1. Habari1. TIF News

Kauli ya Mwenyekiti TIF, Misk ya Roho II

Awali ya yote nimshukuru Allah (Subhanahu wata’alah) kwa kuendelea kutuazima pumzi yake na kututunuku afya na nguvu za kuweza kuandaa Kongamano la pili la Misk ya Roho mwaka 2018.

Kongamano hili la pili litakalofanyika Oktoba 28 katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini hapa jijini Dar es Salaam, limeandaliwa kufuatia lile la kwanza lililofanyika kwa mafanikio makubwa Novemba 26 mwaka jana katika ukumbi huohuo.

Katika wadhifa wangu kama Mwenyekiti wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), natumia fursa hii kwa niaba ya taasisi nzima na idara zake, kwa unyenyekevu wote, kuwakaribisha Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu katika kongamano hili. Kama ilivyowahi kuwa kwa makongamano mengine yote yaliyowahi kuandaliwa na taasisi yetu, hili ni kongamano lililoandaliwa katika ubora mkubwa kwa lengo la kuacha athari chanya, In shaa Allah tukitumai.

Waislamu watapokea ujumbe maridhawa uliosheheni mafunzo ya kiimani na tafsiri pana ya maisha ya mwanadamu hapa duniani na akhera. TIF inaamini katika huduma bora, na ndio maana tumejitahidi kualika masheikh watoa mada, wazuri kutoka eneo zima la Afrika ya Mashariki ambao tunaamini watakata kiu ya hadhira itakayojitokeza ukumbini na walio majumbani watakaofuatilia kupitia runinga, redio na mitandao ya kijamii.

Hapa tunawazungumzia masheikh kama; Sheikh Yusuf Abdi na Sheikh Jamaldin Osman kutoka (Kenya), Sheikh Zuberi Bizimana kutoka Burundi, Sheikh Ally Kajura kutoka Rwanda na Sheikh Muhammad Abduweli kutoka Uganda. Hawa wataungana na masheikh wenyeji ambao ni pamoja na Sheikh Dourmohamed Issa, Sheikh Ally Jumanne na Sheikh Abdulrahman Mhina (Baba Kiruwasha).

Kama ilivyowahi kuwa kwa makongamano mengine yote yaliyowahi kuandaliwa na taasisi yetu, hili ni kongamano lililoandaliwa katika ubora mkubwa kwa lengo la kuacha athari chanya, In shaa Allah, tukitumai Waislamu watapokea ujumbe maridhawa uliosheheni mafunzo ya kiimani na tafsiri pana ya maisha ya mwanadamu hapa duniani na akhera. [Aref Nahdi]

Tunaamini masheikh hawa watakaowasilisha mada katika kongamano hili watakonga nyoyo za Waumini na Watanzania kwa ujumla, kama ambavyo wengine waliowahi kualikwa kwenye makongamano yaliyopita walifanya hivyo, akiwemo Sheikh Yusuf Estes (Marekani), Dkt Muhammad Salah (Egypt) na Sheikh Saeed Rageah (Canada). Pia kina Sheikh Saeed al Qadi (Uingereza) na Sheikh Edris Khamissa na Qari Ziyad Patel wote kutoka Afrika Kusini).

Hivyo narudia kutoa wito tena kwa Waislamu wote na hata wasiokuwa Waislamu kuhudhuria kongamano hili ili kuweza kupata ujumbe wa kida’awa ambao ni muhimu sana katika kujiandaa na maisha ya Akhera, tukizingatia kuwa: “Kila nafsi itaonja umauti.” [Qur’an 3:185]. Katika aya nyingine, Mwenyezi Mungu anasema: “(Allah) aliyeumba mauti na uhai ili akutahinini ninyi watu ni yupi mwenye matendo mema, na hakika Yeye ni Mwenye nguvu na Msamehevu.” [Qura’n 67:2] 

Mitihani hii bila shaka inakuja katika matendo yetu ya kila siku hapa duniani, ambayo baadhi yetu tunayafanya bila kuwa na uelewa wa usahihi wake. Basi kupitia kongamano hili, masheikh watatufafanulia masuala ya msingi katika dini yetu na kutupatia ramani ya kuiendea Akhera yetu kwa salama. Kwa mawaidha yao, masheikh watatusaidia kujirekebisha tunapokosea, kabla ya matendo yetu kupimwa Siku ya Malipo.
Shukran

Kabla sijatamatisha tamko langu, nitakuwa mnyimi wa fadhila kama sitotoa shukrani zangu za dhati kwa wadhamini wote wanaotuunga mkono katika makongamano yanayoandaliwa na TIF, kwani bila ya Allah kisha wao tusingeweza kuandaa kwa ubora uliokusudiwa.

Pia, napenda kuwashukuru wale wote ambao wamekuwa wakiunga mkono harakati za TIF za kusukuma mbele dini ya Allah, wakiwemo vijana wanaojitolea (volunteers). Wao, wanasimama kama watu muhimu katika maendeleo ya TIF na Uislamu kwa ujumla na hivyo nawasihi waendelee kuinga mkono TIF.

Vilevile, niwashukuru na kuwapongeza watendaji wote wa TIF katika idara mbalimbali kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha taasisi hiyo yenye makao yake makuu mkoani Morogoro inafikia malengo yake. Ifahamike tu kuwa wao nao ni sehemu muhimu ya mafanikio ya makongamano mbalimbali ya TIF likiwemo hili la Misk ya Roho II. Niwaombe wazidi kufanyakazi kwa moyo wote, kwani mafanikio ya TIF ndio mafanikio ya Uislamu, Waislamu na wao wenyewe.

Mwisho lakini si kwa umuhimu, niseme kuwa, maandalizi ya kongamano hili yatakuwa yamepotea bure kama walengwa hawakujitokeza kwa wingi ili kupokea mawaidha. Hivyo, kwa wote mtakaojitokeza ukumbini siku ya Oktoba 28 katika ukumbi wa Diamond Jubilee na watakaofuatilia katika vyombo vya habari. Asanteni sana.

Ninamali zia kwa kusema:
“Tumeahidi, tumetimiza na Allah ni shahidi.”

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close