1. Habari

Swala inahitaji maandalizi -2

Kutokana na aya 29:45 katika Qur’an tuliyoitaja katika toleo lililopita na ambayo tutakuwa tukiirejearejea, tulijifunza kuwa,Swala ni nyenzo kubwa ya kumkinga mja na jamii kwa ujumla dhidi ya maovu na machafu. Pia, tuliona kwamba, kukingwa dhidi ya maovu, ndio haswa lengo la agizo la Muumba kwetu la kutekeleza ibada ya swala…

Kazi kubwa inayomkabili kila Muislamu ni kujifunza falsafa iliyotumika kupata msukumo uliomo katika Swala unaomzuia kufanya maasi; nayo, kwa hakika, si kazi ndogo.

Bila shaka utajo (kumzingatia Allah) kunakopatikana katika utekelezaji wa Swala na ahadi za kiroho anazoziweka mja mbele ya Mola wake, tokea wakati wa maandalizi (twahara) hadi salamu, ndio msukumo unaomzuia mja na maovu na machafu.

Allah Aliyetukuka anasema: “…bila shaka Swala ikisaliwa vilivyo, humzuilia (anayesali) na mambo machafu na maovu, na kwa yakini kumbuko la Mwenyezi Mungu lililomo ndani ya Swala ni jambo kubwa (la kumzuilia mtu na mabaya) Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.”

Twahara Moja ya maandalizi muhimu ya kuyazingatia kuelekea katika Swala ni twahara. Maana ya twahara ni kuondoa hadathi na najisi katika mwili, nguo na sehemu ya kusalia.

Katika Qur’an Allah Aliyetukuka anatueleza: “Enyi mlioamini, mnaposimama kwenda kusali basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake (maji) vichwa vyenu na (osheni) miguu yenu mpaka vifundoni, na mkiwa na janaba basi ogeni; na mkiwa wagonjwa au mmo safarini au mmoja wenu ametoka chooni au mmeingiliana na wanawake na hamkupata maji basi kusudieni (tayamamuni) udongo (mchanga) uliosafi na kuupaka nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika tabu bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.” (Qur’an, 5: 6).

Hii ni aya inayowataka Waislamu kabla ya kusimama mbele ya Mola wao, Mfalme wa wafalme kufanya maandalizi kwanza, nayo ni twahara. Twahara kisheria huzingatiwa kuwa ndio sharti mama la Swala.

Kuosha viungo vilivyotajwa katika aya hiyo kunajulikana kama kutia udhu. Viungo hivi vinatakiwa vioshwe kwa utulivu, uangalifu na kwa umakini sana, kwani kuwa na papara wakati wa kutia udhu hupelekea kuviacha vikavu, lakini pia humtia mja hatiani.

Mtume ameonya kwa kusema: “Ole wao na moto wenye kubakisha visigino vyao vikavu,” yaani adhabu kali itawastahikia wasiotimiza udhu wao ambao huviacha baadhi ya viungo vyao vikavu. Aya pia inatutaka tuchukue tahadhari dhidi ya najisi (haja kubwa na ndogo) tunapokuwa chooni na tujiepushe na cheche za mikojo kwenye nguo na miili yetu.

Mtume ameonya kwa kusema, katika hadithi ambayo hata hivyo baadhi ya wanazuoni wamesema sanad yake ni dhaifu: “Hakika ukubwa wa adhabu ya kaburini husababishwa na kutokujikinga na mikojo.”

Allah katika aya tuliyoitaja, pia ametutaka tunapopatwa na janaba tukoge kwa kueneza maji mwili wote, na kwamba haitoshi kuosha tu viungo vya udhu. Kadhalika, katika aya tuliyoinukuu pia vile vile imetaja twahara ya dharura nayo ni kutumia mchanga badala ya maji pale yanapokosekana au katika hali ya ugonjwa usioruhusu kuyatumia. Kadhalika, aya imeashiria kuwa kuamrishwa twahara ni sehemu ya utimizaji wa neema za Allah kwa waja wake.

