Matukio

Misk ya Roho: Wahadhiri walivyokonga nyoyo za Waislamu

Mada zilizowasilishwa na wahadhiri katika kongamano la pili la kida’awa la Misk ya Roho Jumapili ya Oktoba 28 mwaka huu zimeonekana kuwagusa watu wengi ambao wanashuhudia kuwa zimebadili fikra zao na kusaidia kuwaongezea kiwango cha ufahamu juu ya dini yao ya Uislamu.

Katika kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam na umati wa watu, mada mbalimbali ziliwasilishwa na masheikh kutoka ndani na nje ya nchi ambapo walizisuuza nafsi za watu hao waliyokuwa na shauku ya kuwasikiliza.

Miongoni mwa mada zilizowagusa Waislamu walioongea na gazeti hili ni pamoja na mada ya Sheikh Yusuf Abdi kutoka Kenya ambaye yeye aliwaasa masheikh kutowakatisha tamaa watu juu ya kuomba toba kwa Mwenyezi Mungu kila wanapotenda dhambi.

“Hakuna aliyetubia akabadilika kuwa malaika; masheikh wengine msitudanganye kama hamjafahamu someni mfahamu pale unapowaambia vijana hii ni shere [utani]. Unatenda dhambi, kisha watubia, kesho kutwa watenda dhambi kisha watubia, mnajua kwa msemo huo mmewafanya vijana wengi wasema basi tosha, wacha tule raha, tukishakuwa wazee tutarudi msikitini,” alisema Sheikh Abdi.

Sheikh Abdi aliwanasihi watu waendelee kumuomba msamaha Mwenyezi Mwenyezi Mungu kila wanapokosea: “Mtu akitenda dhambi atubie kwa Allah na akitenda tena atubie kwa Allah na akitenda tena atubie kwa Allah na Mwenyezi Mungu atamsamehe.”

Aidha, Sheikh Abdi ambaye pia ni munshid aliwataka watu watambue kuwa ni Mwenyezi Mungu pekee yake ndiye anastahili kuombwa msamaha nasi mtu mwingine.

“Mwenyezi Mungu pekee ndio wakuombwa msamaha, si mtu mwingine, kufanya vinginevyo huko ni shirki na ni dhambi kubwa sana,” alisema Sheikh Abdi.

Dini ni nyepesi

Aidha Sheikh Abdi alisema kuwa dini ya Uislamu ni dini nyepesi inayoendana na maumbile ya mwanadamu tofauti na baadhi ya watu ‘wanavyoharamisha’ mambo yaliyoruhusiwa na Uislamu.

“Utasikia baadhi ya Masheikh wakiwaeleza wafuasi wao kwamba amefikia daraja kiasi kwamba anasema hata wanawake huwa siwatamani, wakipita mbele yangu huwaona kama ni majiwe na huchukulia kwamba yeye ni mcha Mungu, walahi huyo ni mgonjwa, anafaa akaangaliwe,” alisema Sheikh Abdi.

Sheikh Abdi alisema kuwa huo sio utaratibu wa dini ya Kiislamu kwani Mwenyezi Mungu amewataka watu waoe na kuongeza kuwa watu hawapaswi kubadili utaratibu uliyowekwa na Mwenyezi Mungu. Akitolea mfano zaidi, Sheikh Abdi alisema kuwa hata Mtume Muhammad alipomuona mke wake anaswali usiku huku amechoka na anasinzia alimwambia akapumzike, hapa mhadhiri huyo akiamanisha kuwa kila jambo halali katika dini lina nafasi yake muhimu.

Maoni juu ya mada hiyo

Akizungumzia mada hiyo, Rashid Said anasema ni mada nzuri kwa kuwa imezoeleka kwa baadhi ya masheikh na wale wenye elimu ya dini kutoa mawaidha yenye muelekeo wa kuwakatisha tamaa watu juu ya toba.

Mimi nimependa mada ya Sheikh Yusuf Abdi kwani amezungumzia suala la mtu kutokata tamaa ya kuomba toba kwa Mwenyezi Mungu, na unajua binadamu tuna makosa mengi sana,” alisema Said
na kuongeza,

“Mara nyingi baadhi ya masheikh zetu hupenda kutoa mawaidha ya kuwakatisha tamaa waumini wao kiasi kwamba mtu kama alitenda dhambi anaonekana amelaaniwa moja kwa moja, kumbe dini bado inatoa fursa ya kuomba toba kwa mtu huyo.”

Kwa maoni yake Muhammad Juma anasema pamoja na kwamba watu wanapaswa kutubia mara kwa mara, ila hawana budi kufahamu kuwa hawajui siku yao ya mwisho hapa duniani hivyo ni vema wakatubia toba ya kweli.

“Sawa tutubu mara kwa mara ila isiwe kama ndio mchezo, kifo hakijulikani kinakuja lini, ni vizuri mtu akatubu kabisa kwa makosa aliyoyatenda,” alisema Juma.

