Blog

Sheikh Doga, mfano halisi wa uanazuoni

Yussuf Masoud na Suleiman Magali

Hivi karibuni, Tanzania ilikumbwa na msiba mkubwa baada ya kumpoteza mwanazuoni wa fani ya sharia ya Kiislamu aliyefanya kazi ya kufundisha Uislamu na ulinganiaji maisha yake yote.

Sheikh Muharram Juma Doga alifariki jijini katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumanne Agosti 20, 2024 na kuzikwa kesho yake.

Sheikh Doga katika maisha yake kabla na baada ya kurudi masomoni nchini Saudi Arabia, hakufanya kazi yoyote nyingine isipokuwa kusomesha mpaka mauti yalipomfika.

Masheikh na Waumini mbalimbali waliozungumzia namna walivyomjua walisema katika kipindi chote cha uhai wake alisoma dini na kufundisha, na wanaamini aliifanya kazi hiyo kwa ikhlaswi, jitihada kubwa bila ya kuchoka hadi umauti ulipomfika. Masheikh na Waumini pia walimsifu kwa kuhimiza umoja na mshikamano kwa wanafunzi aliokuwa akiwasomesha na hata kwa wanazuoni wenziwe huku pia akichunga dhidi ya kuwafarakanisha Waumini.

Sheikh Bane ashuhudia uwajibikaji wake

Sheikh Suleiman Twaha Bane, rafiki wa karibu wa Sheikh Doga na mwalimu mwenzake, amesema marehemu alikuwa sheikh anayewajibika kwa kuingia darasani kufundisha.

“Sheikh Muharam alikuwa kweli mwanazuoni na alikuwa sheikh anawajibika jambo ambalo wengi wetu tunakosa. Mtu mwingine angekuwa na nusu ya tatizo alilonalo asingeweza kuingia darasani na kufundisha lakini yeye alikuwa anaingia darasani ili kufikisha kile ambacho Allah amempa,” alieleza.

Sheikh Bane alisema marehemu alikuwa ana elimu ya kutosha na alikuwa anaitoa bila ya majivuno na hachagui wa kumsomesha. Alisema kwa Sheikh Doga ilikuwa wanafunzi wote sawa bila ya kujali kipato cha mtu.

 “Namna bora ya kumuenzi sheikh ni kuendeleza darasa lake alilolianzisha kwani kituo hicho kipo na madarasa yapo. Huo ndio wasia wangu ikIwa nyinyi wanafunzi wa sheikh. Sheikh aliwathamini, akiwajali masheikh wenzake na nyinyi mnatakiwa muwe hivyo hivyo” aliongeza.

Mufti – alinufaisha wengi

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi bin Ali, aliwataka masheikh na wanazuoni kuindeleza na kuithamini kazi ya Sheikh Doga katika kufundisha.

Alisema Sheikh Doga alijulikana Tanzania na Afrika Mashariki kwa kazi yake ya da’awah ambayo watu wengi walinufaika kwayo katika uhai wake.

Naye Sheikh Omari Issa akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake ambao wamepata bahati ya kusoma kwa marehemu, alisema, Sheikh Doga siku zote alikuwa anasisitiza umoja na wanafunzi wasiwe na makundi,

“Kwa kweli sheikh maisha yake yalikuwa ya kutujenga. Kwanza alikuwa anasisitiza umoja na alikuwa akifundisha anazionesha sababu zinazopelekea watu kutokuwa wamoja.”

Sheikh Issa alisema marehemu Sheikh Doga alipenda kuweka vitabu mbalimbali darasani ili watu wavisome wasiwe na makundi na ili wakishajua watoke kwenye makundi na kwenda kusimamia kitu ambacho kipo sahihi.

Sheikh Walid: Kigogo kaondoka

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad Omar Kawambwa ambaye alisema anamjua Sheikh Doga siku nyingi alimtaja kama mtu aliyetumia muda wake kuitumikia dini na kwamba ni muhimu wanazuoni kuiga vitendo vyake kwa kuendeleza aliyokuwa akiyafanya ikiwemo kufungua darsa nyingi na kusomesha watu.

