Matukio

Si Kongamano la kukosa, Misk ya roho 2018

Wakati wananchi wengi wakionesha hamu, shauku na matarajio makubwa ya kufukizwa na Misk ya Roho Jumapili hii Oktoba 28, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Mkurugenzi wa Makongamano wa The Islamic Foundation (TIF), TajMohammed Abbas ametaja baadhi ya mada zitakazowasilishwa katika kongamano hilo.

Miongoni mwa mada hizo ni pamoja na kumpenda Allah, ukubwa wa Allah, kanuni za Allah katika maisha yetu, furaha ya kweli inatokana na Allah, jinsi gani ya kupandikiza upendo wa Allah kwa watoto, mpende Allah, wapende binadamu nk.

TajMohammed alisema: “Hili litakuwa kongamano lingine la aina yake ambapo mada kubwa ni “…Utukufu Wake” Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.Tunaamini baada ya kongamano hili, ufahamu wa watu juu ya sifa, majina na upendo wa Allah utapanda zaidi.”

Mada hizo zimetajwa katika wakati ambapo, Gazeti Imaan limenasa kauli za Waislamu na wasio Waislamu nchini wakielezea matarajio yao makubwa kwa kongamano hilo maarufu lililojizolea umaarufu mkubwa, ikiwa hii ni mara yake ya pili kufanyika.

Katika mahojiano na gazeti hili, wengi wamesema kwa uzoefu waliopata kutokana na Kongamano la kwanza la Misk ya Roho lililofanyika Novemba 26 mwaka jana, wanaamini kongamano la pili, linaweza kuwa bora zaidi. Mmoja wa waliozungumza na gazeti hili, Mussa Mchange ambaye alikuwa katika foleni ya kununua tiketi yake, alisema anaamini kongamano hilo huwenda litambadilisha mitazamo yake, kama ambavyo kongamano la mwaka jana lilivyombadilisha.

Mchange alisema, kongamno lililopita lilimsaidia sana kumbadili fikra zake hususan juu ya masuala ya ugaidi na kuchupa mipaka katika Uislamu, hususan kupitia mada ya Sheikh Nurdin Kishki kuhusu ubaya wa kumwagadamu.

Kiukweli, mada ile ilinisaidia sana kuelewa ubaya wa makundi hayo ya kigaidi,” Mchange alisema.

Kwenye mada anayoizungumzia Mchange, Sheikh Nurdin Kishiki alisema: “Dini yetu tukufu ya Uislamu ni dini ya amani na utulivu, ni dini inayopinga aina zote za umwagaji damu, ni dini inayopinga dhuluma za aina zote, ni dini inayopinga unyanyasaji wa aina zote.” Hata hivyo, Mchange alisema, anaamini taasisi waandaaji The Islamic Foundation (TIF), imekuwa fursa ya kushughulikia mapungufu machache yaliyotokea kongamano lililopita ili safari hii mambo yawe bora zaidi.

Naye, Leyla Ashraf anabainisha kuwa jambo kubwa ambalo anatarajia kujifunza ni mbinu za ulinganiaji. “Kwangu hili ni jambo gumu kutokana na kutofahamu misingi ya kazi hiyo, lakini kupitia kongamano la mwaka jana nilijifunza mawili matatu, na nategemea kujifunza zaidi mwaka huu.” Alisema, uzuri wa masheikh kutoka nchi tofauti, kila mmoja anakuja na mtindo wake wa uwasilishaji, jambo ambalo kama walinganiaji watazingatia wanaweza kuboresha uwasilishaji wao.”

Katika matarajio ya wengi pia ni kuwepo tena kwa mada ya ndoa mwaka huu, baada ya mwaka jana Sheikh Juma Amir kukonga nyoyo za wengi. Miongoni mwa walioonesha hamu ya kusikia mada hiyo ni Jamal Hussein, ambaye alikiri kuwa mambo ya mahusiano ya ndoa, familia na malezi ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili Waislamu kwa sasa.

