1. Habari3. Kimatiafa

Kongole Dkt. Shein kwa kusaini sheria ya dawa za kulevya

Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein alitia saini kuidhinisha kuanza kutumika sheria mpya ya dawa za kulevya, ambayo inaiwezesha mahakama kumhukumu mtu aliyekutwa na dawa za kulevya kifungo cha maisha gerezani au kulipa faini ya Tsh. bilioni moja.

Kutiwa saini kwa sheria hiyo kulitangazwa na Mwanasheria wa Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Juma Abdulrahman Zidikheri, wakati akizumgumnza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na akasisitiza kuwa sheria hiyo imeshaanza kutumika rasmi.

Zidikheri alibainisha kuwa sheria hiyo ni endelevu na itawakumba hata wale wanaowezesha kuuzwa kwa dawa hizo haramu.

Kwa hakika huu ni uamuzi mzuri na unaopaswa kuungwa mkono na kila mmoja, kwani hakuna yeyote kati yetu asiyejua madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Kiuchumi, matumizi ya dawa za kulevya huongeza mzigo kwa taifa kwa kuwa hupunguza nguvu kazi na husababisha uharibifu wa mali.

Pia, gharama za udhibiti zikiwamo utoaji wa elimu kwa umma, uendeshaji wa kesi, kuwatunza wafungwa gerezani na kuwatibu watumiaji huongeza mzigo kwa taifa na jamii kwa ujumla. Fedha na nguvu kubwa inayotumika katika kampeni za udhibiti zingeweza kusaidia kufanya shughuli nyingine za maendeleo na ustawi wa nchi kwa ujumla.

Aidha, kwa upande mwingine, dawa za kulevya husababisha mfumuko wa bei unaotokana na fedha za biashara hiyo kuingizwa kwenye mfumo halali, hivyo kuwaongezea wananchi mzigo wa mfumuko unaojitokeza. Kijamii, dawa za kulevya zimeendelea kusababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Huchangia pia migogoro ya kifamilia katika jamii jambo linaloweza kuzisambaratisha kabisa. Wazazi ambao hutumia dawa za kulevya, huonesha mfano mbaya kwa watoto wao na jamii kwa ujumla.

Aidha, watumiaji wamekuwa wakijihusisha na tabia na vitendo viovu kama vile wizi, uporaji, biashara ya ngono na ubakaji. Jamii imekuwa ikiamini kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni jambo la kujitakia, ndiyo maana serikali na jamii imekuwa ikipambana kuelimisha umma juu ya athari za matumizi ya dawa hizo.

Kwa ujumla, athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa kwa jamii kuliko faida zake, ndiyo maana tunathubutu kumuunga mkono na kumpongeza Rais Shein kwa kusaini sheria hiyo, ambayo tunaamini itachochea watu wengi kujiepusha na vitendo vya uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya.

Kimsingi, Dkt. Shein ametekeleza wajibu wake, hivyo nasi tuna kila sababu ya kupiga vita biashara na utumiaji wa dawa za kulevya, kwa kuzingatia mafundisho ya Mtume Muhammad: “Mtu aliyeuona uovu, na auondoe kwa mkono wake, akishindwa, basi auziwie kwa ulimi wake, na kama akishindwa, basi na achukie moyoni mwake, na kuchukia kwa moyo ni imani dhaifu.” [Muslim].

Na kwa kuwa vita hii ni ngumu, tunaamini kuna wengi watakaounga mkono juhudi hizi, ili hatimaye Zanzibar ibaki swalama.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close