Naye Abdulkarim Hassan anasema amejifunza kuwa Muislamu hana budi kufanya sana ibada ila pia anapaswa kushiriki katika mambo mengine yaliyoruhusiwa na Mwenyezi Mungu hapa duniani.

Kuna baadhi ya watu wao utawasikia wao wakihimiza ibada tu za kuswali, kufunga kiasi kwamba mambo ya kimaisha kwao hayana nafasi, nashukuru Sheikh Abdi amelieleza vizuri hili suala kuwa ibada ni muhimu ila kuna mambo ya kimaisha pia,” alisema Hassan.

Hassan anawatolea wito masheikh na wale wenye ufahamu wa dini kujaribu kutoa mawaidha ambayo yanagusia masuala ya akhera pamoja na ya hapa duniani ili watu wasije wakaacha neema zilizowekwa na Mwenyezi Mungu.

Sheikh Abdulrahman Mhina [Baba Kiruwasha]

Mhadhiri mwingine aliyeonekana kuamsha hamasa na kuwagusa watu wengi ni Sheikh Abdulrahman Mhina [Baba Kiruwasha], ambaye alizungumzia mada juu ya ‘Upi ni upendo wa kweli?’

Baba Kiruwasha alisema kuwa upendo wa kweli ndio msingi wa ndoa yoyote ile na unapokosekana basi ndoa huwa katika misukosuko.

Kama upendo haupo katika ndoa basi maisha ya ndoa yanakuwa ni moto mkali, hivyo tufahamu kuwa kwenye amani ndio kwenye upendo, kwenye upendo ndio kwenye amani,” alisema Baba Kiruwasha.

Kuhusu upendo wa kweli, Baba Kiruwasha alisema ni upendo ambao watu hawapendani kwa ajili ya maslahi ambapo alibainisha maslahi hayo yanaweza kuwa ni mtu kumpenda mtu kwa kuwa uzuri fulani, mali yake nakadhalika. Baba Kiruwasha alisema huo sio upendo bali ni upendo fake[wa uongo] na kuwaomba Waislamu wamsome Mtume Muhammad ambae aliishi na wake zake kwa upendo mkubwa.

Kuhusu mada ya baba Kiruwasha, Nurdin Ibrahim yeye anasema ni jambo ambalo linapaswa kuzungumzwa mara kwa mara kwani ndoa nyingi zimekuwa na migogoro kutokana na watu kutopendana.

Baba Kiruwasha ametoa elimu kubwa ya ndoa, watu tumejifunza maana ya upendo wa kweli, na natumai amesaidia watu wengi maana ndoa nyingi za siku hizi hazina upendo,” alisema Ibrahim.

Naye Zamda Ashraf anasema kuwa mada ya baba Kiruwasha imemgusa kwa kuwa imemsaidia ajifunze kuutambua upendo wa kweli wakati watu wanatafuta wachumba.

Watu wengi wanakosea pale wanapotafuta wachumba, baba Kiruwasha leo katwambia upendo wa kweli ni kumpenda mtu jumla jumla na wala siyokuangalia sehemu ya mwili wake au mali zake,” alisema Zamda Ashraf.

Sheikh Ally Kajura[Rwanda]

Naye Sheikh Ally Kajura [Rwanda] alisema furaha ya kweli inatoka kwa Allah na Mtume wake na hivyo kuwataka Waislamu wawekeze zaidi upendo wao kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Sheikh Kajura anasema kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake kunamfanya mtu awe na maisha mema hapa duniani na akhera.

Tukimpenda Mwenyezi Mungu, tutakuwa na maisha mema hapa duniani na Akhera, kwa hiyo Waislamu lazima tumpende Mwenyezi Mungu kama walivokuwa Maswahaba ambao hawakupenda sana vitu vingine zaidi ya Allah na Mtume wake,” alisema Sheikh Kajura.

Sheikh Jamaldin Osman [ Kenya]

Kwa upande wake, Sheikh Jamaldin Osman kutoka Kenya aliwanasihi Waislamu kutojikita zaidi katika masuala mengine na kusahau kumtaja Mwenyezi Mungu na kufanya ibada.

Sheikh Osman alisema kuwa mtu anayemtaja sana Mwenyezi Mungu ndio mwenye furaha ya kweli na yule mwenye kumsahau Mola wake basi anakuwa na maisha magumu hapa duniani na Akhera.

Aidha, Sheikh Osman alibainisha kuwa mwanadamu hana budi kukaa karibu na Mola wake ili apate ulinzi wa maisha yake.

Mwanadamu akimuelekea Mola wake kwa ukweli, basi Mwenyezi Mungu atamuhifadhi,” alisema Sheikh Osman.

Masheikh wengine

Masheikh wengine waliyotoa mada katika kongamano hilo ni Sheikh Zuberi Bizimana [Burundi], Sheikh Muhammad Abduweli kutoka Uganda na kwa hapa nchini alikuwepo pia Sheikh Dourmohamed Issa na Sheikh Ally Jumanne.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close