4. Jamii

Usia wa Mtume (saw) kwa vijana

Kutoka kwa Alqama amehadithia kuwa, alikuwa anatembea na Abdullah bin Masoud [Allah amridhie] ndipo walipokutana na Uthman bin Affaan [Allah amridhie]. Hapo walisimama wakazungumza naye. [Uthman] Akasema: “Ewe Abuu AbdirRahman kwanini tusikuozeshe kijakazi huenda akawa anakukumbusha baadhi ya yale yaliyokupita.” Abuu AbdirRahman [bin Masoud] akasema: “Ama ikiwa utasema hivyo, kwa hakika Mjumbe wa Allah [rehema za Allah na amani zimshukie] alishatuambia,

Enyi kundi la vijana mwenye uwezo miongoni mwenu wa kuoa basi na aoe, kwani ndoa husaidia kuinamisha macho, na kuhifadhi utupu, na yule asiyeweza basi ni juu yake kufunga kwani funga ni kinga kwake yeye [kwa kupunguza matamanio ya kimwili]’” [Bukhari na Muslim].

Tukio hili linatupa mafundisho kadhaa. Kwanza, tunajifunza upendo uliokuwepo baina ya Wema Waliotangulia na namna walivyokuwa wakiusiana na kusaidiana katika mazuri yaliyoweza kuwapa nguvu ya kutekeleza majukumu yao na kumuabudu Allah ipasavyo.

Tunamuona Uthman [Allah amridhie] akimhamasisha Ibn Masoud kuoa, lakini pia anataka yeye [Uthman] kusimamia jambo hilo la kumuozesha, ikiwa Ibn Masoud atakuwa tayari.

Kuhamasishana katika jambo la ndoa Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] amewaachia usia muhimu sana vijana wa umma huu, ambao utawakinga na kuwasaidia kuepuka mengi iwapo watashikamana nao. Huu ni usia wa kuoa, ambao kwa bahati mbaya vijana wengi, na hata wazazi na walezi, wameupuuzia.

Jambo la Ndoa limezingirwa na utamaduni na desturi za miji ambazo zimelifanya kuwa gumu na zito kiasi cha kuwafanya baadhi ya vijana waogope, walifumbie macho na kueneza ufisadi katika ardhi kwa kufanya machafu ya aina mbalimbali.

Ndoa ni kinga

Ni vema kijana akatambua kuwa ndoa ndio silaha nyepesi na rahisi itakayomsaidia kupambana na matamanio ambayo ni sehemu ya maumbile ya kibinadamu; na ni vema kijana akaharakia kuoa kadiri utakavyoweza kwani hakuna katika zama hizi jambo bora la kumwezesha kuepuka maasi kama ndoa.

Kijana atakapoona chochote kikaamsha hisia za matamanio katika nafsi yake, ataelekea kwa mkewe na kupooza matamanio hayo, lakini iwapo hana pakutuliza matamanio katika zama
hizi zilizojaa fitna za aina mbalimbali, atayumba na kuangukia katika maasi. Zama hizi, mazingira yamebadilika. Nyenzo za maasi zimekuwa nyingi. Unapotazama mara nyingi, macho yanaangukia katika haramu, masikio nayo yatasikia haramu. Hata ukiwa peke yako, moyo unagubikwa na fikra za mambo ya haramu na dhambi.

Vijana wengi wamekuwa wanahamsha hisia za matamanio lakini baada ya hapo hawawezi kuzipooza au kuzizuia. Hilo limesababishwa na kupuuza usia huu wa Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie]. Haya matamanio hayapigwi vita bali yanatakiwa yabakie kwa ajili ya manufaa ya umma wa kiislamu, yawekwe mahala panapostahiki ili vipatikane vizazi vinavyomtambua Allah na kuitetea dini yake kwa mwenendo wa Mtume[rehema za Allah na amani zimshukie].

Uwepo wa matamanio na fitna za aina mbalimbali ni sehemu ya maisha ya Muumini ili kudhihirisha umadhubuti na uimara wa imani yake.

Kujibidisha katika funga za Sunna

Watu wengi, hususan vijana wanajitahidi kufunga Ramadhani kwasababu ni funga ya lazima [faradhi] lakini wanapuuza funga za Sunna. Tuelewe kuwa, pamoja na thawabu na fadhila za funga za sunna, pia ipo faida ya kudhoofisha, kuyadhibiti na kuyabana matamanio ya nafsi na mapito ya shetani. Hivyo basi, ni muhimu sana kujibidisha kufunga sunna, ili kupata malipo bora kwa Allah na kujizuia na machafu.

Weka akiba ya afya yako kwa kujizuia na haramu ili uzidi kuimarika na kusalimika na maradhi au udhaifu wa mwili unaotokana na kuyaendea maovu. Harakisha katika kuyaendea maisha ya ndoa kwani faida zake ni nyingi na manufaa yake yanarejea kwako kwa jamii na kwa umma kiujumla.

Kadhalika, zuia macho yasitazame haramu na masikio yasisikilize haramu kwani hiyo ni sababu ya kukufanya usiyaendee. Haramu inayokatazwa kutazamwa au kusikiliza ni pamoja na miziki ambayo sehemu kubwa inahamasisha mapenzi na mahusiano yasiyokuwa ya kisheria. Vijana wengi wameingia katika makundi haya ya wapenda miziki na kuwa katika michanganyiko mibaya ya wanaume na wanawake, jambo ambalo linahatarisha usalama wa imani yao, na matendo yao.

Ujana ni mtihani

Ujana ni ngazi miongoni mwa ngazi anazopitia mwanadamu katika maisha yake. Katika ujana, mtu huwa na mipango mingi na matumaini makubwa, hadi hughafilika. Kikwazo kingine kikubwa kwa vijana ni kutochukua hatua za haraka na za papo hapo katika muda muafaka za kubadilisha mwelekeo wa maisha yao, na badala yake husema ‘Nitafanya.’ Wengi wanasema ‘nitaoa,’ ‘nitatubu,’ ‘nitaswali,’ ‘hamna neno nitabadilika;’ Kauli ambazo ni bahari isiyokuwa na mwisho. Waliozama katika bahari hii ni wengi mno, wamekuwa wakisema ‘nitafanya’ mpaka wamekufa. Hawakupata muda wa kufanya.

Walipofikisha miaka 30 walisema nitatubu nikifikisha 40, walipofikia 40 wakasema ikifika 50. Walisahau kuwa, kila kukicha kifo kilikuwa kinawakaribia na makaburi yalikuwa yakiwangoja, hatimaye wakaingia makaburini na huku wakiwa na yale matumaini ya ‘nitafanya.’

Tags
Show More

Related Articles

Check Also

Close
Back to top button
Close