1. Habari

MAISHA YA MASWAHABA: Salmaan al-Faarisy (Allah amridhie)

Wiki hii tunaanza kumzungumzia Swahaba aitwaye Salmaan al-Faarisy. Huyu ni Swahaba aliyepata umaarufu mkubwa nakupendwa sana na Waislamu kuanzia wakati wa Mtume hadi leo hii. Salmaan ambaye alitokea Fursi, (Iran ya leo), alipewa jina la ‘Assaii waraal haqiqa’ (mwenda nyuma ya haki).

Jina la Salmaan kabla ya kusilimu lilikuwa ni Ruuzba bin Jashbuudhan. Ni Swahaba huyu ndie aliyeshauri Waislamu wachimbe handaki katika vita vya Ahzaab katika mwaka wa tano Hijriya. Pia, alikuwa wa kwanza kuingia katika Uislamu miongoni mwa wasio Waarabu. Kisa cha safari ya kusilimu kwa Swahaba huyu kina mvuto, maajabu na mazingatio makubwa na ya aina yake hususan kwa wadadisi, watafiti wa mambo ya dini, na wanaotaka kuifikia dini ya haki.

Dkt Abdurahman Aafat Albshaa, amemnukuu Swahaba huyu akijielezea namna alivyoisaka dini ya haki hadi kuipata neema ya Uislamu. Salmaan anasema: “Nilikuwa kijana wa kifursi kutoka mji wa As-bahaan (kati kati ya Teheran ya leo). Baba yangu alikuwa chifu wa kijiji hicho na ni miongoni mwa matajiri wakubwa hapo, akinipenda tangu nilipokuwa mdogo. Nilipokuwa kijana, baba alinifungia ndani kama wafanyiwavyo wasichana, akiniogopea kuathiriwa na mifumo mingine ya nje.

Dini yetu ilikuwa ni Majuusiyya (waabudu moto na Jua) na nilikuwa mtekelezaji mzuri wa dini mpaka nikawa mtunzaji wa moto ambao tulikuwa tukiuabudu na kuhakikisha kuwa hauzimiki hata kwa muda mfupi. Baba yangu alikuwa na shamba kubwa likitupatia mazao mengi. Siku moja, baba alipata dharura fulani, hivyo hakwenda shambani. Akaniambia, ‘Mwanangu, mimi nimeshughulishwa kama unionavyo, basi hebu nenda ukalishughulikie. ’ Nikatoka nikaenda.

Njiani nikakuta moja ya makanisa ya Wakristo nikasikia, sauti za misa zao wakisali na kuimba. “Sikuwa nikijua lolote kuhusiana na (Ukristo na), Wakiristo wala wafuasi wa dini nyingine yoyote kwa vile baba alinizuia kabisa kuonana na watu. Niliingia ndani ya kanisa ili nijue wanachokifanya. Nilipoziona ibada zao, zilinifurahisha na kusema, ‘Dini yao ni bora kuliko dini yetu. ’Nilibaki hapo mpaka jua likazama wala sikwenda tena shambani.” [Taz: ‘Suwarun min hayaat swahaba’ uk108].

Mjadala baina ya Salmaan na baba yake

Salmaan anaendelea kusimulia: “Kisha nikawauliza (Wakrsto), ‘Dini yenu hii asili yake ni wapi?’ Wakasema: kutoka miji ya Sham. Basi ulipofika usiku nilirudi nyumbani baba akaniuliza lililojiri shambani (na kwa nini nimechelewa kurudi). Nikamjibu, ‘Ewe baba, kuna watu fulani niliwapitia (kwenye kanisa lao) nikawaona wanaabudu basi nikafurahishwa sana na ibada zao, na nilibaki hapo mpaka jua likazama. ’

“Baba akashtuka, akakasirika na kufazaika kwa taarifa zangu akaniambia, ‘Mwanangu, hakuna heri yoyote katika dini ile. Dini yako na wazee wako (Majusiyya) ni bora kuliko ile.’ Nikambishia na kumwambia, ‘Hapana, ile ndio dini nzuri na bora.’ Kuanzia hapo, baba yangu aliogopa mimi kubadilisha dini na akaamua kunifunga nyumbani kwa minyororo miguuni mwangu.”

Salmaan atoroka.

Salmaan alituma ujumbe kwa viongozi wa kanisa na kuwataka ukitokea msafara kuelekea Sham wamuhabarishe. Anasimulia: “Hazikupita siku nyingi, mara nikapata habari kwamba kuna jamaa wataondoka kuelekea Sham, nikajitahidi kuipapatua minyororo mpaka nikaiweza (kujifungua), nikasafiri pamoja nao mpaka tukafika miji ya Sham. Tulipofika nikawauliza, ‘Ni yupi mtu mwenye nafasi kubwa zaidi katika watu wa dini yenu?’Nikajibiwa: ‘Askofu ambaye ndie mlezi wa kanisa.’”

Salmaan akutana na Askofu.

