1. Habari

Swala inahitaji maandalizi-1

Swala ni nguzo ya pili katika nguzo za kiislamu, na ni ibada kongwe iliyotekelezwa na Mitume wa zama zote pamoja na wafuasi wao. Swala pia ni kigezo kikuu cha ukweli wa Uislamu wa mtu. Kuitekeleza swala ni sababu ya kukingwa na adhabu ya moto huko Akhera, kupata radhi za Allah  na kuingizwa Peponi. Vile vile kuiacha Swala ndio sababu kuu ya kuingizwa motoni siku ya kiyama, Allah atuepushe na hayo!

 

Lengo la Swala
Kupitia Qur’an na Sunna, tunajifunza kuwa lengo la Swala hapa duniani ni kumtakasa mja dhidi ya madhambi na kumkataza na mambo ya aibu, maovu na machafu. Allah amesema: “Soma uliyofunuliwa katika kitabu na simamisha swala. Hakika ya swala (ikiswaliwa vilivyo) hukataza maovu na machafu, na utajo wa Mwenyezi Mungu (uliomo ndani ya swala) ni mkubwa zaidi na Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo,” (Qur’an 29:45).

Kiuzoefu, shughuli ama kazi yoyote ambayo inatarajiwa kuleta matokeo mema huhitaji maandalizi ya muda mrefu au angalau mfupi kutegemea ukubwa wa kazi hiyo. Shughuli itakayofanywa bila ya maandalizi mnasaba na ya kutosha, kamwe haileti fanaka wala kufikia lengo.

Baya zaidi humgharimu mtendaji mali na wakati pasipo kuvuna chochote ila majuto na machofu. Mara nyingi wanadamu hulazimika kutumia muda, akili na pesa nyingi katika kuandaa shughuli zao kwa kuwa wanataka zipendeze na kuleta matokeo yatakayowafurahisha wahusika. Tuchukue mfano wa sherehe ya harusi.

Baada ya kukamilika hatua za posa, ulipaji mahari na kupangwa siku ya sherehe; wahusika wa pande mbili hushughulika sana katika kuandaa vyakula, mavazi maalumu ya kupendeza kwa Bwana na Bi harusi, mialiko hutolewa pamoja na kuandaliwa vitu vingi vyengine. Yote hayo yanafanywa ili sherehe ya siku moja tu ifanikiwe inavyotarajiwa.

Inawezekana maandalizi ya harusi moja tu yakachukua muda wa mwaka mzima. Hali ni hiyo hiyo panapotaka kufanywa mikutano, mihadhara, mechi za mipira ama maigizo. Waislamu tutakuwa tumefanya kosa kubwa sana iwapo tutakubaliana na ukweli huu katika mambo ya dunia yetu na kujisahaulisha kuhusu ukweli huu katika mambo ya ibada ambayo ndio lengo haswa la uwepo wetu juu ya mgongo huu wa ardhi.

Makala yetu ina nia ya kufafanua jinsi gani Muislamu anaweza kufanya maandalizi sahihi kwa ajili ya kuiendea swala yake ili Afikie lengo. Kadhalika tutabaini makosa wayafanyayo Waislamu wengi wanaposali ambayo yamekuwa sababu ya kutokulifikia lengo. Hivyo, mpendwa msomaji! Fuatilia vyema makala hii muhimu unufaike, huku tukimuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kuihudhurisha na atunufaishe kwayo.

Maandalizi ya swala
Idadi ya Waislamu wanaoonekana wakipigana vikumbo kwenye mahodhi ya kuchukulia udhu na kisha milango ya misikiti ni kubwa si haba. Hili ni jambo zuri kwani huonesha uwepo wa Uislamu katika eneo husika.

Lakini swali la msingi ni, kiasi gani cha maandalizi sahihi kwa ajili ya swala waliyoyafanya waumini hawa, ambao baada ya kumaliza ibada zao hujipa matumaini makubwa kwamba wamefanya ndivyo na kusubiri Allah awarehemu?

Kujiandaa kwa ajili ya ibada ya Swala ni pamoja na kuisoma Swala na kujua masharti, nguzo, sunna na miiko yake; na vilevile kujua utaratibu mzima wa utekelezaji swala, pamoja na kulielewa vyema dhumuni (lengo) halisi analotakiwa mwenye kuswali alifikie.

Maandalizi mengine ni ile nidhamu ya wakati wa kuiendea Swala yenyewe. Takriban makosa yote wanayoyafanya waislamu hadi wakaonekana kama wanacheza wanapoiendea au wanapokuwa katika ibada ya swala huwa yanatokana na ukosefu wa maandalizi na utayari wa kutosha kwenye maeneo tuliyoyagusia. Kwa mfano, wakati fulani tunaweza kumuona mmoja wetu anajikuna mgongoni au ananyanyua kichwa akiangaza macho yake kiasi cha kumjua kila aingiae na atokae msikitini, au labda anaangalia saa kwenye ukuta wa msikiti au iliyo mkononi mwake, au kuchezea ndevu zake.

 

Katika tukio kama hilo, inatubainikia dhahiri kwamba muhusika amekosa kujua nafasi na utukufu wa anayezungumza naye, Allah Mfalme wa Wafalme, Muumba wa kila kitu kwani vitendo hivyo hawezi kuvifanya hata mbele ya mheshimiwa diwani, Mheshimiwa rais, ambao wote hawa
ni viumbe wenzake tu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close