Matukio

Niingizeni kwenye amani yenu kama mlivyoniingiza kwenye vita yenu

Kutoka kwa Nuuman bin Bashir (Allah amridhie) amesema, siku moja Abubakar (Allah amridhie) alibisha hodi nyumbani kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akasikia Aisha anazungumza na Mtume kwa sauti ya juu, alipoingia ndani akamshika ili ampige kofi, akamwambia: “Naona unanyanyua sauti yako juu ya Mtume.” Mtume akamzuia. Abubakar akatoka nje hali ya kuwa amekasirika.

Baada ya kuondoka Abubakar, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akamwambia Aisha: “Umenionaje nilivyokuokoa na huyu mtu.” Abubakar akakaa siku kadhaa, kisha akaenda tena nyumbani kwa Mtume. Aliporuhusiwa kuingia ndani aliwakuta wameshapatana, akawaambia: “Niingizeni kwenye amani yenu kama mlivyoniingiza kwenye vita yenu.” Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akamwambia: “Tumeshafanya hivyo.” (Abuu Daudi). Tukio hili linatufunza umuhimu na faida za kuvumiliana, kuzuia hasira na kuishi vizuri na wanawake.

Mtume alivyozuia hasira ya Aisha

Kuna wakati hutokea mume na mke kukwazana katika jambo – liwe dogo au kubwa. Licha ya kuwa na cheo cha Utume, Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa ni mume kama walivyo waume wengine. Yapo baadhi ya mambo yaliyomtokea Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) katika maisha ya kijamii na ya kifamilia.

Katika Hadithi iliyotangulia, Mtume alitofautiana na mama Aisha hali iliyopelekea Bi. Aisha kupaza sauti mbele ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Abubakar (Allah amridhie) alikasirishwa na kitendo cha binti yake kunyanyua sauti mbele ya Mtume, akataka kumpiga. Mtume akamzuia. Baada ya kuondoka Abubakar Mtume alimtuliza Aisha na kumchekesha huku akimwambia: “Unaonaje nilivyokuokoa?”

Huu ni muongozo wa Mtume kwa Waislamu juu ya namna ya kutuliza hasira na kuepuka kuendeleza mvutano na kulikuza jambo. Ubishani unakuza tatizo, pia hupelekea watu kutoleana lugha mbaya au kupigana. Kinachotakiwa ni kutuliza ugomvi kadri inavyowezekana.

Kuwavumilia wanawake
Allah Aliyetukuka amemnyanyua daraja mwanaume kwa kumfanya kiongozi na msimamizi wa familia. Kwa ajili hiyo, mume anapaswa awe mvumilivu, mwenye hekima na busara ya hali ya juu ili azishinde changamoto za kifamilia. Mume hapaswi kushadadia na kulikuza tatizo bali awe upande wa kutuliza na kumaliza tatizo. Mume akishindwa kumaliza tatizo atasababisha mgongano na ukosefu wa amani na utulivu katika jamii. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimtuliza mkewe na kumvumilia bila kujali kuwa amefanya kosa la kupaza sauti mbele yake.

Nasaha za wanazuoni
Tukio hili linatukumbusha nasaha za wanazuoni na adabu mbalimbali walizotufundisha kujipamba nazo pindi mtu anaposhikwa na hasira. Ni wajibu kwa Waislamu kuishi kwa wema, kusaidiana, kunasihiana na kuzuia mambo mabaya yasitokee. Watu wanapokasirika wanaweza kuchukua hatua na maamuzi mabAya na mwishowe kujuta baada ya hasira kuisha.

Imamu Ghazali (Allah amrehem) amesema: “Hakuna ubishi kuwa ndugu anatakiwa awe mwenye msamaha kwa ndugu yake na akubali kuwa udhuru wake huo (sababu iliyopelekea nduguye kukosea) ni wajibu katika haki ya undugu.”

Njia ya kuondoa hasira
SulaIman bin Surad (Allah amridhie) amehadithia kuwa alikuwa amekaa na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Ikawa watu wawili wanatukanana, mmoja wao uso wake ulikuwa mwekundu na mishipa yake ya shingo imetutumuka.

Mtume akasema: “Hakika mimi ninajua neno ambalo kama angelisema hali aliyonayo ingeondoka, kama angesema ‘Audhu billahi minas – shaitwanir – rajiim’ ataondokewa na hilo alilonalo.’” Wakamwambia: “Hakika Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema, ujilinde kwa Allah na Shetani aliyelaaniwa (Sema audhubillahi).” (Bukhari na Muslim).

Pia, katika Hadithi nyingine, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Atakayezuia hasira yake huku akiwa ni mwenye uwezo wa kuitekeleza (kufanya lolote) Allah atamuita mbele za watu Siku ya Kiyama na atampa hiyari ya kumchagua Hurul–ayni (mwanamke wa peponi) amtakaye.” (Abuu Daud na Tirmidhi). Ni kwa kutumia mafundisho ya Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) ndiyo tutaweza kuiepuka hasira.

Usia wa Mtume kwa Maswahaba zake na umma wa Kiislamu Siku moja Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimwambia mtu aliyekuja nyumbani kwake kumuomba ampe usia, akamwambia: “Usikasirike.” Yule mtu akarudia upya kumuomba usia Mtume, Mtume akamwambia: “Usikasirike.” (Bukhari).

Mtume alifahamu kinaga ubaga maisha na tabia za Maswahaba zake, hivyo akawa anawapa usia unaoendana na uhalisia wa maisha yao. Ni kwa ajili hiyo utaona usia wa Mtume kwa Maswahaba zake ulikuwa ukitofautiana kulingana na hali zao na tabia zao.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close