BAKARI HASSAN SALIM
WANANCHI wa mtaa wa Lukobe-Kambi Tano katika manispaa ya Morogoro wameishukuru taasisi ya The Islamic Foundation kwa kuwachimbia kisima kiefu cha maji katika mtaa wao.
Kisima hicho kimechimbwa nje ya uzio wa Masjid Imaan, msikiti ambao upo katika kata ya Lukobe ukimilikiwa na taasisi ya The Islamc Foundation.
Wakizungumza na Gazeti Imaan, wakiongozwa na Imam wa msikiti huo, sheikh Nuru Abdulrahman Mohamed, wananchi hao wamesema kuwa kisima hicho hakitoi huduma kwa Waislamu pekee wanaosali msikitini hapo bali Watanzania wote waishio eneo hilo, bila kujali imani zao.
Wakazi hao walisema wakati Waumini wanatumia maji hayo kwa ajili ya kuchukua wudhu kwa ajili sala, mamia ya wakazi wa eneo hilo nao watatumia maji hayo kwa matumizi ya majumbani kama kupikia, kuoga na kadhalika.
Imam Nuru, akifafanua umuhimu wa kisima hicho alisema maji ni mahitaji muhimu na ya kila siku ya mwanadamu na kwa mwenye kuyatoa kama sadaka anapata fadhila kubwa mbele ya Allah Mtukufu.
Imam huyo aliiomba taasisi ya The Islamic Foundation iendelee na moyo huo huo wa kusaidia huduma muhimu, ikiwemo maji kwa kusambaza visima vya maji.
Akimuunga mkono Imam huyo, mkazi mmoja, aliyejitambulisha kama bi Fatuma Mohammed alisema kwa kuchimba kisima hicho, taasisi ya The Islamic Foundation imeonesha mambo mawili: Kwanza inaunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita kwa vitendo na pili imeleta ukombozi wa wanawake kwa kuwaletea maji karibu yao.