4. Jamii

Waislamu wajitahidi kuchangia elimu ya madrasa

Katika makala iliyopita tuligusia changamoto za mfumo wa elimu ya madrasa zetu pamoja na malipo ya walimu wa vyuo hivyo. Wapo baadhi ya wasomaji wetu ambao walionesha kuguswa na habari hiyo na kushauri taasisi husika zichukue jitihada za kuondoa changamoto zinazokabili madrasa zetu nyingi hususani zile za ngazi za chini kabisa.

Kwa kuwa tuligusia masuala mengi ila leo tunapenda tukazie zaidi katika suala la michango kwa walimu wa madrasa tukiamini hili ni suala ambalo linawezekana kwa haraka kwani kikubwa ni utayari tu wa wazazi.

Mara kadhaa tumesema kuwa walimu hawa ndio wamebeba “roho” za vijana wetu wengi. Hawa ni watu ambao wana jukumu kubwa la kuwafundisha vijana hao elimu ya dini ya Kiislamu na kufahamu mafundisho yake.

Tulisema walimu wa madrasa ndio huwajenga vijana wetu kimaadili na kiimani. Na vijana hao ndio tunawategemea hapo baadae waje kuwa masheikh, viongozi wetu na kadhalika. Watu husema ili jamii iwe na utulivu, amani na maadili basi hakuna budi vijana wadogo wakajengwa kwenye mstari ulionyooka hususani wa dini.

Lakini kwa bahati mbaya, wengi wa walimu hawa wamekuwa hawathaminiwi kama inavyostahili. Wengi wa walimu hawa wanaishi katika mazingira magumu kutokana na kipato kidogo wanachopata. Ni kweli tunahimizwa kujitolea kwa kwa ajili ya dini yetu ili kupata thawabu toka kwa Muumba wetu, lakini kwa upande mwingine walimu hawa wanafamilia zinazohitaji huduma muhimu.

Huduma kama za vyakula, mavazi na malazi, kwani wapo wengine wamepanga na wanalipa kodi. Hayo ni baadhi tu ya mahitaji ila yapo mengine tu. Hivyo mahitaji hayo ni muhimu kwa walimu kwa sababu bila hivyo ni vigumu kuwa katika mazingira mazuri ya wao kutoa elimu kwa vijana wetu.

Sote tunafahamu mtu anaekabiliwa na shida kama za ukosefu wa mahitaji ya msingi ya mwanadamu hawezi kutimiza jukumu lake ipasavyo. Na walimu wanapoyapata mahitaji hayo inawajengea mazingira mazuri ya wao kutoa elimu stahiki kwa vijana wetu, kwa lugha nyingine tunasema inawafanya wahisi kuwa na wajibu mkubwa.

Tena ni jambo la kusikitisha na la ajabu eti mtoto anapomwambia mzazi wake kuwa mwalimu wa madarasa anahitaji ada na michango mingine, basi wazazi wengi huja juu na kusema hao walimu wenu nao kila siku wanataka hela tu! Ila wakati huo huo wanapoombwa hela za mafunzo ya ziada “Tuition” wengi wa wazazi hao hufanya hivyo haraka na kuhakikisha mtoto hakosi kwenda darasani.

Wao wanaona elimu ya mazingira ndio pekee ina manufaa kwa vijana wao kuliko elimu ya dini. Kwa maana kuwa itamuwezesha kuajiriwa hapa dunini na kupata kipato. Wanasahau kuwa nayo elimu ya dini ni muhimu kwa vijana wao kwani inampa muongozo bora hapa duniani na kuwa na manufaa baada ya kufariki.

Ukiachia hilo tu, wapo watu wengi tu leo waliosoma elimu ya dini na wameajiriwa au kujiajiri na wana kipato kizuri tu. Tukirejea kwa walimu, hapo juu tumeona umuhimu wao, hivyo tunauasa umma wa kiislamu kuwajali na kuwa heshimu walimu hao.

Pia tunauasa umma ujitahidi kutoa ada na michango mingine pale inapohitajika ili kuwawezesha walimu hawa wawe ni watu wenye uwezo wa kijikimu na wao kuona thamani ya kazi yao.

Ili kusoma makala iliyopita kuhusu kuchangia elimu ya madrasa bonyesha kiungo hiki👇

Wazazi wa Kiislamu tulipe michango ya madrasa

Tags
Show More

Related Articles

Check Also

Close
Back to top button
Close