Matukio

HAY–AT yatunuku wahitimu kozi ya uimamu na uongozi

Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay–at) kwa kushirikiana na Chuo cha ualimu na uongozi Kigogo umewatunuku vyeti pamoja na vitabu mbalimbali vya dini ya Kiislamu wahitimu 23 wa kozi ya uimamu na uongozi wa maendeleo ya jamii kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Hafla ya kuwatunuku wahitimu hao ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa Lamada uliopo Ilala, jijini Dar es Salaam, ambapo pia wito umetolewa kwa maimamu wa misikiti kujifunza elimu mbalimbali zinazohitajika kwa maendeleo na ustawi wa jamii. Katika hafla hiyo, Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum aliwakabidhi vyeti wahitimu 23, ambao kwa muda wa miezi 6 kuanzia Aprili mosi, 2018 hadi Novemba 30, 2019 walikuwa wakipatiwa mafunzo mbalimbali yakiwamo ya usimamizi wa misikiti na ujasiliamali kutoka kwa wakufunzi mbalimbali na Masheikh wa Hay–at.

Sheikh Kilemile na misikiti Akizungumza katika mahafali hayo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu nchini (Hay–at), Sheikh Suleiman Kilemile alisema kuwa misikiti mingi ya Waislamu katika zama hizi imepotezwa lengo lake tofauti na ilivyokuwa wakati wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). “Msikiti wa Mtume ulikuwa ndiyo bunge, ndiyo sehemu ya kufanya mashauri ya maendeleo ya jamii ya Kiislamu …hiyo ndiyo moja ya kazi za misikiti,” alidokeza Sheikh Kilemile na kufahamisha kuwa Uimamu ni taaluma pana hivyo mwenye kuutaka anapaswa awe na utambuzi wa mambo mbalimbali ya kidini na kijamii.

Sheikh Kilemile aliongeza: “Uimamu si kusalisha …kuongoza sala ni sehemu ndogo ya majukumu ya Imamu. Imamu ni yule anayewazidi wengine kusoma Qur’an na kuielewa vema. Ajabu ni kwamba siku hizi kila fani ina cheti isipokuwa Uimamu. Hivi sasa mtu yeyote akiweza kusoma Surat Fat’ha (Alhamdu) na Ikhlas (Qulhuwa llahu) anafanywa kuwa Imam.”

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Sheikh wa mkoa wa Dar es salaam, Alhad Mussa Salum amewataka Waislamu kujiepusha na makundi ya upotovu na yaliyopitukia mipaka katika dini, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakiwatusi na kuwavunjia heshima Maswahaba watukufu (Allah awaridhie). Sheikh Alhad aliiambia hadhira ya mahafali hayo kuwa, makundi ya upotovu ni tatizo kubwa ambalo athari yake haishii tu kwa Waislamu bali jamii nzima. “Jihadharini na wanaowatusi Maswahaba wa Mtume na wale wanaowatoa Waislamu katika madhehebu sahihi na kuwapeleka kwenye madhehebu ya upotofu,” alisisitiza Sheikh Alhad.

Sambamba na hilo, pia Sheikh huyo wa mkoa wa Dar es Salaam aliwataka wahitimu hao wa kozi ya uimamu na uongozi kuzingatia vema maadili ya dini sanjari na kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa Waumini wanaowaongoza. Sheikh Alhad aliongeza kuwa, baadhi ya maimamu wamekuwa wakivalia mavazi yasiyoendana na utamaduni wa Kiislamu, ambapo ametoa mfano jinsi baadhi yao wanavyovaa mavazi kama wanayovaa watu wa nchi za magharibi. Naye Mkufunzi wa kozi ya uongozi na ujasiliamali, Mohamed Bassanga aliwahimiza wahitimu hao kufanyakazi kwa bidii huku wakimtegemea Mwenyezi Mungu katika jitihada zao.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close