Matukio

Uongo unavyotumika kuangamiza Waislamu

Duniani kuna dhana mbili zinazokinzana, kuna uongo na kweli. Ukweli ni haki itokayo kwa Mungu Muumba, na batili ni uongo unaosimamiwa na Shetani [Iblis] aliyelaaniwa, pamoja na washirika wake wa kijini na kibinadamu. Kwa hiyo, siku zote duniani kuna mvutano na mapambano makali baina ya ukweli na uongo. Lini yatakoma? Sijui!

Yote kwa yote, daima ukweli utabaki kuwa na nguvu kwa sababu umo ndani ya haki, na uongo ni dhaifu kwa kuwa umejificha ndani ya batili. Aghalabu haki inapotaka kuongoza dunia batili huchomoza haraka kuizuia haki isitimize wajibu wake.

Sijafahamu kwa nini hali hii hutokea, labda kila moja ina silika yake ya kujichomoza. Mashambulizi yanayoendelea kutekelezwa na majeshi ya Wazayuni dhidi ya Waislamu wanyonge wa Palestina yanathibitisha ni kwa kiasi gani batili inavyoendelea kushika kasi ulimwenguni. Mifano ya nchi za Waislamu kama Palestina, wanaokabiliwa na hujuma za mara kwa mara za mashambulizi na mauaji ni mingi, dunia nzima.

Kwa miongo mingi, Marekani kwa kushirikiana na nchi nyingine za Magharibi ikiwamo Uingereza imekuwa ikiongoza harakati za mapambano dhidi ya mataifa ya Waislamu kama vile Syria, Iraq na Yemen kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi.

Isitoshe Marekani hutumia njia za mashambulizi ya kikatili na mauaji ya watu wasio na hatia ambazo pia hutumiwa na magaidi kama nyenzo ya kuweka shinikizo kwa dola ambazo hazikubaliani na matakwa yao kwa lengo la kufikia maslahi maalum ya magaidi, huku makundi ya kigaidi yakitumia njia rahisi na nyepesi kutishia hali ya amani na utulivu wa mataifa husika.

Na miongoni mwa mambo yanayoleta mkanganyiko katika kuliondosha tatizo la ugaidi, ni pale mataifa ya magharibi yanapofanya juhudi zinazodhihirisha chuki yao dhidi ya dini tukufu ya Uislamu na Waislamu, jambo linalochochea ukuaji wa harakati za ugaidi duniani.

Marekani inayodai kuwa inapambana na ugaidi na magaidi, imeugeuza uongo na kuuweka katika sura na umbile la haki. Jambo hili limeshika hatamu katika zama hizi ambazo ni vigumu mtu kutofautisha uongo na kweli hasa katika mambo yanayohusiana na haki za binadamu.

Lakini kimsingi, hilo siyo jambo la kushangaza kwa sababu siku zote madhalimu wanauogopa ukweli kama wanavyokiogopa na kukichukia kifo, na ndiyo maana wanauficha ukweli ili jamii isiwaone kuwa wao ni wanyonyaji na wababaishaji. Uongo umewafanya waishi kwa tabu na wasiwasi kwa kuelewa kuwa siku moja ukweli utawaumbua. Wanachoogopea zaidi, ni siku dunia itakapowatambua kuwa wao ni waongo na wazushi. Kwa kulijua hilo, madhalimu usiku na mchana wamekuwa wakitumia muda mwingi, nguvu, fedha pamoja na hazina ya akili kuuzima uongo ili dhuluma na uzushi wao vichukue nafasi ya haki na ukweli.

Wanachanganya kweli na uongo Allah Mtukufu anasema ndani ya Qur’an: “Wala msichanganye kweli na uongo na mkaificha kweli hali ya kuwa mnajua.” [Qur’an, 2:42]. Allah akasema tena: “Sema: Hakika Mola wangu Mlezi hutoa haki, Mjuzi mno wa ghaibu. Sema: Haki imefika, na batili haijitokezi, wala hairudi.” [Qur’an, 34:48].

Funzo mojawapo tunalolipata katika Aya hizi ni kuwa, haki ni yenye kuishinda batili na kwamba uongo hauna uwezo wa kukabiliana na haki. Ukweli hauhitaji nguvu, propaganda au mashinikizo ili ugande kwenye fikra za watu. Kinyume chake, uongo unahitaji fedha, wapambe na kutumia nguvu na mashinikizo ili angalau uweze kukubalika. Na siku zote uongo unapopambanishwa na haki hugwaya na kutetema kana kwamba umemwagiwa maji ya baridi.

Katika kile inachodai kuwa ni mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi, Marekani na Uingereza zimekuwa zikifanya uvamizi wa kijeshi katika mataifa yenye Waislamu wengi kwa sababu tu, vikundi vingi vinavyojihusisha na maovu hayo vimejikita katika nchi hizo. Katika kufanikisha azma hiyo, nchi hizo zimekuwa mstari wa mbele kupigia debe suala zima la uhuru na haki za binadamu zikijaribu kuuonesha ulimwengu kwamba zinalinda na kutetea ‘haki’ za watu wanyonge na wachache.

Vita ya Iraq, Afghanistan na Libya ni baadhi tu ya yale yanayoshuhudiwa katika mataifa haya makubwa kuzivamia kijeshi nchi za Waislamu kwa dhana ya udanganyifu ya kuwakomboa raia wa nchi hizo dhidi ya kile wanachokiita sheria za dhuluma zinazowanyima ‘uhuru na demokrasia.’

Show More

Related Articles

Back to top button
Close