Matukio

Sheikh Abdi: Elimu zote mbili zinamuezesha mtu kumfahamu Allah

Sheikh Yusuf Abdi kutoka nchini Kenya amewataka Waislamu kusoma elimu ya dini na ya mazingira akisema kuwa elimu zote hizo zinamuwezesha mwanadamu kumfahamu Mwenyezi Mungu juu ya uwezo na nguvu zake.

Mhadhiri huyo kutoka Kenya aliyasema hayo katika kongamano la pili la Misk ya Roho lililofanyika Oktoba 28 mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam ambapo alisema si masomo ya dini pekee ndiyo humfanya Muislamu amfahamu Mola wake.

Waislamu tunahitajika tusome, tena tusome sio vile tunavyofikiria sisi, kwamba unapotaka kumjua Mwenyezi Mungu basi usome masomo tunayoyaita ya dini, bali kulingana na niliyoyasikiliza leo, nimeona ya kwamba Waislamu tunafaa tusome sayansi, tunafaa tusome agriculture[kilimo],” alisema Sheikh Abdi na kuongeza,
Yote haya yanatupeleka sisi kumjua Allah, na kama huniamini soma aya ya kwanza aliyoteremshia Mtume wetu Muhammad [rehema za Allah na amani zimshukie].”

Katika aya hiyo inayopatikana katika Qur’an, 96:1-2 na ambayo ilikuwa ya kwanza kuteremshwa kwa Mtume Muhammad na kutakiwa kuisoma inasema:

“Soma [ewe Muhammad] kwa jina la Mola wako mlezi aliyeumba, ambae aliemuumba mwanadamu kutokana pande la damu.”

Sheikh Abdi anasema kuwa aya hiyo ni mfano mojawapo unaonesha ujuzi na ukubwa wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa binadamu mambo ambayo hupatikana pia katika somo la elimu ya viumbe[biolojia] linalofundishwa katika elimu ya mazingira.

Aidha, Sheikh Abdi aliwataka Waislamu kudumisha udugu baina yao kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe na Uislamu kwa ujumla.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close