Matukio

Kipyenga cha Misk ya roho Kimeshapulizwa

Kamati ya maandalizi yanena

Furaha isiyo kifani ilitawala katika nyoyo za wapenzi na mashabiki wa Kongamano la Afrika Mashariki la Misk ya Rohokufuatia kamati ya utendaji ya kongamano hilo kutua ndani ya studio za Redio na Televisheni Imaan zilizopo katika ofisi za makao makuu ya taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) zilizopo eneo la Msamvu mkoani Morogoro.

Safu hiyo ya uongozi iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Makongamano, Tajmohamed Abbas ilipata wasaa wa kuuhabarisha umma kuhusu ujio wa Kongamano la Tatu la Afrika Mashariki (Misk ya Roho 2019).

Wengine waliombatana na Mkurugenzi wa Makongamano ni Niyazhan Ibrahim ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa makongamano pamoja na Ramadhani Maulid ambaye ni Meneja Mauzo.

Katika kipindi maalum cha Tv na Redio Imaan, yalielezwa mengi yahusuyo Kongamano la Misk ya Roho, umuhimu wake, mafanikio na changamoto za makongamano yaliyopita. Akilielezea kongamano hilo, Naibu Mkurugenzi wa Makongamano, Niyazhan alisema Misk ya Roho ni kongamano la kida’awah la Afrika Mashariki linaloandaliwa na taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) chini ya Idara ya Da’awah, Kitengo cha Makongamano.

Niyazhan alisema, taasisi huwaalika masheikh na walinganiaji mbalimbali kutoka nchi za Afrika Mashariki yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa Allah kwa jamii.

Mpaka sasa, tayari yameshafanyika makongamano mawili ya Misk ya Roho ambapo kongamano la kwanza lilifanyika mwaka 2017 na la pili lilifanyika mwaka 2018. Kamati sasa ndio ipo katika harakati za kuandaa msimu wa tatu wa kongamano la Misk ya Roho 2019.

Kwa mujibu wa Niyazhan,katika makongamano yote hayo, masheikh kutoka nchi zote za Afrika Mashariki wamekuwa wakihudhurisha mada mbalimbali zenye kuunufaisha umma.

Naye Mkurugenzi wa Makongamano wa taasisi ya TIF, Tajmohamed Abbas alisema makongamano yaliyotangulia yalifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika vipengele vya mahudhurio, mada zilizowasilishwa na katika kuacha athari.

Maboresho Misk ya Roho 2019

Akizungumzia maboresho, Niyazhan alisema tangu mwanzo wa makongamano haya, kamati ya utendaji ya maandalizi imekuwa ikijitahidi kulifanya kongamano hili liwe bora zaidi na mwaka huu In shaa Allah watu watarajie mengi mazuri.

Tayari wahadhiri wa mwaka huu wametajwa wakiwemo Sheikh Djumapili Mbabajende (Rwanda)Sheikh Zuberi Bizimana (Burundi), Sheikh Muhammad Abduweli (Uganda).

Wahadhiri kutoka Kenya ni Sheikh Yusuf Abdi na Sheikh Abubakar Abdi Abubakar Yassin (Sheikh Abu Hamza). Masheikh wenyeji kutoka Tanzania ni Sheikh Ibrahim Twaha na Dk. Sheikh Salim Qahtwan.

Katika kipindi hicho maalum, Mkurugenzi Tajmohamed Abbas alitaja tarehe itakayofanyika kongamano la Misk ya Roho kuwa ni Desemba 1, 2019 palepale katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Tajmohamed alisistiza watu kuhudhuria katika kongamano hilo ili wafaidike, ambapo mada kuu ya kongamano itahusu kitabu kitukufu Qur’an, ambacho ni muujiza na ufunuo wa mwisho kwa umma huu.

Tajmohamed alisema, kongamano hili pia litapambwa na mada mbalimbali chini ya mwamvuli wa mada hiyo kuu ambayo ni ‘Kitabu Changu…’

Kwa upande wake, Meneja Mauzo, Ramadhani Maulid aliwashukuru watu wote waliojitokeza katika makongamano yaliyopita na kuwasihi wajitokeze kwa wingi katika makongamano yajayo ikiwemo hili la Misk ya Roho 2019.

Maulid alitaja vituo vya mauzo ya tiketi za kongamano kuwa ni

 • Kanzu Point iliyopo City Mall (Barabara ya Morogoro na bibi Titi),
 • Taste Me Upanga na Dar Free Market, Street Soul Mlimani City,
 • GGS Bolts and Nuts Kariakoo (Makutano ya mtaa wa Livingstone na Mafia),
 • Ibn Hazm Bookstore (Msikiti wa Mtambani), Duka la Kanzu Zetu Ilala mtaa wa Arusha,
 • Yaqub Jewellers Posta mtaa wa Indira Gandhi na Mlimani City,
 • Msikiti wa Kichangani Magomeni Mikumi (Piga 0714 541957),
 • Msikiti wa Irshaad Tandika mtaa wa Chihota (Piga 0710 100605),
 • Mbagala Rangi tatu Sokoni (0715 328512),
 • Buguruni kwa Mnyamani karibu na Hospitali ya Plan (0655611248),
 • Masjid Munawwar Chanika kwa Baniani (0655 912437),
 • Msikiti wa Ijumaa Gongo la Mboto (0689 849020),
 • Msikiti wa Matangini Kimara (0715 903098),
 • TIF Hub Kituo cha Mwendokasi Morocco Kawawa Road (0715 827337) na
 • Mkoa wa Morogoro ni Msamvu Makao Makuu ya Taasisi ya The Islamic Foundation. Tiketi hizi zinapatikana kwa gharama ya shilingi za kitanzania 10,000/= tu.

Pia unaweza kununua tiketi kwa njia ya mtandao ambayo ni kupitia namba ya Tigo Pesa 0718 000433 na M-Pesa ni 0742 877775 Hakikisha jina ni Tajmohamed Shaaban.

Kwa kumalizia Naibu Mkurugenzi wa Makongamano ndugu Niyazhan Ibrahim alisisitiza watu kuwahi kujipatia tiketi zao mapema iwezekanavyo ili kuepuka usumbufu siku za mwishoni ambapo uhitaji unakuwa mkubwa na hivyo wengine kukosa nafasi ya kuhudhuria kongamano hilo.

Mwisho kabisa ningependa kuwafahamisha wasomaji wa gazeti hili wakae mkao wa kula wakijiandaa kulipokea kongamano la tatu la Afrika Mashariki.

Ukihitaji maelezo zaidi kuhusu kongamano hili fuatilia katika kurasa za mitandao ya kijamii ya @Islamicftz au kupitia tovuti maalum ya kongamano hili www.miskyaroho. islamicftz.org

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close