2. Taifa

Mwaka 1440 Hijiriya, muda wa kujitathmini

Ikiwa tumeingia mwaka mpya wa 1440 Hijriya, Waislamu mbalimbali hapa nchini na duniani wamenasihiwa kujitathmini juu ya uhusiano uliopo baina yao na Muumba wao, pia, kudumisha umoja miongoni mwao kwa kuacha kufarakana kwa mujibu wa makundi.

Baadhi ya Masheikh waliozungumza na gazeti imaan wamewataka Waislamu kuupokea mwaka mpya wa Hijriya kwa kuyahama maasi na kupupia mambo mema kwani hiyo ndio njia itakayowafanya wapate radhi za Mola wao. Aidha, masheikh hao wamesisitiza kuhusu umuhimu wa kila muislamu kujiepusha na mambo yanayopelekea katika shirki na badala yake wamuelekee Allah kwa kushikama na Tauhidi.

Katibu Mkuu wa Baraza la Sunna (BASUTA) nchini, Sheikh Shaaban Mussa amewataka Waislamu kujitathmini kabla kufanyiwa tathmini. Pia, aliwaasa Waislamu kote nchini wasijisahau na wala wasizisahau au kuwa tayari kusahaulishwa kadhia mbalimbali zinazoukwaza Uislamu au kuwakwaza wao kama jamii ya Kiislamu.

Akifafanua zaidi, Sheikh Shaaban alisema: “Kila mmoja wetu ajitahidi kumuabudu Mwenyezi Mungu kama alivyofundisha au tulivyofundishwa na Mtume wake kwa mujibu wa uelewa wa wema waliotangulia, yaani bila kuzusha jambo lisilokuwa na asili katika dini.”

Aidha, Sheikh Shaaban alisema: “Sote tunajua kama hivi sasa tupo kwenye kituo cha pili, na kabla ya hapo tulikuwa kwenye matumbo ya mama zetu, na kila mmoja muda wake ukifika atakufa na ataingizwa kaburini na ambacho ni kituo cha tatu, na huko kaburini kunahitaji amali na maandalizi ya kutosha. Je, umejiandaaje?”

Sheikh Shaaban pia aliwalaumu  Waislamu wanaowasaliti na kuwahilikisha wenzao kwa uonevu. Alisema: “Ni vema wakajichunguza, wakajitathmini, na wakajiuliza! Kwa umri alionao mtu sasa, hivi amebakisha miaka mingapi ya kuishi hapa duniani? Kama hajui na hana jibu! Je, haujafika wakati wakujitathmini?”“Kusanya chochote ukitakacho hapa duniani, lakini ukumbuke ipo siku utaondoka hapa duniani kama uliyokuja,” alionya Sheikh Shaaban.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa BASUTA, Sheikh Muhammad Issa, alisema katika tathmini yake ya mwaka mpya wa Hijriya kuwa, Watanzania wana haja ya kujitathmini kuhusu ibada ya Hijja, kwani takwimu za idadi ya Watanzania wanaokwenda kufanya ibada hiyo nchini Saudi Arabia zinaonesha kuwa ni ndogo ikilinganishwa na idadi halisi ya mahujaji wa nchi hiyo wanaotakiwa kwenda huko kila mwaka.

Sheikh Muhammad alisema, Tanzania imepewa idadi ya kupeleka mahujaji 25,000 kila mwaka lakini kwa mujibu wa ripoti ya Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia ni kwamba katika msimu wa Hijja mwaka huu 2018 kati ya idadi hiyo ya elfu 25 ni takribani mahujaji 3,000 (10%) ndiyo waliyokwenda Hijja.

Kwa upande wake, Imamu wa Masjid Istiqaama iliyopo Mbezi mwisho, jijini Dar es salaam, Sheikh Ramadhani Abdi amewanasihi Waislamu waupokee mwaka mpya wa Hijriya kwa kufanya sana ibada, toba ya kweli na kumuomba msamaha Mwenyezi Mungu. Aidha aliwataka Waislamu waache kufanya mambo kimazoea, bali wajifunze elimu sahihi ya dini yao.

Sheikh Abdi alisema: “Ni muhimu kujitathmini juu ya ibada tunazofanya kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Kwanza tunaendelea kuhesabu miaka tukiwa ni wenye kuzaliwa na wengine kufa. Hata hivyo, sisi sote ni wapita njia, tumeletwa dunia kwa sababu moja tu, nayo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu.”

Naye, Katibu wa Mudir wa Kituo cha Kiislamu cha Kimisri (Al-markaz Al-islamiy) kilichopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Sheikh Yahya Mkali aliwataka Waislamu waanze kumrudia Mwenyezi Mungu na kufanya ibada kwa wingi. “Waislamu waanze kufanya ibada kwa wingi, waache kufanya mambo mabaya ambayo yatawagharimu siku ya kiyama,”

Alisema Sheikh Mkali huku akinukuu Hadithi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ninayosema: “Hijra iliyokuwa bora zaidi ni kuhama yale anayochukia Rabb [Mola] wako,” [An-Nasai].

Lakini je, ni ipi hasa sababu ya kujitathimini kila mwaka unapomalizika? Miaka ya Kiislamu imeanza kuhesabiwa baada ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kuhama kutoka Makka kwenda Madina. Umar (Allah amridhie) alitoa ushauri kuwa, kwa vile ni mara ya kwanza wanahamia katika mji unaotekelezwa Sharia ya Kiisalmu, basi ni bora kuanza kuhesabu miaka kwa kuanzia mwezi huo waliohama, ambao ulikuwa ni mwezi wa Muharram.

Na pia inasemekana kuwa Umar (Allah amridhie) alikuwa akipokea barua kutoka kwa Magavana (watawala) wa nchi mbalimbali zilizokuwa chini ya Uislamu, ambao wakati huo zilikuwa zikiandikwa majina ya miezi bila mwaka. Umar aliwashauri Maswahaba wenzake (Allah awaridhie wote) juu ya kufikiria suala la kuanzisha tarehe. Wapo waliopendekeza tarehe zianze kwa kufuata miaka ya Kirumi, na waoo waliopendekeza zianze kwa miaka ya kifursi. Mwishowe wakakubaliana ianze pale alipohama Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kutoka mji wa Makka kwenda Madina.

Hivyo, wakati tunaingia mwaka 1440 wa Hijriya kila Muislamu anapaswa kujitahmini juu ya kile alichomfanyia Mwenyezi Mungu katika ibada zake. Huu ni wakati mwingine kwetu kufanya tathmini ya matendo yetu mienendo yetu na mustaqbali wa dini yetu. Tushukuru kuudiriki mwaka wa 1440 Hijriya, pia tubadilike. Allah atujalie kuuanza vema mwaka huu kwa kwa heri na amani.

 

Hivyo, wakati tunaingia mwaka 1440 wa Hijriya kila Muislamu anapaswa kujitahmini juu ya kile alichomfanyia Mwenyezi Mungu katika ibada zake

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close