Matukio

Aachana na ‘bollywood’ kwa ajili ya Allah!

“Mwanga!”, “Kamera!”, “Sauti!”, “Action”! Kwa mabinti  wengi wadogo nchini India, kukua na kuwa muigizaji wa filamu za Bollywood huwa ni ndoto yao kubwa.

Kujionyesha kifahari na kupendeza, hafla za kupeana zawadi, mavazi ya gharama kubwa, umaarufu na umashuhuri, hayo ndiyo mambo wanayotafuta kwa gharama yoyote ile.

Mmoja wa mabinti kama hao, ambao ndoto yake hiyo iligeuka na kuwa ya kweli alikuwa Zaira Wasim. Miaka mitatu tu iliyopita, Zaira Wasim, mwenye umri wa miaka 22, aling’ara katika filamu inayoitwa ‘Dangal’ iliyofanya vizuri mno katika historia ya filamu za Kihindi na kuingiza fedha nyingi.

Wiki mbili zilizopita, Zaira Wasim ameushitua ulimwengu wa Bollywood na mamilioni ya washabiki wake nchini India na ulimwenguni kote kwa kutangaza kwamba ameamua kurejea kwa Mwenyezi Mungu. Katika maelezo aliyoyaweka katika mtandao wa Facebook, msanii huyo mashuhuri wa filamu za Kihindi alitoa ya moyoni kuujulisha ulimwengu.

Maneno yaliyotoka kinywani mwa Zaira yalionekana kujaa majuto kwa makosa aliyoyafanya na kujisalimisha kiukweli kwa Muumba wake. Dada yetu huyu amefafanua jinsi alivyohangaika na imani yake katika ulimwengu uliojaa uchafu na uovu na kwamba alijiona hastahili kuwa kule.

Ni muhimu wanazuoni tusiwafanye vijana wetu wakajihisi wana madhambi mengi mno kiasi kwamba hakuna matumaini kwao.

Maneno haya yanaakisi kwa usahihi kabisa hisia za vijana wengi ambao wameupa mgongo mtindo wa maisha ya kifahari na kuponda raha. Dada yetu huyu katika Imani, amefafanua kwamba licha ya vishawishi vya umaarufu wake na mafanikio, alipata utulivu katika maneno ya Allah ‘Azza wa Jalla’.

Licha ya kozi nyingi za Kiislamu na matukio tunayoweza kuhudhuria, dada yetu huyu, kwa sentensi nyepesi kabisa, ametuonyesha maana halisi ya maneno yafuatayo ya Mwenyezi Mungu: “Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndiyo nyoyo hupata utulivu!” [Qur’an 13:28].

Katika posti ndefu ya Faebook ya dada Zaira, mambo matatu yanajitokeza: majuto, kumpenda Allah Ta’ala, na mapenzi kwa Qur’an. Kabla hatujaangalia kila moja kwa undani. Naomba mniwie radhi wasomaji wangu, siwezi kuwaletea ujumbe wote wa Zaira Wasim kama ulivyo, lakini nimeamua kufanya uchambuzi mdogo wa maeneo hayo matatu kwa sababu naamini yana mafunzo makubwa.

Kupotea kwa baraka
Wote tunafanya madhambi ya hapa na pale. Hakuna mwanaume au mwanamke aliye hai isipokuwa ameshawahi kukiuka baadhi ya Sharia za Allah ‘Azza wa Jalla’, lakini Mwenyezi Mungu asichotaka kutoka kwetu ni kudumu katika madhambi. Athari ya kung’ang’ania kufanya dhambi inageuza dhambi ndogo na kuwa kubwa, na gharama ya hiyo inaweza kuwa kupoteza baraka.

Kwa hiyo, baraka ni nini? Ni pale faida ya kiungu inapowekwa kwenye jambo kiasi kwamba uzuri wake unakua zaidi ya vile ilivyotarajiwa. Kwa mfano, unaweza kuwa na watu wawili wenye kiasi kinachofanana cha kipato, mmoja kwa njia ya halali na mwingine kwa haramu. Huyu wa pili anaweza kuwa na nyumba isiyo na furaha, wakati mwenzake anaweza kuwa na nyumba yenye upendo, furaha na vicheko. Tofauti ni nini? Baraka.

Kupoteza Dua ya Malaika
Tunapokuwa na matatizo, mara kwa mara tunawakimbilia watu ambao tunadhani wako safi ili watuombee dua – wazazi wetu, wanazuoni, masheikh wetu, na wengine kama hao. Lakini fikiria kwamba Malaika, ambao wameumbwa tu kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu, wakuombee dua wewe!

Tena hapa hatuzungumzii Malaika yoyote tu, bali wale maalumu ambao wana heshima ya kubeba kiti cha enzi cha Allah ‘Azza wa Jalla’ na kusema: “Mola wetu Mlezi! Umekienea kila kitu kwa rehema na ujuzi. Basi wasamehe waliotubu na wakaifuata Njia yako, na waepushena adhabu ya Jahannam.” [Qur’an, 40:7].

Tiba ya madhambi – toba
Katika Aya iliyopita, pia tumeona tiba ya madhambi yetu – toba. Lakini toba ni nini Toba ni kuomba msamaha na msingi wa kuomba msamaha ni kujuta. Toba ni hisia ya huzuni tunayopata ndani ya moyo kwa kushindwa kumtii Mwenyezi Mungu. Huo ni msingi wa Uislamu na ni wajibu: “Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.” [Qur’an, 24:31].

