Matukio

Kwa ajili ya kupata Radhi za Allah

Umeshawahi kuwa katika sehemu ambayo umezungukwa na watu wengi lakini bado ukajihisi mpweke? Mara nyingine tunahisi kama kuna kitu kimekosekana na mara nyingine tunajilaumu kwa kuwa katika muda huo, mioyo yetu haihisi ukaribu na Allah. Unahisi pumzi kama vile imekuwa nzito na kuna maumivu katika roho yako.

Katika njia rahisi za kutufanya tuhisi kama tunavuta pumzi safi na kupelekea kupata utulivu wa roho, ni kuwa katika vikao vya wale ambao mioyo yao imekuja pamoja kwa ajili ya Allah (swt). Roho zao safi na tabia zao njema, hutufanya tuhisi jua lililokuwa limepotea, limechomoza tena maishani mwetu, na kuleta mwangaza. Ni wale ambao wenye uzuri katika fikra zao, mioyo yao na roho zao, wenye wema katika kila wafanyayo kwa kuwa muhimu zaidi kwao wao, ni mapenzi yao kwa ajili ya Allah (swt) na kuitafuta ridhaa yake. Ni wale ndugu zetu wa ukweli, ambao tukiwaona wanatufanya tumkumbuke Allah na tukiwa nao imani zetu huongezeka. Umewafahamu kwa muda mchache lakini unahisi kama vile umekuwa ukiwafahamu milele.

Ni uwepo wao, unaoifanya hali ya roho yako asubuhi ya kwenda kujitolea kwa ajili ya Allah iwe tofauti kabisa na hali yako jioni, pale ambapo shughuli inapokwisha, kwa sababu wanaokuja katika shughuli hizi wanakuja na malengo tofauti, si kama shughuli nyingine za kawaida. Basi na sisi tusafishe nia zetu na tuwe wawakilishi wa wema, ili tuweze kuifanya kazi ya Allah (swt) kwa heshima inayostahili.

Je, unatafuta marafiki wa kweli?

Kumbuka, rafiki wa kweli ni yule ambae anataka wewe uwe karibu na Allah kama anavyotaka yeye. Yupo tayari kukusaidia kwa hali na mali katika safari yetu hii ya kumuelekea Allah. Kama yupo tayari kujitolea kwa ajili ya  kupata ridhaa ya Allah peke yake, basi mtu huyu hatopata tabu kutoa kila alichonacho katika kulifikia lengo lake hilo. Atajitahidi kutumia kila alichopewa na Allah (swt), iwe ni nguvu zake, afya yake, mali yake na hata tabasamu lake katika njia hii.

Katika dunia hii ilojaa giza, tunahitaji kuzungukwa na watu wenye nuru. Nuru ni wewe, unayejitolea kadri uwezavyo kwa ajili ya Allah. Kwa kuwa si kazi ya mtu mmoja, tunapoungana tunakuwa chanzo cha mwanga thabiti wa Uislamu. Mioyo inayoungana kwa mapenzi yao ya Allah (swt), ndio inayosukuma damu ya wema katika jamii.

Kumbuka, rafiki wa kweli ni yule ambae anataka wewe uwe karibu na Allah kama anavyotaka yeye.

Tuwe mfano dhahiri wa huruma, wema na tabia zote njema alizotufundisha Mtume wetu (saw), hivyo kuonyesha matumaini kwamba watu wa kweli bado wapo duniani. Kuna maneno ya hekima yaliwahi kusemwa, “Nisipowaka mimi, usipowaka wewe, tusipowaka sisi, giza la dunia litaondoka vipi?” Ni maneno yanayonipa nguvu ya kuendelea pindi ninachokifanya kinapokuwa kigumu. Itabidi ujikumbushe kwamba wewe ni mshumaa; waka, ungua, maumivu yachukuwe wewe, ili utoe mwanga. Hakika malipo yake ni makubwa zaidi.

Hakuna kitu cha thamani kama imani, kama utulivu, na usafi wa roho. Wahimize wale unaowapenda kwa ajili ya Allah, waendelee kujitolea kwa ajili yake ili kuthibitisha upendo wako kwao.Tujitahidi bila kuchoka mpaka siku tutakayovuta pumzi yetu ya mwisho, ili tutakapokutana na yeye ambae tumeishi kwa ajili yake, tuweze kusema, “Kwa kile ulichonipa, ya Allah, nilikitoa kwa ajili yako, kwa kuwa ni kwako wewe kilitoka, hivyo kwako wewe nilikirudisha.”

Namuomba Allah (swt) azikubali juhudi zetu, atuongezee nguvu ya kuitumikia dini yake na daima atuweke miongoni mwa waja wake wema, wanaotukumbusha uwepo wake. Amin.

Islamicftz.org/kujitolea

Tags
Show More

Mariam Mohamed Mzingi

ni mwanafunzi wa udaktari mwaka wa tatu. Licha ya masomo hayo magumu, amekuwa akiandika na kutafsiri makala mbalimbali, pamoja na kujitolea katika shughuli za kuitumikia jamii. Anapenda kujifunza lugha na kujumuika na watu wa tamaduni mbalimbali. Ni mmoja kati ya wanaojitolea katika timu ya masoko na mitandao ya kijamii ya TIF. Anasaidia katika kutafsiri, kuandika nakala na kuhariri.

Related Articles

Back to top button
Close