wa TIF walishukuru uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwapokea na kuwapa ushirikiano katika kipindi chote cha ziara yao, bila ya kuwasahau watu wote walioshirikiana nao kwa njia moja au nyingine kwenye kufanikisha ziara yao.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close