Matukio

Wahadhiri Misk ya Roho waahidi makubwa

Wahadhiri watakasowasilisha mada katika kongamano la Misk ya Roho litalofanyika Oktoba 28 mwaka huu, wameahidi, Insha Allah, kutoa ujumbe mzito utakaobadili fikra za watu wengi, na kuboresha ufahamu wao juu ya Utukufu wa Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya masheikh hao walioongea na Gazeti Imaan wamewataka Waislamu kujitahidi kutokosa kuhudhuria kongamano ambalo linawakutanisha Watanzania na wahadhiri na masheikh wa ndani na nje ya nchi, wenye mbinu mbalimbali za ufikishaji katika medani ya da’awah.

Mmoja wa masheikh waliozungumza na Gazeti Imaan ni Sheikh Dourmohammed Issa kutoka mkoani Mbeya ambapo amesema amejiandaa vema kufikisha katika elimu aliyojaliwa na Allah Aliyetukuka ili kukonga nyoyo za Waumini. “Hili si kongamano la kukosa,” alisema Sheikh Dourmohammed kupitia simu alipowasiliana na mwandishi wetu. Sheikh Issa alisema kuwa anachotamani katika nafsi yake ni kuona mada yake inafanikiwa kuleta mabadiliko kwa watakaodhuria hadi watosheke.

Sheikh Dour mohammed aliongeza: “Tutajitahidi kadiri tuwezavyo ili kile ambacho Waislamu walikuwa na hamu nacho waweze kukipata. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki na uwezo wa kuwasilisha mada tulizopangiwa.”

Aidha, Sheikh Issa alitoa wito kwa Waislamu wengi kujitokeza siku hiyo ili waweze kupata ujumbe wa dini yao na kuweza kutenda kulingana na mafundisho ya Uislamu. Sanjari na hivyo, Sheikh Dourmohammed aliwataka Waislamu wawe watulivu siku hiyo ya kongamano ili iwe rahisi kuzingatia kile kinachozungumzwa.

Naye Sheikh Ally Jumanne amesema kuwa amejiandaa vya kutosha na anaamini kupitia kongamano hilo umma utawaidhika na kuvuna mambo mengi ya kheri. Sheikh Ally alitanabaisha kuwa, wahadhiri wameandaa khutba za kipekee kwa sababu wanajua uzito wa kongamano na kwa maana hiyo hakuna shaka watakuja na mambo yenye kuleta tija katika jamii.

“Uislamu marejeo yake ni ule ukongwe wake. Kilekile cha zamani mtu anaweza kukileta katika sura nzuri zaidi. Lakini mbinu za ufundishaji ndizo huwa zinabadilika badilika, kwa hivyo ‘Insha Allah’ nadhani hayo yatakuwapo kwangu mimi na kwa Masheikh wengine,” alisema Sheikh Ally.

Kwa upande wake, Sheikh Abdulrahman Mhina (Baba Kiruwasha) ambaye amebobea katika masuala ya ndoa katika Uislamu, amebainisha kuwa siku hiyo Waislamu wategemee mambo mapya na yenye ujumbe yakinifu.

Kuna mambo mengi mapya katika masikio ya watu yatakayokuwepo siku hiyo lakini sio mapya katika dini, kwa hiyo watu waje kwani kuna mambo ambayo tayari wameshayasikia na kuna mengine huenda hawajayasikia,” alimaliza kusema Baba Kiruwasha.

Baba Kiruwasha ambaye kwa muda mrefu amekuwa akifanya kipindi cha malezi ya ndoa katika Redio Imaan anabainisha kuwa hatapenda kuona wahudhuriaji wanalalamika kuwa kiu yao haijatimizwa. Ukiacha masheikh hao wa Tanzania, kongamano hili pia litahusisha masheikh kutoka nchi za Afrika ya Mashariki wakiwemo Sheikh Yusuf Abdi na Sheikh Jamaldin Osman kutoka Kenya, Sheikh Zuberi Bizimana (Burundi), Sheikh Ally Kajura (Rwanda) na Sheikh Muhammad Abduweli (Uganda).

Wageni wengine
Ukiacha masheikh hao watakaowasilisha mada katika kongamano, wageni kadhaa maarufu wanatarajiwa kuhudhuria wakiwemo Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, Mufti wa Zanzibar Sheikh Omar al – Kaabi na Rais wa taasisi ya Al – Hikma, Sheikh AbdulQadir al – Ahdal.

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close