2. Taifa

Mahujaji wazinduliwa kuhusu hati za kusafiria

Wakati taasisi za Kitanzania za kusafirisha mahujaji zikiwa katika maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kuelekea mjini Makka, nchini Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hijja mwezi Julai mwaka huu, viongozi wa taasisi hizo wamewataka Waislamu wanaotarajia kwenda Hijja ambao hati zao za kusafiria zina uhai wa chini ya miezi sita kubadilisha hati zao za kusafiria kabla ya Julai 2019. Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Taasisi ya kusafirisha Mahujaji ya M2 Travel, Mohsin Mohamed Hussein, alisema kuwa kubadilisha hati mapema kutawasaidia mahujaji kuondokana na usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa safari.

“Kwa kuelewa kuwa mahujaji wengi wanajitokeza siku za mwisho kukamilisha taratibu za safari, sisi kama viongozi wa taasisi za usafirishaji tunawahimiza na kuwasisitiza wale walioko mikoani wafike jijini Dar es Salaam mapema kwa ajili ya kubadilisha hati zao,” alisema Mohsin.

Wito huo wa Muhsin, unafuatia taarifa iliyotolewa Juni 3, mwaka huu na Idara ya Uhamiaji hapa nchini inayosema kuwa, hati mpya ya kusafiria inatakiwa iwe na uhai wa angalau kuanzia miezi sita ili mwenye hati hiyo aweze kuomba Visa ya nchi anayotaka kwenda na kuruhusiwa kuondoka kupitia vituo vya kuingia na kutoka nchini.

Kwa ajili hiyo basi, Waislamu wote wanaotarajia kwenda Hijja mwaka huu, na ambao hati zao zina sifa hiyo, wanapaswa kupata hati mpya kabla ya Julai Mosi, 2019 ili waruhusiwe kwenda Makka nchini Saudi Arabia.

Hata hivyo, Mohsin alitoa angalizo kuwa huenda idadi ya mahujaji watakaokwenda nchini Saudi Arabia mwaka huu ikapungua kutokana na baadhi yao kuwa safarini na wengine kuishi maeneo ya vijijini, ambayo ni nadra mtu kufikiwa na taarifa. “Ukizingatia hayo yote unaona kabisa kuwa idadi ya mahujaji huenda ikapungua, kwani ni wiki mbili tu zimebaki kabla ya zoezi kufungwa,” aliongeza kusema Mohsin. Kufanyika kwa zoezi la kubadilisha hati za kusafiria kutoka zile za zamani, yaani MRP hadi mpya (E–Passport) ni utekelezaji wa mpango mkakati wa serikali katika kubadilisha huduma zinazotolewa na serikali ili zifanyike kidigitali au kwa kutumia teknolojia. Kulingana na taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhamiaji, mwisho wa matumizi ya hati za zamani za kusafiria ni Januari 31, 2020.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close