Matukio

Kumtii Allah si maneno tu bali vitendo, Sheikh Abduweli

Kumshukuru Allah si kusema Alhamdulillah, bali kumtii kwa kutenda mema na kuacha makatazo yake.” Hayo ni maneno aliyoyasema Sheikh Muhammad Abduweli wakati wa Kongamano la Kida’awa la Afrika Mashariki ‘Misk ya Roho’ lililofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es salaam.

Sheikh Abduweli aliyekuwa akiwasilisha mada ‘Ukubwa wa Mwenyezi Mungu’ alisema kuwa watu wengi katika zama hizi wamekuwa wakiwategemea zaidi wanadamu wenzao kuliko Allah tofauti na Maswahaba wa Mtume [Allah awaridhie] ambao wao walikuwa wakimtegemea zaidi Allah kwa kila kitu.

Mwenyekiti wa The Islamic Foundation pamoja na wahadhiri wa Misk Ya roho 2018

Sheikh Abduweli alisema kuwa, kila siku wanadamu wanalala na kuamka lakini hawajui ukubwa wa Mwenyezi Mungu na ndio maana wanamuasi Allah na wala hawafanyi toba.

Daima mtu anayemjua Allah kisawasawa hawezi kumuasi Allah, na badala yake atamhofu Allah kila wakati. Mwenyezi Mungu alianza kutushukuru kabla ya sisi kumshukuru, hivyo yeyote ambaye hamjui Mwenyezi Mungu basi hana anachokijua,” alidokeza Sheikh Abduweli.

Na kwa sababu Mwenyezi Mungu anajua mambo ya siri na ya dhahiri yanayofanywa na viumbe wake, Sheikh Abduweli aliitaka hadhira ya kongamano hilo kutumia fursa ya uhai wao kutubia kwa Mola wao kwani hiyo ndio njia ya kuepuka adhabu ya Allah siku ya kiyama, akinukuu aya ya Qur’ an, 2:186 isemayo,

Na watakapokuuliza [Muhammad] waja wangu kuhusu mimi, waambie mimi niko karibu nao, nasikia maombi ya muombaji, pindi anaponiomba. Basi wanitii Mimi Katika niliyowaamrisha na niliyowakataza, na waniamini ili wapate kuongoka.”

Katika hatua nyingine, Sheikh Abduweli aliwataka Waislamu kusoma, kuhifadhi na kufanyia kazi Qur’ an kwani kufanya hivyo kutawafanya watambue ukubwa na utukufu wa Mwenyezi Mungu. Sheikh Abduweli alisema:

Si sahihi Muislamu kuhifadhi Qur’an pasina kuifanyia kazi.”

Sheikh Abduweli alimalizia kwa kusema: “Wengi kati ya wale wanaohifadhi Qur’ an hawazingatii yaliyomo ndani yoke na kwamba lau wanadamu wangejua ukubwa wa Mwenyezi Mungu basi roho na nafsi zao zingetetema na kupata woga.”

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close