1. Habari1. TIF NewsMatukio

Misk ya Roho: Tulipotoka na tunapoelekea

Kila sifa njema anastahiki Allah (Subhanahu wataala) pekee, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Rehema na salamu zimuendee Mtukufu wa Daraja, kipenzi chetu Mtume Muhammad pamoja na Maswahaba zake na waliotutangulia kwa wema mpaka siku ya mwisho.

Napenda kuchukua fursa hii adhimu kuwakaribisha wapenzi wasomaji katika safu hii ambayo kwa taufiki ya Allah tutawaletea mfululizo wa makala zihusuzo ujio wa Kongamano la Tatu la Afrika Mashariki lijulikanalo kama Misk ya Roho 2019.

Misk ya roho ni kongamano la kida’awah la Afrika Mashariki linaloandaliwa na taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) chini ya Idara ya Da’awah (kitengo cha makongamano).

Kupitia kongamano hili, tunaalika masheikh na walinganiaji mbalimbali kutoka nchi za Afrika Mashariki –yaani- Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa Allah kwa jamii.

Kimsingi, Misk ya Roho ni moja ya jukwaa adimu linalounganisha udugu kati ya masheikh waalikwa, wahudhuriaji na waandaaji.

Nikikumbuka na kukariri vizuri maneno ya mmoja wa masheikh waliohudhuria Kongamano la Pili la Misk ya Roho 2018 akipiga soga na masheikh wenzake wakati wa chakula cha usiku alisema: “Ni fursa iliyoje nikiwa na miaka michache katika da’awah kupata wasaa wa kuhutubia jukwaa moja na masheikh nguli walioanza kufanya da’awah miaka mingi kabla yangu kuzaliwa.” Kwa muktadha huu, tunaweza kung’amua ukweli kuwa Misk ya Roho ni jukwaa huru kwa walinganiaji wa kada tofauti kutoka Afrika Mashariki kubadilishana uzoefu na utendaji linganifu katika tasnia ya da’awah katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Sanjari na hayo tunashuhudia kuwa wanaofaidika na makongamano haya
si wahudhuriaji tu kwa kupata maneno kutoka katika Kitabu na Sunna, bali pia watu katika nyanja na medani tofauti tofauti. Mfano mzuri ni pale watu popote pale walipo duniani wanapoweza kutazama mubashara makongamano haya kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo vyombo vya habari vya Imaan (redio na runinga) pamoja na vyombo vya habari washirika.

Makongamano haya ni njia mojawapo ya kuonesha umoja, mshikamano na ushirikiano wetu. Umoja na mshikamano huu unaweza kuwa fursa kwa wafanyabiashara kufahamiana na kutambuana, aina ya shughuli wanazojishughulisha nazo (interaction platform).

Lakini pia inaweza kuwa fursa ya kutumia mali yako katika njia anayoipenda Allah na kuiridhia kwa kujitolea kudhamini. Ukidhamini, mbali na kuwafaidisha watu, pia kongamano hili linaweza kukusaidia kukuza biashara yako kwa matangazo na kwa kutumia mali yako katika njia ya halali. Kwa mtazamo mwingine, hii ni njia ya kuepuka kutumia mali yako katika njia isiyofaa.

Mwisho kabisa ningependa kuwafahamisha wasomaji wa gazeti hili kuwa jiandaeni panapo majaliwa inshaaAllah mtalipokea Kongamano la Tatu la Afrika Mashariki.

Na katika matoleo yajayo InshaaAllah tutapata muhtasari wa mada zilizohudhurishwa na masheikh waliohudhuria kongamano la Misk ya Roho mwaka 2018, na pia tutakuwa tukitoa taarifa zihusuzo kongamano hili kwa kadiri zitakavyokuwa zikijitokeza.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close