Katika kongamano la mwaka jana, Sheikh Juma Amir alisema mambo ya ndoa ni katika mambo magumu yanayoleta matatizo katika jamii kwa sababu watu wamepuuza elimu hiyo, kiasi kwamba hata aliyeoa hajui kwa nini kaoa na aliyeolewa hajui kwa nini kaolewa.

Katika kulisifu kongamano hili, dada mmoja, Mariam Sadiki amesema Misk ya Roho ni kitu muhimu kwake kwani humfunza mambo mengi. “Napenda Misk ya Roho kwani hunikutanisha na masheikh mbalimbali tena wengine kutoka nje ya nchi yetu, jambo ambalo linatupa fursa ya kujifunza kutoka kwa masheikh wa nje pia,” anasema Mariam. Mariam anasisitiza kuwa ni vizuri Waislamu wakajitahidi kufuatilia masheikh wanaozungumza kupitia kongamano la Misk ya Roho kwani hutoa ujumbe muhimu katika dini yao.

Razaq Saleh yeye anatoa wito kwa Waislamu kuyatekeleza yale yanayozungumzwa na wahadhiri kwenye kongamano la Misk ya Roho ili waweze kuusukuma mbele Uislamu. Pia Saleh alisema ni muhimu Waislamu wasiishie tu kusikiliza mawaidha mazuri yatakayotolewa bali waende mbele zaidi katika kuweka katika matendo.

Niwasihi Waislamu wenzangu tuhudhurie Kongamano la Misk ya Roho kwani humo kunafaida kubwa sana kwetu, bila kujifunza Uislamu wetu hatuwezi kufanikiwa,” anatoa wito Saleh. Kongamano la Misk ya Roho ni miongoni mwa makongamano ya kida’awa ya Afrika Mashariki yanayoandaliwa na taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) yenye lengo la kuendeleza Uislamu kwa kukuza ufahamu wa masuala ya dini.

Kurushwa mubashara
Waislamu na wasio Waislamu ambao watashindwa kuhudhuria kongamano la Misk ya Roho II hawana sababu ya kulalamika sana kwani taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) imeandaa mikakati madhubuti na kuhakikisha wanawezeshwa kuona au kusikia kila kitu, mwanzo mpaka mwisho wakiwa majumbani mwao!

Ni kwamba, Gazeti Imaan limeambiwa kuwa kongamano la Misk ya Roho II, linatarajiwa kurushwa mubashara, In shaa Allah, kupitia vyombo vya habari vya Imaan na washirika wengine wa media. Mkurugenzi wa vyombo vya habari vya Imaani, Ahmed Bawazir, amesema haiwezekani kwa Waislamu wote kukusanyika kwa wakati mmoja katika ukumbi wa Diamond Jubilee kwa pamoja, ndio maana wameamua kurushwa mubashara tukio hilo.

Lengo la kongamano ni watu kupata ujumbe bila kujali mtu yuko wapi, ndio maana tunarusha mubashara,” alisema Bawazir na kuongeza: “Ukumbi wa Diamond Jubilee hautoshi watu wote, hivyo tunataka aliyeko Kigoma, Sumbawanga, Pemba na kwengineko apate ujumbe wa dini yake.”

Kongamano la pili la Misk ya Roho linatarajia kufanyika Octoba 28, mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 11 jioni. Aidha litaambatana na nasheed pamoja na huduma ya chakula na vinywaji.

Wahadhiri watakaopamba kongamano hilo ni Sheikh Dourmohamed Issa kutoka Tanzania, Sheikh Ally Jumanne kutoka Tanzania, Sheikh Abdulrahman Mhina (Baba Kiruwasha) kutoka Tanzania. Wengine ni Sheikh Yusuf Abdi kutoka Kenya, Sheikh Jamaldin Osman kutoka Kenya, Sheikh Zuberi Bizimana kutoka Burundi, Sheikh Ally Kajura kutoka Rwanda na Sheikh Muhammad Abduweli kutoka Uganda.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close