Matukio

‘Kuihudumia Dini’ Na Sheikh Zuberi Bizimana

Sheikh Zuberi Bizimana ni mmoja kati ya Masheikh waliobahatika kuwasilisha mada katika kongamano la Misk ya roho lililofanyika Novemba 26, mwaka 2017 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Sheikh Bizimana alizaliwa huko Buyenzi nchini Burundi na kutokana na mapenzi yake ya kutafuta elimu ya dini alipata fursa ya kusoma katika chuo cha Muhammad Ibn Al-Saudi kilichopo Riyadh nchini Saudi Arabia.

Akihutubia kwenye kongamano hilo la Misk ya Roho, alianza muhadhara wake kwa kutoa kisa cha kijana mmoja mwenye nguvu na mwenye kupendeza, ambaye yeye na familia yake waliishi katika mji fulani wenye maendeleo, mji wenye nguvu, nafasi na utukufu lakini wakazi wa mji huo uliofadhilishwa walimkufuru Mwenyezi Mungu na kuzifanyia vitimbi aya zake Allah.

Wakazi wa mji huo pamoja na viongozi wao walikutana kujadili jambo ovu la kuufanyia uadui na kuuvunja Uislamu na Waislamu wenyewe kwa ujumla. Pamoja na maazimio mengi katika mkutano huo lakini azimio lao kuu lilikuwa ni kuupiga vita na kuuvunja Uislamu na Waislamu.

Kijana huyu hakuweza kusema apingane na haki na wala hakuwa na uvivu wa aina yoyote katika kuutetea uislamu ingawa alikuwa peke yake kwenye azma ya kuutetea na kuuhami Uislamu. Kijana huyo alithubutu kusimama mbele ya watu wa mji wote ili wasiweze kutekeleza azma yao ya kuupiga vita Uislamu na kuwauwa watu wote wanaolingania dini ya Allah.

Alipata ujasiri wa kusimama mbele yao kuwapa mawaidha na akawakumbusha wasitekeleze waliyoazimia lakini walichoamua kukifanya ni kumuua kinyama. Kisa hiki kikasimuliwa tena kwa maneno ya Allah ndani ya Surat Yasin (Quran, 36:13-26).

Baada ya kisa hicho, Sheikh Bizimana aliwaambia Waislamu kuwa amewaletea barua tano, na katika barua hizo
tano kila Muislamu achague barua moja ambayo ataenda nayo nyumbani.

Barua ya kwanza…

Kutoka katika kisa cha Nabii Nuh [Amani iwe juu yake] Anasema Allah Mtukufu: “Na hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka hamsini…,” [Qur’ an, 29: 29- 14].

Katika surah hii, Allah anatuonesha kuwa Nabii Nuh [Amani iwe juu yake] aliwalingania watu wake kwa muda wa miaka 950, na kazi aliyoifanya Nabii Nuh inasimuliwa katika Qur’ an Surat Nuh ambayo ni sura ya 71 kuanzia aya ya kwanza mpaka ya 28.

Katika sura hiyo kuanzia aya ya 5 mpaka ya 9, Allah Aliyetukuka anasema: “Akasema: Ewe Mola wangu mlezi! Hakika mimi nimewaita watu wangu usiku na mchana. Lakini wito wangu haukuwazidishia ila kukimbia. Na hakika mimi kila nilipowaita ili upate kuwaghufiria, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia, na wakatakabari vikubwa mno. Tena niliwaita kwa uwazi. Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao kwa siri.”

Lakini pamoja na juhudi zote hizo, kwa miaka 950 bado hawakutaka kuwaidhika wakamfanyia vitimbi vikubwa. Sheikh Bizimana alisema barua hii imfikie kila Muislamu na impe moyo wa kulingania dini, kwamba kazi ya kulingania haina malipo yoyote hapa duniani isipokuwa malipo yapo kwa Allah na kazi hii haina mwisho.

Barua ya pili…

Kuitumikia dini ya Allah ni kazi ya kila Muislamu

Hapa Sheikh Bizimana alitukumbusha kuwa kazi ya kulingania dini ni kazi ya waislamu wote; wanaume na wanawake. Akatoa kisa cha jamaa mmoja aliyekwenda kwa Mtume Muhammed [rehma na amani za Allah ziwe juu yake] akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi nimekuja kusilimu lakini nataka nikapigane vita kisha nisilimu,” Mtume akawambia: “Laa silimu kwanza halafu ndio ukapigane vita.” Yule mtu akasema: “Nashuhudia kuwa hakuna Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah, na nashuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wake.” Kisha akasilimu na baada ya kusilimu akaenda kupigana vita na kufariki.

Jamaa huyu kaishi katika uislamu siku moja tu akaenda kupigana na akafariki akiwa katika dini ya Allah akimpigania Allah. Je, wewe na mimi tulioishi katika Uislamu toka kuzaliwa kwetu na hatujafanya kitu, tutaenda kumwambia nini Mola wetu siku ya kiyama?

Sheikh Bizimana alimaliza kwa kusema, hakika kuitumikia dini ya Allah na wewe kuwa muislamu ni pacha mbili, katu haziachani, ukiwa muislamu una jukumu la kuitumikia dini.