Kupitia toba ya dhati, lazima moyo mwepesi utaona ufunguo wa mafanikio katika maisha ya hapa duniani na ya kesho Akhera. Hiki ndiyo kitu ambacho dada yetu Zaira amekielewa kwa uwazi. Neno hapa kwa vijana wetu ni kwamba, tunahitaji kujipa changamoto ya kuwasiliana nao katika jukwaa na lugha wanayoielewa.

Tujibu maswali yale hasa wanayouliza, na siyo yale tunayotaka kuyajibu. Ni rahisi kwetu kubaki na kasumba ya kuwanukuu wanazuoni wa karne ya tatu na kuwafikishia vijana ujumbe bila ya kuangalia jinsi ya kufikisha ujumbe ule ule katika mazingira ya leo. Mara nyingi ujumbe huo mzuri hudondokea kwenye sikio lililokufa la vijana, ambao wameshatekwa na mastaa kama Drake, Riri, Diamond na wengineo.

Ni muhimu wanazuoni tusiwafanye vijana wetu wakajihisi wana madhambi mengi mno kiasi kwamba hakuna matumaini kwao. Isitoshe, wote tuna madhambi kwa viwango tofauti na ya aina tofauti. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Watoto wote wa Adam wanafanya madhambi na mbora wa wanaotenda madhambi ni wale wanaotubu.” [Tirmidhiy].

Bila shaka, kauli ya kishujaa ya muigizaji huyu wa Bollywood inaweza kuwa nukta nzuri ya kuanzia kujadili vipaumbele na malengo katika maisha haya na vijana wetu. Tusipoteze fursa hii adhimu. Kutoka mtenda dhambi na kuwa mtu mwingine, ni rahisi sana kuhisi hakuna matumaini. Kwa hakika, hicho ndicho shetani anachotaka kutoka kwako – kukata tamaa na dhambi zako! Huko pengine ni kufanya kosa kubwa zaidi kuliko madhambi yako yote yakikusanywa pamoja.

Unawezaje kukata tamaa na rehema za Mwenyezi Mungu wakati amesema katika Hadithi Qudsi: “Ewe mwana wa Adam, kwa kadri utakavyoniita na kuniomba, nita kusamehe kwa yale uliyofanya na  sintojali. Ewe mwana wa Adam, hata kama dhambi zako zingefika mawinguni na kisha ukaniomba msamaha, ningekusamehe. Ewe mwana wa Adam, hata ungekuja kwangu na mzigo wa madhambi kama Dunia, na kisha ukanielekea mimi, bila ya kunishirikisha na chochote, ningekupa msamaha takriban mkubwa kama huo.” [Tirmidhiy].

Tujikumbushe kidogo kuhusu wachawi wa Firauni. Hawa watu walikuwa wakifanya uchawi mweusi kwa hiyo dhambi zao lazima ziwe kubwa. Lakini, walipoona muujiza wa Musa (amani ya Allah imshukie), Allah ‘Azza wa Jalla’ alifungua nyoyo zao na wakauona ukweli, wakasujudu na kusema: “Ewe Mola Mlezi wetu! Tumiminie subira na utufishe hali ya kuwa ni Waislamu.” [Qur’an, 7:126].

Kujenga uhusiano na Allah
Kwa hiyo, kumjua Mwenyezi Mungu kwa usahihi na kujenga uhusiano na Qur’an vinakwenda pamoja. Ni kutoka kwenye Qur’an, usomaji wake na akisi yake, ndipo tunapoweza kujifunza kuhusu Mwenyezi Mungu. Maisha ni safari tu ya kumuelekea Allah ‘Azza wa Jalla’.Dada yetu Zaira siyo msanii wa kwanza kuachana na umaarufu na fedha. Sinead O’Connor, ambaye amechukua jina la Shuhada ni mmoja wa watu waliosilimu. Wasanii wengine mashuhuri ambao wameingia kwenye Uislamu ni pamoja na muimbaji na mtunzi wa nyimbo Cat Stevens, ambaye sasa anajulikana kama Yusuph Islam, Rapa Ice Cube, ambaye alisilimu miaka ya 1990.

Mwingine katika waliosilimu ni pamoja na na Mos Def ambaye alisema: “Ama unajipinda kwenye kazi yako, au matamanio yako. Kwa hiyo, njia bora ya kuishi maisha yako ni kujaribu kujipinda katika Swala, kwa Allah.” Zaidi, hatuwezi kumsahau mchekeshaji David Chappelle, ambaye aliingia katika Muislamu mwaka 1998 na kusema: “Kwa kawaida sizungumzii dini yangu hadharani kwa sababu sitaki watu wanihusishe mimi na upuuzi niliofanya na kitu hiki kizuri.”

Pia hatuwezi kumsahau mwanasoka wa kimataifa, Emmanuel Adebayo na vile vile nyota wa Rugby, Sonny Bill Williams, ambaye alisema: “Inanipa furaha. Imenifanya niwe mtulivu kama mwanaume na kunisaidia kukua. Sasa nina imani ndani yangu na imenisaidia kuwa hivi nilivyo leo.”

Tunaishi katika zama ambazo umaarufu unapendwa na watu maarufu wanaabudiwa. Hata hivyo, pengine hawa wasanii maarufu wametambua kwamba licha ya kuwa katika kundi la watu wanaokupenda, bado unaweza kujihisi uko mpweke, isipokuwa pale utakapoelewa na kujisalimisha kwa ukweli usiopingika kwamba roho inalilia kumjua Muumba wake. Mwenyezi Mungu anasema: “Je! Wakati haujafika bado kwa walioamini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyoteremka? Wala wasiwe kama waliopewa Kitabu kabla yao, muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikawa ngumu, na wengi wao wakawa wapotovu.” [Qur’an, 57:16].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close