1. Habari

Tanzania kugeuka taifa la wacheza kamari?

Gazeti la Imaan mara nyingi limekuwa likiandika habari za madhara ya kamari, kiasi kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakidhani chombo hiki kinatia chumvi tu na kwamba madhara si makubwa kihivyo!!

Kama ulikuwa unafikiria hivyo fikiria upya; kwani, sasa hivi hadi maprofesa katika vyuo vikuu mbalimbali wabobezi katika utafiti na tafakuri za kina wanaona madhara ya kamari kiasi cha kuibua suala hilo katika majukwaa makubwa yanayojadili maendeleo kitaifa na kimataifa.

Kauli ya hivi karibuni ya kukemea kamari imetolewa na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bi. Agnes Nyomola, ambaye yeye ni mtaalamu wa sayansi ya mimea [Botany] alipokuwa akichangia mada katika Kongamano la Kutathmini hali ya Uchumi na Siasa katika miaka mitatu ya utawala wa Rais Magufuli.

Katika mchango wake, Prof. Nyomola alionya, mbele ya Rais John Magufuli, kuwa, isipoangalia Tanzania inaweza kuwa inatengeneza taifa la wacheza kamari.

Kuna kitu ambacho mimi kinanisikitisha kinachoendelea sasa hivi. Kuna vitu vimezuka sasa hivi vya [akataja jina kampuni moja ya kuchezesha kamari] sijui kubeti, sijui… vitu vya ajabu. Tusipoangalia tutatengeneza taifa la wacheza kamari,” alisema Prof Nyomola.

Prof. Nyomola alisema kamari inaathiri vijana wengi, ambao ndio nguvu kazi na wakiwa pia ni asilimia 52 ya Watanzania wote, hivyo basi, ni bora nchi iwaangalie kwa macho ya karibu na kuwaweka katika mstari kielimu, kiroho na kiimani ili waje kuwa waendeshaji wazuri wa nchi hii. Prof. Nyomola alisema, anachojua yeye, kucheza kamari kidini ni dhambi, na pia ni kosa la jinai, na ndio maana hata nchi zilizoendelea, kwa kuelewa madhara ya kamari, kuna maeneo maalumu ya michezo hiyo tofauti na Tanzania ambako kamari inachezwa hadharani, vijijini mpaka mijini.

Katika mataifa yaliyoendelea, mathalani Marekani, ukitaka ‘kugamble’ unaenda Las Vegas. Kwa nini sisi tunafanya hivi vitu nje nje, katoto kadogo kashajua kubeti?” alilalamika Prof. Nyomola.

Prof. Nyomola pia alikanya dhidi ya tabia ya vijana kutafuta njia za mkato [shortcuts] za kutafuta pesa, ikiwemo kamari.

Ukimwambia akutengenezee hata bustani hapo mbele ya nyumba hawezi kwa sababu ya hizo shortcut za hela ya haraka haraka.”

Ili kusoma makala yetu iliyopita kuhusu uchezaji wa kamari nchini, bonyeza kiuongo hiki👇👇👇…

Kamari: Hawajui uharamu wake au uasi?

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close