Salmaan (Allah amridhie) anaendelea kusimulia: “Nikamfuata (askofu) na kumwambia, ‘Mimi nimeupenda Ukristo na ningependa kuwa nawe, nikutumikie na nijifunze kwako pamoja na kufanya ibada pamoja.’ Askofu akasema, ‘Karibu ingia tu.’”

Salmaan anazidi kusimulia.

“Sikukaa naye muda mrefu mara nikagundua kuwa ni mtu (kiongozi) muovu (tapeli), anawalazimisha wafuasi wake kutoa sadaka kwa ajili ya maskini pamoja na kuendeleza dini akiahidi watapata thawabu nyingi, lakini wakimpa (fedha hizo) anazificha wala hawapi mafakiri kama alivyodai mpaka akafanikiwa kuijaza mitungi saba ya dhahabu.” [Taz: ‘Suwarun min hayaat swahaba’ uk 109]

Salmaan hakufurahishwa na mwenendo wa kiongozi yule tapeli na anasema: “Nikamchukia sana kwa kile nilichokiona akiwafanyia wafuasi wake.” Lakini hazikupita siku nyingi mara Askofu akafariki.

Salmaan kufichua uovu wa Askofu.

Salmaan kwa ujasiri kabisa aliwatokea Wafuasi waliokuwa wamejikusanya kutaka kumzika kiongozi wao kwa mazishi ya heshima na kuwaambia: “Jamaa yenu huyu alikuwa mtu mbaya (mtu hiyana). Alikuamrisheni mtoe sadaka lakini alikuwa akijilimbikizia na wala hakuwa akiwapa masikini chochote.” Wakamuuliza: “Uliyajuaje hayo?” Akawaambia: “Nitakuonesheni mahala lilipo kasiki lake.” Aliwaonesha mahala lilipo, wakaitoa mitungi saba ikiwa imejaa dhahabu na fedha.Walipoiona mali ile, walihamaki wakasema: “Wallahi hatumziki. Wakamsulubu na kumpiga kwa mawe.”

Kanisa lateua askofu mwingine.

Salmaan anaendelea kuhadithia: “Baada ya muda mchache walimchagua kiongozi mwingine, nikakaa kwake kitambo. Nilimkuta kuwa mtu mwema (mwaminifu). Hakufanana na mtu yoyote kwa wingi wa ibada, ucha Mungu na kuipenda zaidi Akhera. Nikampenda sana. Askofu yule mpya alipofikiwa na ishara za umauti nilimwambia. ‘Ewe fulani, unaniusia niende kwa nani niwe naye baada yako?’

Askofu akasema, ‘Sikia kijana wangu; simtambui mtu aliye na imani uliyonayo wewe ila mtu mmoja tu katika mji wa Muuswil (ni mji wa zamani karibu na mto Dajla huko Iraq). Huyo ni mtu mkweli hajapotoka na wala hajabadisha mafunzo ya dini, jiunge naye.”

Salmaan kuelekea Muuswil.

Mtawa yule alipofariki, Salmaan aliondoka kama alivyousiwa na kufika Muuswil. (Alikutana na mwalimu, mwanadini aliyeagizwa kwake) akamsimulia habari yake yote. Yule mtu akamwambia Salmaan: “Kaa pamoja na mimi hapa.”Salmaan anasema: “Nikamkuta na kheri nyingi na hali nzuri ya kidini na ibada, lakini naye hazikupita siku nyingi akafikwa na umauti.” Ndipo alipomuomba amtajie mwanadini (msomi) mwengine amfuate hapo atakapokufa. Mwalimu alimwambia Salmaan: “Sikiliza mwanagu. Wallah hakuna sasa mtu aliye juu ya haki tuliyo nayo sisi ila namjua mtu mmoja tu ambaye anapatikana katika mji wa Nasiibiyn (maili sita kutoka Muuswil kuelekea Shaam)” [Taz: ‘Suwarun min hayat swahaba’ uk 111].

Salmaan aelekea Nasiibyn.

Mara tu baada ya kufariki mwalimu wake, Salmaan Alfaarisy (Allah awe radhi naye) alifuata wasia wa mwalimu wake na kuelekea Nasibyn ambako alikutana na mwalimu na mtu wa dini aliyeagizwa kwake. Kwa kweli alikuwa mtu mwema kama walivyokuwa wenzake wawili waliopita, ila hakukaa muda mrefu naye akafikiwa na umauti. Alipokaribia kufa alimuelekeza Salmaan kwamba katika mji wa Ammuuriya kuna mtu mwema ambaye ndiye pekee aliyebaki juu
ya mgongo wa ardhi, aende akaishi naye.

Salmaan amesema: “Baada ya kufariki dunia nilikwenda Ammuuriya, nikakutana na mtawa huyo. Nilimkuta kuwa ni mtu aliyeshika mwenendo sahihi wa waliotangulia, nikamsimulia habari yangu na kuishi naye kiasi cha kuishi. Nikiwa kwake nilijipatia ng’ombe kidogo na kondoo…

Itaendelea

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close