Barua ya tatu…

Kulingania Dini

Katika barua ya tatu, Sheikh Bizimana alisema: ‘Tazameni Yusuf [amani ya Allah iwe juu yake] ameingizwa katika jela, tena kwa dhuluma lakini hakulalamika na wala hakusahau kulingania mpaka ndani ya jela’. Sheikh Bizimana anasema Yusuf alitafuta namna ya wale watu kumwamini zaidi akawaambia: “Ninadhani kila mfungwa aliyekuwa hapa, chakula atakachopikiwa nyumbani kabla hakijaja mimi nakijua.” Na kweli alipewa uwezo huo na Allah, na kuvuta imani za wafungwa wale.

Aliendelea kuwajenga kiimani mpaka alipofikia malengo yake ya kuwalingania akasema: “Licha ya kuwalingania ninyi lakini nimewaacha ndugu zangu wanaamini kinyume na Allah”. Hili ni funzo kwetu kuwa, pamoja  na magumu yote tunayopitia au dhuluma zote tunazofanyiwa bado tuna jukumu la kulingania dini ya Allah.

Elewa kwamba kazi ya kulingania dini ya kiislamu inaendelea mpaka pale roho yako itakapotolewa.

Na hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka hamsini…” [Qur’an, 29: 29- 14]

Barua ya nne…

Kisa cha swahaba Abuu Mihjaan Al-Thaqafi

Katika barua hii ya nne, Sheikh Bizimana alisema kuwa kuna baadhi ya watu kutokana na mwenendo mbaya wa maisha yao, wamezama katika maasi, na Iblisi anawajengea hofu ya kujiona kuwa hawafai na hawawezi kufanya kazi ya dini. Kwa hali hiyo Sheikh Bizimana aliwataka Waislamu wafuatilie kisa cha swahaba wa Mtume aliyekuwa mlevi na bado alifanya kazi ya dini.

Swahaba huyu alikuwa ni mlevi kupita kiasi na kila alipokuwa akinywa pombe alikuwa akiadhibiwa kwa kupigwa fimbo 40 za adhabu ya mlevi kama ilivyo katika sharia ya kiislamu, lakini bado siku ya pili alikuwa anarudia kunywa na wala hakuona ulevi huo kama unampa uzito wa kufanya kazi ya Allah, alikuwa ni mmoja wa wapiganaji wa Jihad na kamwe hakuuchukulia ulevi wake kama udhuru wa kuacha kufanya kazi ya dini.

Katika vita vya ukombozi wa mji wa Fursi [Iran ya leo] vilivyoongozwa na swahaba Saadi Ibn Abi Waqas, miongoni mwa wanajeshi wa jeshi la kiislamu, alikuwepo Abuu Mihjaan Al-Thaqafi. Walipokuwa kambini aliwatoroka akaenda kutafuta pombe na akarudi amelewa, anapepesuka, na alipoonekana na kiongozi wa vita, Saad alikasirika sana ila hakumpiga tena na akampa adhabu ya kutopigana ingawa alitoroka na kwenda kuongeza nguvu katika jeshi la waislamu lililoshinda vita hiyo, lakini alilia kwa uchungu wa kukatazwa kushiriki vita kwa sababu ya ulevi na hiyo ikawa ni sababu ya kuacha ulevi na kuongoka.

Basi usidhani kama wewe huwezi kulingania dini ya Allah kwa sababu ya dhambi zako, lingania dini ya Allah huku ukimwomba akuondoshe kwenye tabia hiyo chafu.

Barua ya tano…

Kisa cha hud hud

Na katika barua ya mwisho, Sheikh Bizimana alisema siku moja alikuja Nabii Suleiman, akalitazama jeshi lake na kumkosa hud hud, alikasirika na kusema kwa kiapo: “Nitamchinja isipokuwa akija na habari [au hoja] itakayomsaidia.” Hud hud akarudi na kuwakuta wanajeshi wakiwa na huzuni wamebadilika kwa majonzi.

Suleiman akamwona na kabla hajaongea, hudhud akasema: “Nimezunguka na nimefika kule wewe hujafika, na nimekuja kutoka Saba’a [Sheba] na habari nzito.” Hud hud akampa habari ya Malkia Balqis na washirikina [Kama ilivyoelezwa katika Qur’ an [27: 27-44]. Sheikh Bizimana alihitimisha muhadhara wake kwa kubainisha kuwa hii ni kazi iliyofanywa na hudhud, iweje wewe kiumbe wa Allah aliyekujaalia zaidi ya viumbe vingine ushindwe na mnyama?

Tags
Show More

Limbanga M. Limbanga

ni mhandisi wa Umeme na Elekroniki. Pamoja na shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa katika uhandisi pia anatumia muda wake katika kujitolea kuandika,kuhariri na kutafsiri makala mbalimbali, ni mmoja kati ya vijana wa kujitolea katika taasisi ya TIF katika masuala ya kidini na kijamii. Anapendelea kuielemisha jamii na kutumia ujuzi wake kunufaisha wengine.

Related Articles

Back to top button
Close