Matukio

Shura ya Maimamu yajadili ukombozi wa kiuchumi, kielimu kwa Waislamu

Kutetereka kwa hali za Waislamu kiuchumi na kielimu tangu nchi ipate uhuru miaka ya 1960 kumewalazimu viongozi wa Shura ya Maimamu hapa nchini kuandaa mikakati itakayosaidia kuwakwamua Waislamu katika hali hizo.

Shura ya Maimamu iliyoketi Jumapili hii katika mkutano wa Maimamu wa Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Machinga Complex jijini humo ilipokea ripoti za kamati zake ambazo zilisheni maelezo na ufafanuzi wa maeneo ambayo Waislamu wamekwama na mikakati ya kujiondoa katika changamoto hizo.

Ripoti ya Kamati ya Mipango, Uchumi na Fedha iliyowasilishwa na Katibu wake Imamu Mbaraka Majura imeonesha kuwa Waislamu wenyewe wana uwezo wa kujikwamua kiuchumi na kimaendeleo. Majura aIisema kuwa jambo lililo muhimu ni kwa Waislamu hao kupatiwa elimu itakayowaonesha umuhimu wa kuchangia maendeleo ya Waislamu na Uislamu hapa nchini.

“Tumeona ni muhimu tutoe elimu kwa Waumini (juu ya umuhimu wa kuchangia maendeleo ya Uislamu) ndani na nje ya misikiti. Mfumo huu ukiweza kueleweka na kukubalika unaweza kuwa chachu ya mafanikio ya njia ya mapato,” alisema Imamu Majura.

Pia Imamu Majura alisema kuwa, wamedhamiria kuwa na miradi mbalimbali itakayosaidia kuleta mapato ya uhakika katika kuendesha masuala ya Waislamu.

Shura ya Maimamu katika kuhakikisha tunakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato katika kusukuma mbele maendeleo ya Waislamu tumedhamiria kutafuta ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji,” alisema Imamu Majura.

Aidha, kamati hiyo imesema kuwa ili kustawisha mipango ya Shura ya Maimamu, kwa sasa watahakikisha wanawatumia wataalumu wa fani mbalimbali miongoni mwa Waislamu.

Mambo mengi ya Kiislamu yamekuwa yakiendeshwa bila utaalamu wowote. Unakuta wasimamizi wa masuala ya fedha hawana taaluma hiyo. Sisi tumeamua kuhakikisha masuala yetu yanasimamiwa na watu waliosomea fani husika,” alisema Imamu Majura.

Majura aliongeza kuwa, watahakikisha wanaweka utaratibu wa kuwatambua Waislamu wenye fani mbalimbali ili waweze kutoa utaalamu wao katika miradi itakayoanzishwa. Zaidi alisema kuwa, wamepanga mikakati ya kuwanoa vijana wa Kiislamu ili kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

“Shura imedhamiria kuanzisha program ya vijana ambayo itazal isha vijana wenye fani mbalimbali ili kujenga nguvu kazi ya maendeleo,” alisema Majura.

Kwa upande mwingine, Imamu Majura alisema wamedhamiria kuhakikisha wanawashawishi Waislamu waanze kujitolea mali za Waqf.

“Shura inadhamira ya kufanya ushawishi miongoni mwa Waislamu waanze kujitolewa mali za Waqf ili kusaidia maendeleo yao,” anasema Imamu Majura.

Hata hivyo imamu Majura alikiri kuwa baadhi ya Waislamu huko nyuma walitoa mali nyingi za Waqf kwa baadhi ya taasisi za Kiislamu lakini hazikutumika kiuadilifu na kufujwa na hivyo kushindwa kuwasaidia Waislamu.

Kuhusu miradi yao ya sasa ya maduka, visima vya maji, mifuko ya kusaidiana, Majura alisema wanaifanyia utafiti ili kuhakikisha inastawi zaidi na kuleta manufaa kwa walengwa.


Elimu na Waislamu
Naye Mwalimu Dadi Rajab ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya elimu na Da’awa ya Shura hiyo ya Maimamu amesema kuwa wana mkakati wa kufanya utafiti kubaini jinsi ya kuimarisha elimu miongoni mwa Waislamu.

Rajab ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Kiislamu ya Mivumoni alisema Shura imejipanga kuamsha fikra za Waislamu katika masuala ya elimu ikiwemo kuifanya misikiti kuwa chachu ya elimu kwa Waislamu.

Suala la Uongozi na Uislamu
Katibu wa Shura ya Maimamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, amewataka Waislamu wawe na ari ya kujifunza masuala ya uongozi na kushiriki katika uchaguzi wa nyadhifa mbalimbali za uongozi wa nchi kulingana na utaratibu na sheria zilizowekwa.

Sheikh Ponda alisema kuwa Waislamu wengi wamekuwa nyuma katika kugombea nyadhifa za uongozi wa nchi, huku baadhi wakidai kuwa suala hilo halipo katika dini. Kwanini mkwamo mpaka sasa?

Historia inaonesha kuwa Waislamu hapa nchini walianza harakati za kujikwamua kimaendeleo mwanzoni kabisa wakati nchi inapata uhuru miaka ya 1960. Moja ya taasisi ambayo inatajwa kuwa mfano wa kuigwa ilikuwa ni Jumuiya ya Ustawi wa Waislamu ya Afrika Mashariki (EAMWS) ilianza kuwekeza kwenye elimu, ikiwemo mipango ya kujenga chuo kikuu.

Hata hivyo tangu kipindi hicho, hali za Waislamu bado zinatajwa kuwa bado ni hafifu ukilinganisha na jamii zingine. Musa Rajab anasema uduni huo wa maendeleo umetokana na kukosekana kwa dhamira ya dhati ya baadhi ya viongozi wa Kiislamu waliopewa madaraka ya kusimamia maendeleo ya Waislamu. Nae, Ismail Issa anasema Waislamu wamekuwa wakipitia hangamoto nyingi baadhi zikiwemo ndani ya Waislamu wenyewe, zingine kutoka nje, hata hivyo bado anaamini kama Waislamu wakisimama imara wataweza kuinuka kiuchumi na kielimu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close