1. Habari

Mufti akemea ushoga

Wakati mijadala ya sakata la ushoga likiendelea nchini na duniani, Mufti  Sheikh Abubakar Zubeir ametoa neno lake na kusema, vitendo hivyo vichafu havikubaliki ndani ya Uislamu na jamii kwa ujumla.

Mufti Zubeir aliwaambia waandishi wa habari kuwa, vitendo vya kishoga ni kiashiria kibaya cha mmomonyoko wa maadili katika jamii:

Uislamu haukubali ushoga, Uislamu unakataza juu ya masuala haya, kwa sababu kama tunazungumzia mmomonyoko wa maadili; huo ndio mmomonyoko zaidi,” alisema Mufti Zubeir.

Mufti Zubeir alisema hakuna dini yoyote ulimwenguni inayokubali jambo hilo na kwamba ni lazima likemewe na kila mtu wakiwemo viongozi wa dini. Aidha Mufti Zubeir alisema, mmomonyoko wa maadili unatokana na watu kukosa tabia njema na hivyo kuitaka jamii nzima kusimama kidete katika kuhakikisha maadili yanatamalaki katika jamii.

Nasaha zangu kwa umma na kwa taifa zima tushikamane juu ya malezi bora, malezi yenye maadili, kuangalia vijana na watoto wetu na kufundisha tabia njema ndani ya majumba yetu na nje ya majumba yetu na shuleni,” alisema Mufti.

Kwa upande wake, Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam (Bakwata), Alhadi Mussa Salum akiongea kupitia mkanda wa video uliosambaa mitandaoni amesema kuwa ushoga ni miongoni mwa dhambi kubwa na umekatazwa katika dini zote:

Katika dhambi kubwa baada ya shirki ni liwati, jambo hili limekatazwa ndani ya vitabu vyote vya dini na limelaaniwa,” alisema Sheikh Mussa.

Sheikh Mussa alisema, ushoga haulipi, na unaweza kuangamiza jamii kama kilivyoangamizwa kizazi cha Luti wakati wa Sodoma na Gomora kutokana na matendo ya kulawitiana wanaume kwa wanaume.

Kauli za masheikh hao zimekuja mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutangaza dhamira ya kuwasaka watu wanaojihusisha na ushoga, hatua ambayo hata hivyo ilipingwa kupitia tamko la Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa hapo Novemba 4 mwaka huu. Tamko hilo lilisema hatua hiyo ya Makonda ni msimamo wake binafsi na si msimamo wa Serikali.

Hata hivyo, naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akiongea Bungeni hivi karibuni alisema vitendo vya ushoga ni kinyume cha sheria za hapa nchini na kwamba Serikali haiwezi kuvivumilia.

Hii si mara ya kwanza taifa kujikuta katika mjadala huo wa ushoga, itakumbukwa mwaka 2011, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alitoa msimamo mkali dhidi ya vitendo hivyo.

Msimamo wa Membe ulikuja kufuatia kauli ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron kusema kuwa nchi itakayokataa ushoga itanyimwa misaada.

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close