1. Habari

Kongole serikali kwa kuvalia njuga maadili kazini

Kila ifikapo Desemba 10 ya kila mwaka, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa huadhimisha siku ya maadili na haki za binadamu, ikiwa ni utekelezaji wa tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948 linalozitaka serikali zote duniani kutambua haki za msingi za mwanadamu ikiwemo haki ya kuishi, kupata chakula na malazi.

Kwa hapa Tanzania siku hiyo ilianza kuadhimishwa mwaka jana 2017 kwa lengo la kutoa fursa kwa serikali kujitathmini kama imefanya juhudi za kutosha katika kupunguza vitendo vya rushwa, kuimarisha uwajibikaji kazini na misingi ya utawala bora kwa ujumla wake.

Katika maadhimisho ya mwaka huu yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alionya kuwa serikali haitamvumilia kiongozi yeyote wa umma atakayetanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma katika utendaji wake.

Majaliwa alisema mgongano wa maslahi umechangia rasilimali za nchi kunufaisha watu wachache isivyo halali huku wananchi wengi wakiendelea kuwa mafukara.

Aidha, Majaliwa alifafanua kuwa, baadhi ya madiwani na watumishi wa halmashauri wamekuwa wakishiriki kutoa maamuzi yanayohitimishwa kwa kumpatia kazi mkandarasi au mzabuni wakati kampuni husika inamilikiwa na mwenza, rafiki, ndugu wa karibu au mtoa rushwa.

Kwa wafuatiliaji wa mambo, si mara ya kwanza kusikia kauli kama hii. Wapo baadhi ya watumishi wanaofanya kazi za serikali kwa kutanguliza mbele manufaa na faida (maslahi) binafsi, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya utawala bora.

Kwa upande mwingine, kauli ya Waziri Mkuu Majaliwa inabeba uzito mkubwa kwa kuwa yeye ni kiongozi wa serikali kwa muda mrefu hivyo anatambua vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa serikali. Kwa lugha ya kihabari, tunasema hicho ni chanzo chenye mamlaka (authoritative source). Kwa minajili hiyo, bila shaka kauli ya Majaliwa ni ukweli mtupu. Hakika baadhi ya watumishi wa umma wamekuwa wakiangalia zaidi matumbo yao na kusahau kabisa kwamba, utumishi wao ni wa kuwatumikia Watanzania.

Mwenyezi Mungu anasema: “Wala msiliane mali zenu kwa baatili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.” [Qur’an 2: 188].

Kwa upande wetu sisi Gazeti Imaan, tunaipongeza serikali kwa kuvalia njuga suala la maadili ya utumishi kazini. Hakika hili ni jambo jema linalopaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo.

Ni imani yetu mkakati huo wa serikali utaleta mabadiliko ya kiutendaji ndani ya serikali. Serikali imeonesha juhudi zake kukabiliana na baadhi ya maovu yanayoathiri jamii, lakini vile vile ni muhimu kwa viongozi wa dini kuzungumzia jambo hili. Hii inatokana na ukweli kuwa viongozi wa dini ni watu wanaoheshimiwa na kuaminiwa sana na wanajamii wakiwemo viongozi.na watumishi wengine wa serikali.

Mgongano wa maslahi ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuisababishia hasara serikali kwa muda mrefu, ni lazima jambo hili lidhibitiwe. Na ili kukomesha kadhia hizi, ni vema zinapoibuka tuhuma dhidi ya viongozi wanaokiuka maadili ya kazi zitazamwe kwa uadilifu na kama kweli zipo viongozi hao wachukuliwe hatua stahiki.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close