1. TIF NewsMatukio

Umuhimu wa kuhudhuria kongamano la Misk ya Roho

Misk ya Roho ni Kongamano kubwa la kida’awah kuwahi kufanyika katika historia ya Tanzania.
Ni Watanzania au wana Afrika Mashariki wa kawaida wachache sana wanaoweza kumudu kusafiri nchi mbalimbali za eneo hili kuhudhuria mihadhara na makongamano ili kustafidi na kupata ladha tofauti za masheikh wa nchi hizo. Hii ni kwa sababu za uchache wa kipato na muda.

Hata hivyo, Kongamano la Misk ya Roho limebadilisha hali hii. Kupitia kongamano hilo,tunaweza kuwapata masheikh wengi kutoka nchi zote hizo katika jukwaa moja. Hii ni fursa adhimu sana.

Kuna sababu nyingi na umuhimu mkubwa wa kuhudhuria mihadhara, warsha na makongamano mbalimbali ya Kiislamu ambayo huchangia kuchagiza mwamko wa umma wa Kiislamu hasa katika zama hizi ambapo jamii imekumbwa na baa la ujahili. Kongamano la Misk ya Roho ni moja ya makongamano hayo.

Waumini wakisiliza kwa makini

Misk ya Roho ni Kongamano kubwa la Kida’awah kuwahi kufanyika katika historia ya Tanzania. Wapo wanaoamini kuwa ni kongamano kubwa la Kiislamu kuliko yote kiathari, hususan kwa sababu linarushwa mubashara katika vyombo vya habari eneo zima la Afrika ya Mashariki. Mwaka jana lilipofanyika kwa mara ya kwanza, kongamano hili lilihudhuriwa na maelfu ya watu ambao wengi wao walitumia fursa hiyo kujenga mahusiano ya kindugu, kidini, kibiashara nk.

Madhumuni makuu ya kongamano hili ni kulingania, lakini ulinganiaji huo pia unaweza kuwa nyenzo ya kuchochea faida nyingine kama kujuana, kujenga urafiki na kukutanisha watu waliopoteana kwa muda mrefu.

Kongamano hili pia ni uwanja wa kujenga undugu wa kiimani, kama ambavyo mmoja wa masheikh waliohudhuria kongamano la kwanza la Misk ya Roho, alivyosema: “Mimi naheshimiwa sana huko kwetu lakini sikuwahi kuwa na muamala na baadhi ya masheikh wa nchi nyingine.”

Hii maana yake ni kuwa, Misk ya Roho ilimpatia sheikh yule fursa ya kukaa na wenzake na kubadilishana fikra na kutanua mawanda yake ya kutoa da’awah katika nchi nyingine.

Kongamano la Misk ya Roho pia kwa upande mwingine linaweza kuwa kama mkutano mkuu wa Waislamu wa Afrika Mashariki unaowaleta pamoja waumini na viongozi wao ili kujadili mambo mbalimbali yanayoikumba jamii yetu kwa ujumla.

Mijadala hiyo kama itatiliwa maanani na Waislamu kwa kiasi kikubwa huweza kuleta mabadiliko chanya katika ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Tunapoangazia umuhimu wa kongamano hili, ni vyema pia kuyatupia macho manufaa yapatikanayo katika mada zinazowasilishwa ambazo kwa kiasi kikubwa zinaigusa jamii moja kwa moja na zinalenga kujenga mustakabali mwema.

Mfano rejea ni mada zilizosheheni katika kongamano la kwanza la Misk ya Roho la mwaka 2017 ikiwemo jinsi ya kuwa na Ikhlas, umuhimu wa elimu na thamani ya amani.

Kwa upande wa wafanyabiashara halali wa Kiislamu ambao kwa kipindi kirefu wamekosa sehemu ya kutangaza biashara zao kwenye vyombo vinavyowafikia moja kwa moja wanajamii, kongamano hili ni fursa ya dhahabu kwao. Wafanyabiashara waje waungane The Islamic Foundation (TIF) katika kufanikisha maandalizi ya kongamano hili.

Kongamano la Misk ya Roho pia ni sehemu mbadala ya vijana kustarehe na kufurahi katika namna ambayo Allah anaipenda na kuiridhia, tofauti na ilivyozoeleka ambapo vijana wamekuwa wanapenda kwenda maeneo batili na potofu.

Familia nazo zinaweza kutumia kongamano la Misk ya Roho kama siku maalumu ya kutoka kwa pamoja (outing) katika kujenga mahusiano mazuri kwa familia zetu na kuwazoesha wanafamilia kuhudhuria vikao vyema.

Ni kheri iliyoje kuwa mmoja ya waliohudhuria au waliodhamini kikao ambacho ndani yake anatajwa Allah na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimfikie). Bila shaka, hakuna kati yetu anatamani kukosa kheri zake mwaka huu. Hivyo basi, tuazimie sasa kuwa wadau wa kwanza wa kongamano hili na mengine mengi yanayoandaliwa kwa ajili yetu na taasisi ya The Islamic Foundation (TIF).

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close