 “Nyumba ya mwanachuoni ni ile ambayo watu wanapishana na vitabu sio ‘brifcase’ za dhahabu. Mahitaji ya elimu ya dini kwa sasa ni makubwa na vigogo ndio hao wanaondoka,” alisema Sheikh Doga.

Sheikh Walid alisema ni wakati wa kila mmoja miongoni mwa wanazuoni waliofurika katika msiba huo ambaye anafahamu kitu kidogo kusomesha bila kujali tofauti zao za kielimu – wanaojua sana au kidogo.

Dkt Tego – Sheikh alikuwa jirani mzuri

Naye, Dkt Abdallah Tego, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, ambaye ni jirani wa Sheikh Muharam Juma Doga amesema amemfahamu Sheikh huyo na Kaka yake Muhsin toka mwaka 1989 walipohamia rasmi Temeke.

Dkt Tego alisema Sheikh Doga ni kiongozi ambaye aliyependa ushirikiano na majirani zake, na alikuwa mstari wa mbele kusaidia shughuli za kijamii hasa zile zinazohitaji elimu ya dini.

Miongoni mwa mambo ambayo mhadhiri huyo anamkumbuka kwayo Sheikh Doga ni kushirikiana na majirani zake katika mazishi ikiwemo kuongoza swala za jeneza kwa marhumu mbalimbali waliokuwa mtaani kwake. Dkt Tego pia alisema Sheikh Doga hakupenda migogoro na hakumbuki ni siku gani Sheikh aligombana na majirani zake.

Akihadithia zaidi kuhusu Sheikh Doga, mtaalamu huyo wa huduma za kifedha za Kiislamu, alisema amekuwa anamuona Sheikh Doga tangu amfahamu akifundisha dini siku nzima.

“Wanafunzi walikuwa wanapishana, wako wa asubuhi wanafundishwa wanaondoka, wapo wa mchana watafundisha na kuondoka na watakuja wa jioni watafundishwa na kuondoka. Licha ya ukweli kuwa tembea yake ilikuwa ya shida, alijitahidi kwenda Alharamain kufundisha hivyohivyo,” alisema Dkt Tego.

Sheikh Juma Pori- Sheikh Doga rafiki, muasisi

Kwa upande wake Sheikh Juma Pori amesema Sheikh Muharam Juma Doga alikuwa ni rafiki wa masheikh wenzake na muasisi wa mambo mengi yanayosaidia kusukuma gurudumu la Uislamu hapa nchini.

Sheikh Pori alisema Sheikh Doga ana mchango mkubwa sana katika kuanzishwa kwa kituo cha Al-Haramanin, akiwa ni mmoja kati ya watu wanne waliosababisha kupatikana kwa majengo hayo pale walipokwenda kwa Mufti wa Saudi Arabia wa wakati huo Abdul-Aziz ibn Abdullah ibn Baz na kumuomba kujengwa kituo hicho, yeye akiwa kama mfasiri. Aidha, Sheikh Doga anatajwa kuwa mmoja wa waasisi wa kitengo cha dini katika chuo hicho cha Al-Haramain.

Kadhalika, Sheikh Doga ni katika waasisi wa Baraza la Sunna Tanzania (BASUTA), na aliteuliwa kuwa Amir wa mwanzo lakini alikataa kuwa kiongozi kutokana na ukweli kuwa yeye hakupenda madaraka.

Sheikh Doga pia alishiriki kuasisi taasisi ya Al-kheiry ambayo Katibu wake Mkuu ni Ahmadi Urari na ni katika waasisi wa Jumuiya ya Wanazuoni Tanzania (Hay-atul Ulamaa) ambayo sasa inaongozwa na Sheikh Abdallah Ndauga.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button