Katika Sunna

Umuhimu wa maandalizi haya (twahara) kwa ajili ya kuielekea ibada ya Swala vile vile tunaupata katika sunna. Mtume amesema: “Kifunguzi cha Swala ni twahara, na huhirimiwa kwa takbir, na hufunguliwa kwa salamu.” Na katika hadithi nyingine, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amewaelekeza Waislamu kivitendo namna ya utekelezaji wa agizo lililokuja katika aya hii.

Uthman bin Affan (Alllah amridhie) alitawadha, alipomaliza aliwaambia watu: “Nimemuona Mtume wa Allah akitawadha mfano wa udhu wangu huu. Kisha akasema: “Atakayetawadha kama hivi husamehewa dhambi zake zilizopita…” (Muslim).

Qur’an na Sunna vinatutaka tufahamu kwamba, twahara ni sharti na ni ibada ya lazima kabla ya kuingia kwenye matendo ya swala. Mja akiitenda sawa ibada (swala) itakubalika na akiiharibu basi Swala haitakuwa na maana yoyote.

Falsafa ya udhu

Katika fiq-hi ya Swala tunajifunza kuwa viungo vya udhu vinatakiwa viwe safi wakati Muislamu anataka kuchukua udhu. Hili linatufanya kujiuliza: basi kuna haja gani ya kuviosha tena viungo hivyo? Kumbe lengo hasa la udhu si kuondoa vumbi ama uchafu, bali kuchukua ahadi mbele ya Mola wetu za utiifu kupitia viungo vyetu hivi muhimu.

Muislamu anapoosha viganja au mikono yake, anamuahidi Allah kuwa hatoitumia mikono hiyo kwa kutoa au kupokea vya haramu au kwa kuwadhuru wengine.Anaposukutua, anausafisha ulimi wake na dhambi na kumuahidi Allah kuwa, siku zote atautumia kwa yanayomridhisha na kamwe hatotamka dhambi au maasi.

Anapoosha uso, anamuahidi Allah kwamba, hatoyatumia macho yake kuvitazama vya haramu au kumnyenyekea mwengine kwa kumuabudu au kumuomba zaidi ya Allah Aliyetukuka. Akipangusa kichwa na masikio yake, anaisafisha akili yake na dhana potofu ya kumdhania Mwenyezi Mungu na kumuahidi daima ataitumia akili yake kuyawaza ya heri. Pia, humuahidi Allah kwamba hatosikiliza ya haramu na daima atayatumia masikio yake kwa kuyasikiliza ya heri.

Na anapoosha miguu yake anamuahidi Allah kwamba, hatoitumia katika kuyaendea ya haramu na maasi, bali ataitumia kuyaendea yanayomridhisha Mola wake. Katika hadithi iliyosimuliwa na Abuu Huraira, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Muislamu akitawadha na kuosha uso wake, hutoka kwenye uso wake dhambi zote alizozichuma kwa macho yake pamoja na tone la mwisho la maji. Akiosha mikono yake, dhambi aliyoichuma kwa kushika huondoka pamoja na tone la mwisho la maji. Akiosha miguu yake dhambi zote alizoziendea kwa miguu hiyo hutoka pamoja na maji ya mwisho, mpaka anatoka (kwenye udhu) akiwa ameshatakaswa na dhambi.” (Muslim; pia Taz: Riyaadh Swaalihyn Uk 334-335).

Kutokana na hadithi hii, tumeanza kuona siri ya msukumo ulio katika ibada hii tukufu tangu tukiwa katika maandalizi. Ni ile hisia ya kumzingatia Allah anayokuwa nayo Muislamu wakati anapoosha viungo vyake vilivyo safi tayari, ‘waladhikru llaahi akbar.’ Iwapo atayafanya maandalizi haya kwa utulivu na umakini huanza kufutiwa dhambi zake kabla hata ya kusimama
kwa ajili ya kuitekeleza ibada yenyewe ya swala. Tunamuomba Allah atuongoze waja wake.

Swala inahitaji maandalizi-1

 

Swala inahitaji maandalizi-3

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close