1. Habari1. TIF News

MISKI YA ROHO TENA…

Salamu alaykumu, kipazani najongea.
Ndugu zangu isilamu, ujumbe nawaletea.
Miski tuliyoihamu, punde tu itatujia.
Roho zipate nukia, miski inatulazimu.

Uturi huu muhimu, TIF yatusogezea.
Mashekhe walo adhimu, toka kwetu tanzania.
Hata watokao lamu, burundi uganda pia.
Roho zipate nukia, miski inatulazimu.

Tusiwazie ugumu, ni nafuu nawambia.
Shilingi si darahimu, elfu tano kuchangia.
Tiketi kila sehemu, hata kwa simu lipia.
Roho zipate nukia, miski inatulazimu.

Kwani atatia timu, ba sheghele twamjua.
Ataja ondosha ghamu, bizimana maridhia.
Yusufu wa taadhimu, nyuma hawezi bakia.
Roho zipate nukia, miski inatulazimu.

Bure tusijialumu, wawili wafanania.
Mashekhe wenye nidhamu, orodha yajisemea.
Ni shekhe Ally mwalimu, na wa kigali sawia.
Roho zipate nukia, miski inatulazimu.

Siku hiyo ni karamu, Muhammadi tatongoa.
Thumma atapewa zamu, She’ Jamali mwenye twaa.
Asukume gurudumu, uturi kunyunyizia.
Roho zipate nukia, miski inatulazimu.

Kumbuka ile awamu, mazuri yalotokea.
Tulivyochota elimu, mengi tulivyong’amua.
Kunenwa mada muhimu, hata ghuna kusikia.
Roho zipate nukia, miski inatulazimu.

Miski huondosha sumu, bongoni iliyojaa.
Kujikinga jahanamu, mbinu tutazigundua.
Mola atatukirimu, thawabu kutujazia.
Roho zipate nukia, miski inatulazimu.

Mwisho nafunga nudhumu, ukumbi kuwaambia.
Wale msopafahamu, Diamond ulizia.
Chonde usijidhulumu, kikosa utajutia.
Roho zipate nukia, miski inatulazimu.

*****

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close