1. Habari1. TIF News

Mahujaji TIF 2018 Wako Tayari Kwa Safari

“labbayka Allaahumma Labbyka, Labbayka Laa Shariika Laka Labbayka, Innal-hamda
Wal-ni’mata laka wal-mulk, Laa Shariika Laka”

Nimekuitika Mola wangu nimekuitika, Nimekuitika huna Mshirika nimekuitika, Hakika Sifa zote njema na neema na ufalme ni vyako, huna mshirika.

Hivyo ndivyo watakavyokuwa wakitamka mahujaji wote wakiwemo sita wanaokwenda chini ya mwavuli wa The Islamic Foundation (TIF) kwa ufadhili wa taasisi ya The Zayed Bin Sultan Al Nahyan Charitable and Humanitarian Foundation ya Falme za Kiarabu(UAE).

Akiongea na Gazeti Imaan, kiongozi wa msafara huo wa mahujaji wanaume watano na mwanamke mmoja, Sheikh Muhammad Issa, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Taasisi za Answar Sunnah Tanzania (BASUTA), amesema maandalizi ya safari yamekamilika.

“Mahujaji wetu wanakwenda na taasisi ya kupeleka mahujaji ya Khidmat na Peace Travel Agency na tayari wameshapata chanjo, visa na tiketi za safari pamoja na mavazi ya kuvaa wakiwa Hijja yaani Ihraam na wameshahudhuria semina za maandalizi. Kilichobaki ni kuondoka tu kuelekea viwanja takatifu”, alisema.

Safari ya mahujaji hawa itaanza siku ya Jumamosi tarehe 12 Agosti 2018 uwanja wa ndege wa JNIA jijini Dar es Salaam kuelekea Cairo Misri na ndege ya Shirika la Ndege la Misri na kubadili ndege kutoka Cairo kuelekea Jeddah nchini Saudia Arabia ambapo wanatarajiwa kuwasili siku hiyo hiyo majira ya saa 12 jioni in Shaa Allah.

Akitoa nasaha zake kwa mahujaji hao watarajiwa, Mkurugenzi wa TIF, Sheikh Ibrahim Twaha alisema kuwa fursa ya Hijja ni jambo adhimu hivyo mahujaji wetu watumie fursa hiyo kuonesha shukrani yao kwa Allah na kutumia muda mwingi wakiwa huko katika ibada kwani hilo ndio lengo la kuacha miji na shughuli zao.

Kwa miaka kadhaa sasa TIF imekuwa ikipeleka mahujaji katika mradi wa taasisi hiyo kutoka Imarati wa kufadhili mahujaji kutoka nchi mbali mbali duniani ikiwemo Tanzania. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa TIF, Aref Nahdi, gharama za kusafirisha hujaji mmoja mwaka huu ni Tshs 10,488,000 ambapo kwa mahujaji saba wa TIF ni Tshs 73,416,000.

Akiwaasa mahujaji hao, Nahdi aliwataka wakawe mabalozi wa kuonesha mfano mzuri wakiwa huko. Pia aliwaombea: “Allah awafikishe salama wafanye ibada yao salama watuombee dua na sisi, Allah atusamehe madhambi yetu na ajaalie TIF iendelee kupeleka mahujaji kila mwaka.”

Mahujaji wa TIF na wenzao wanaokwenda na taasisi ya Khidma na Peace Travel Agency, wanatarajiwa kurejea Septemba 2 baada ya kuhiji na kutembelea mji wa Madina na maeneo mbali mbali ya kihistoria. Sheikh Hashim Rusanganya, mmoja wa masheikh anayeongoza mahujaji hao alitaja baadhi ya maeneo ya kihistoria watakayoyatembelea mjini Makka na Madina kuwa ni pamoja na nyumba aliyozaliwa Mtume Muhammad, (rehema za Allah na amani zimshukie), nyumbani kwa Bi Khadija bint Khuwaylid (Allah amridhie), pamoja na ilipokuwa nyumba ya Abu Jahal, adui mkubwa wa Uislamu.

Watakapokuwa Madina, licha ya kuzuru kaburi la Mtume na Makhalifa Abubakar na Umar (Allah awaridhie), mahujaji hao wanatarajiwa pia kuzuru makaburi ya Maswahaba Albaqii na Masjid Quba, Qiblatain, al-Ghamaamah, vilima vya Uhud na kwingineko.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close